Sunday, 6 August 2017

Bi KHADIKA KAMA MALKIA WA MAQRAISHI

Bi KHADIKA KAMA MALKIA WA MAQURAISHI
Assalaam Alaykum.
Khadija alikuwa mtu wa nyumbani, pia ndugu zake na binamu zake hawakupenda kusafiri na misafara. Kwa hiyo, alimuajiri wakala wakati wowote msafara ulipotoka kwenda nje (ya Hijazi), na kumfanya wakala huyo kuwa na madaraka ya kupeleka bidhaa zake kwenye masoko ya nje kuziuza huko. Kwa uwezo mzuri wa kuteua mawakala, na kununua na kuuza wakati na mahali muafaka aliweza kupata faida kubwa sana, na baadaye, akawa mfanyabiashara tajiri sana wa Makka.
Ibn Sa'ad anasema kwenye Tabqaat yake kwamba misafara ya wafanya biashara wa Makka ilipoanza safari, mzigo wa Khadija peke yake ulikuwa sawa na mizigo ya wafanyabishara wengine wote wa Qurayish katika msafara huo. Alikuwa dhahiri kwa kila mtu ni kama msemo "golden touch" ("mguso wa dhahabu") yaani kila atakacho kigusa hata kama ni vumbi litageuka kuwa dhahabu. Watu wa Makka, katika hali hiyo, walimpa jina la Malkia wa Qurayish. Aidha walimwita Malikia wa Makka.

MUBAHALA (MAAPIZANO KATI YA MTUME NA WAKRISTO)

MUBAHALA (MAAPIZANO KATI YA MTUME NA WAKRISTO)
Assalaam Alaykum.
Kabla hatujaingia ndani kuzungumzia suala la Mubahala, kwanza ni vizuri tufahamishe maana ya Mubahala. Muhabala ni: Kuapizana. Ujumbe wa Kikristo kutoka Najran ulifika kwa Mtume kujadili suala la Nabii Isa (a.s.). Mtume aliwajulisha kuwa: Hakika mfano wa Isa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam, aliumbwa kwa udongo kisha akamwambia: Kuwa naye akawa. (3:59).
Kwa kuwa Nabii Isa alizaliwa bila baba, Wakristo wamedhani kuwa baba yake ni Mwenyezi Mungu. Aya hii inaondoa dhana hiyo ambayo inapingana na utukufu wa Mwenyezi Mungu, na inawapigia mfano wa ajabu zaidi katika kuumbwa Adam bila ya baba wala mama. Aliumbwa kwa udongo kisha akaambiwa: kuwa naye akawa, na kwa neno hilo hilo Nabii Isa (a.s) ndivyo alivyoumbwa.
Ujumbe huo ulipokuwa haukukubaliana na hoja hii, Mwenyezi Mungu akateremsha Aya:- "Na atakayehojiana nawe (Muhammad) katika hili baada ya ujuzi uliokufikia, waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu, na nafsi zetu na nafsi zenu, kisha tuombe kwa kunyenyekea tuijaalie laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie wenye kusema uongo." (3:61).
Hili lilikuwa tarehe ishirini na nne mfungo tatu mwaka wa kumi. Mtume akawaita ili waanze kuapizana. Wakajibu:- "Ngojea tujadiliane". Walipokwenda faragha, wakamuuliza Askofu Abdul Masih; ana Maoni gani katika suala hili? Akajibu:- Enyi Wakristo: Wallahi nyinyi mnajua kuwa Muhammad ni Nabii aliyeletwa na amekuja na ushahidi ulio wazi juu ya jambo la huyu (Yesu a.s.). Wallahi hakuna watu walioapizana na Nabii wakasalimika, ikiwa mtaapizana naye mtaangamia".
Askofu Peter yeye aliwaambia: "Enyi Wakristo: Mimi naziona nyuso hizi (kundi la Mtume) kama zitamuomba Mwenyezi Mungu auondoe mlima kutoka mahala pake, Wallahi atauondoa. Msiapizane naye mtaangamia, na hatabaki Mkristo ye yote hapa duniani mpaka siku ya Kiama".
Alipoulizwa Ahtam, akawaambia: Niacheni nikamuulize Muhammad, alipomkabili Mtume akamuuliza, "Ewe Abulqasim'! Unatoka na kina nani kwa ajili ya maapizano haya?" Mtume (s.a.w.) akamjibu: "Ninaapizana nanyi nikiwa na watu bora hapa duniani na watukufu mno mbele ya Mwenyezi Mungu, nao ni hawa (akawaonyesha) Ali, Fatima, Hasan na Husein."
Taarifa ya kikosi hicho cha Mtume (s.a.w) ilipowafikia wakaogopa kuapizana na Mtume, na badala yake wakaomba sulhu kwa Mtume (s.a.w.) kwa kutoa dirham arobaini elfu.
TAZAMA: 
Tarikh Ibn Athir J.2 Uk. 200 
Tafsirul Qurtubi J.4 Uk. 104 
Tafsirul Ibn Kathir J.1 Uk. 376-379 
Tafsirul Khazin J.1 Uk. 359-360 
Tafsirul Maragh J.3 Uk. 175 
Tafsirul Kabir J.8 Uk. 81 
Zadul Masir J.1 UK. 399
Katika Ayatul Mubahala, iliposema:- "Tuwaite watoto wetu" Mtume (s.a.w.) alimwita: Hasan na Husein. Iliposema: "Na wanawake wetu" Mtume (s.a.w.) alimwita: "Fatima bint Muhammad". Iliposema: "Na nafsi zetu" mtume akamwita: "Ali". Kwa hivyo Ali bin Abi Talib ni nafsi ya Mtume Muhamad (s.a.w.).
Tukio hili Ia Mubahala tukilitazama kwa upande wa pili, linatukumbusha lile tukio la "KlSAA" Iliposhuka Ayatut Tat'hir:- Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba (ya Mtume) na (anataka) kukutakaseni sana sana" (33:33). Iliposhuka Aya hii Mtume alimchukua Ali na Fatima na Hasan na Husein, akawafunika nguo kisha akasema: "Ee Mola! Hawa ni watu wa nyumba yangu, basi waondolee uchafu na uwatakase sana sana." Mama Ummu Salama (mke wa Mtume) alipotaka kuingia humo, Mtume (s.a.w.) akamzuia:
Kama ambavyo kwenye tukio la Mubahala ulipofika wakati wa kuomba maombi maalumu kwa ajili ya maapizano kati yake na Wakristo wa Najran, Mtume alimchukua Ali na Fatima na Hasan na Husein tu. Ingawa wakati huo Mtume (s.a.w.) alikuwa nao wakeze, na Masahaba ambao ni marafiki zake pia, lakini hapa hawakuingia. Wake za Mtume na Masahaba hawakuingia katika "KISAA" na hawakusimama katika uwanja wa Mubahala, kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwahusisha darja hii Ahlul Bait tu peke yao.
TAZAMA: 
Tafsirul Khazin J.3 Uk. 259 
Tafsirul Ibn Kathir J.3 Uk. 494 
Tafsirul Qurtubi J.14 Uk. 183 
Zadul Masir J.6 Uk. 381

MNAJIMU

MNAJIMU
Kiongozi wa Waumini, Ali mwana wa Abu Talib (a.s) na jeshi lake juu ya migongo ya farasi walikuwa wakaribia kuelekea Nahrwan.
Ghafla mmoja katika wafuasi wake maarufu alimjia na bwana mwingine akisema: “Ewe kiongozi wa waumini, huyu bwana ni mtabiri na ana jambo la kukueleza.” Mtabiri huyo akasema: “Ewe kiongozi wa waumini, si vizuri nyinyi kusafiri wakati huu, tafadhali subirini masaa mawili au matatu ya siku yapite kisha muendelee na safari yenu”.
“Kwa nini?”
“Kwa sababu nyota zinatuambia kuwa mtu yeyote ambaye atasafiri nyakati hizi atashindwa na adui yake. Yeye na wafuasi wake watapata shida kubwa. Lakini mkisafiri wakati ambao nimependekeza mtashinda na mtafaulu katika kufikia lengo lenu.”
Imam akasema, “Farasi wangu anatarajiwa kupata mtoto unaweza kuniambia atakayezaliwa atakuwa farasi wa kiume au wa kike?”
“Nikifanya hesabu naweza kueleza”
“Unasema uwongo, kwa wewe haiwezekani, kwa sababu imeandikwa katika Qur’an, ‘Hakuna yeyote isipokuwa Allah anayejua kuhusu mambo yaliyofichikana, na pia ni Mwenyezi Mungu peke Yake ambaye anaejua ni nini kilichobebwa (kiume ama kike) katika tumbo la mama.’ Hata Mtume wa Mungu (Muhammad (s.a.w.w) hakuwahi kudai jambo kama hili unalodai. Unadai kuwa una elimu yote kuhusu dunia hii? Na je, unajua wakati mtu ana bahati nzuri ama mbaya katika majaaliwa yake? Kama mtu yeyote anakuamini na kuamini mambo yako, basi hamhitajii Mwenyezi Mungu kabisa.”
Baada ya hayo yote imam Ali (a.s) aliwaambia wale watu wengine waliobaki: “Tambueni! Msifuate mambo kama haya, yanamfanya mtu kuamini yasiyoonekana na ni kama mtabiri ama mchawi. Na mchawi ni kafiri na kafiri ni wa motoni.”
Baada ya hayo aliziangalia mbingu na akasema maneno machache ambayo yalikuwa yanahusu imani yake kwa Allah (s.w.t).
Kisha alimwangalia yule mtabiri na akasema “Kwa makusudi nitakwenda kinyume na ushauri wako na tutaondoka sasa hivi bila kuchelewa.” Mara baada ya maneno hayo aliwaamuru wafuasi wake waanze safari.
Waliondoka kuelekea kwa maadui. Kama ilivyolinganishwa na vita vya jihad vingine, katika Jihad hii, Imam (a.s) alifaulu ajabu na kupata ushindi mkubwa.