Sunday 6 August 2017

MNAJIMU

MNAJIMU
Kiongozi wa Waumini, Ali mwana wa Abu Talib (a.s) na jeshi lake juu ya migongo ya farasi walikuwa wakaribia kuelekea Nahrwan.
Ghafla mmoja katika wafuasi wake maarufu alimjia na bwana mwingine akisema: “Ewe kiongozi wa waumini, huyu bwana ni mtabiri na ana jambo la kukueleza.” Mtabiri huyo akasema: “Ewe kiongozi wa waumini, si vizuri nyinyi kusafiri wakati huu, tafadhali subirini masaa mawili au matatu ya siku yapite kisha muendelee na safari yenu”.
“Kwa nini?”
“Kwa sababu nyota zinatuambia kuwa mtu yeyote ambaye atasafiri nyakati hizi atashindwa na adui yake. Yeye na wafuasi wake watapata shida kubwa. Lakini mkisafiri wakati ambao nimependekeza mtashinda na mtafaulu katika kufikia lengo lenu.”
Imam akasema, “Farasi wangu anatarajiwa kupata mtoto unaweza kuniambia atakayezaliwa atakuwa farasi wa kiume au wa kike?”
“Nikifanya hesabu naweza kueleza”
“Unasema uwongo, kwa wewe haiwezekani, kwa sababu imeandikwa katika Qur’an, ‘Hakuna yeyote isipokuwa Allah anayejua kuhusu mambo yaliyofichikana, na pia ni Mwenyezi Mungu peke Yake ambaye anaejua ni nini kilichobebwa (kiume ama kike) katika tumbo la mama.’ Hata Mtume wa Mungu (Muhammad (s.a.w.w) hakuwahi kudai jambo kama hili unalodai. Unadai kuwa una elimu yote kuhusu dunia hii? Na je, unajua wakati mtu ana bahati nzuri ama mbaya katika majaaliwa yake? Kama mtu yeyote anakuamini na kuamini mambo yako, basi hamhitajii Mwenyezi Mungu kabisa.”
Baada ya hayo yote imam Ali (a.s) aliwaambia wale watu wengine waliobaki: “Tambueni! Msifuate mambo kama haya, yanamfanya mtu kuamini yasiyoonekana na ni kama mtabiri ama mchawi. Na mchawi ni kafiri na kafiri ni wa motoni.”
Baada ya hayo aliziangalia mbingu na akasema maneno machache ambayo yalikuwa yanahusu imani yake kwa Allah (s.w.t).
Kisha alimwangalia yule mtabiri na akasema “Kwa makusudi nitakwenda kinyume na ushauri wako na tutaondoka sasa hivi bila kuchelewa.” Mara baada ya maneno hayo aliwaamuru wafuasi wake waanze safari.
Waliondoka kuelekea kwa maadui. Kama ilivyolinganishwa na vita vya jihad vingine, katika Jihad hii, Imam (a.s) alifaulu ajabu na kupata ushindi mkubwa.

No comments:

Post a Comment