Monday, 16 November 2015

BINTI WA NABII MUHAMMAD (s.a.w.w.)

BINTI WA NABII MUHAMMAD (s.a.w.w.)

Yeye  ni  Fatima  Zahra; Baba yake ni Rasulullah (Mjumbe na Mtume wake Mwenyezi Mungu) Muhammad bin Abdullah (s.a.w.w.); na mama yake ni Bibi Mtukufu Khadija Mama wa Waislamu, na mumewe ni bwana wa mawasii Ali Ameerul-Muuminiin, na watoto wake na wajukuze ni maimam watoharifu (juu yao Rehma na Amani).
Alizaliwa Bibi Fatima (a.s.) siku ya mwezi ishirini, mwezi wa mfungo tisa, mwaka wa arobaini na tano toka alipozaliwa Mtume (s.a.w.w).
Na akafa bibi huyo siku ya Jumanne mwezi tatu, mfungo tisa, mwaka wa kumi na moja wa Hijiria [5]. Na umri wake ni miaka kumi nanane.
Na akasimamia matendo ya kifo chake Amirul Muminiin Ali (a.s.), akamzika Madina Munawwara (Mji wenye nuru, mji wake Mtume, uliopo katika Saudia Arabia), na akalificha kaburi lake kama alivyo usia mwenyewe Bibi Fatima.
Alikuwa bibi huyo kama baba yake kwa ibada na kumcha Mungu na ubora, na zimeshuka katika sifa zake aya nyingi za Qur'ani al-Hakim.
Alikuwa Mtume (s.a.w.w.) akimwita "Bibi wa wanawake wa Ulimwenguni", na akimpenda mapenzi mazuri mpaka yeye akiwa anaingia kwa Mtume (s.a.w.w.) humkaribisha na kusimama na kumkalisha mahali pake, pengine humbusu mikono yake.
Na Mtume (s.a.w.w.) akasema: "Mungu huridhika analoridhika nalo Fatima na hukasirika Unalo mkasirisha Fatima."
Pia Mtukufu Mtume amesema: "Wabora wa wanawake wa peponi ni wanne: Mariam Binti Imrani, na Khadija Binti Khuwailid, na Fatima Binti Muhammad (s.a.w.w.) na Asia Bint Muzaahim.
Mtu mmoja akamwuliza bibi Aaisha "Mtu gani alikuwa mpenzi mno wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.)? Akajibu: Fatima.
Kisha akamwuliza: Ni gani kutokana na wanaume? Akajibu: Mume wake Bibi Fatima, yaani Ali bin Abi Talib (as.).
Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) akasema: "Hakika, Mwenyezi Mungu ameniamrisha mimi nimwoze Fatima kwa Ali (a.s.).
Kazaa bibi huyo kwa Amirul Muuminiin Ali (a.s.): Imam Hassan (a.s.), Imam Hussein (a.s.), Bibi Zainab (a.s.), Bibi Ummu Kulthum (a.s.) na Muhsin (a.s.)- Lakini bwana Muhsin kafa tumboni zama alipopata mama yake msukosuko wa maadui. Kwa hiyo jumla ya watoto wa bibi Fatima ni 5.
Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) amesema: "Kila mtoto huchukuwa ukoo wa baba yake isipokuwa vizazi vya Fatima, kwani mimi ndiyo walii wao na nasaba wao (yaani, vizazi vya Fatima wote ukoo wao unatokana kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Pia Mtume Mtukufu amesema:- "Kila ukoo na uhusiano utafutika siku ya qiyama isipokuwa ukoowangu na uhusiano wangu.

JANNAT AU PEPO

JANNAT AU PEPO
Assalaam alaykum.
Jannat ni mahala pema kabisa ambapo Allah (s.w) amewaandalia watendao mema na kujiepusha na maovu.
Katika ukurasa wa 279, juzuu 13 ya kitabu Lisan al-'Arab, twaambiwa kuwa pepo inaitwa Jannat 'Adan ikimaanisha kuwa ni "Mahala pa milele", Bustani ya Kati (al-awsat)."
Kitabu hichohicho kinatutambulisha katika uk.427, juzuu ya 7 kuwa al-awsat inaweza kumaanisha kuwa: iliyo Bora. Hakuna shaka kuwa tutaweza kuona na kupata maelezo na mafafanuzi zaidi juu ya Jannat 'adan kuliko kusema tu al-firdows, Jannat au Peponi, katika Qur'an Tukufu. Hali hii inatuacha sisi kwa kudadisi kuwa mahala bora kabisa, na iliyokuu, inayolengwa katika Jannat zote ni Jannat 'Adan.
Peponi, au al-Firdows kama vile inavyoitwa katika Kiarabu, ni neno la kuazimwa. Waarabu aliowatokezea Mtume Muhammad (s.a.w.w.) walikuwa hawana itikadi ya maisha baada ya kufa, na Jannat na Jahannam. Na kwa hakika swala hili lilikuwa gumu kwake Mtume (s.a.w.w.) alipoanza kuhubiri. Sura-i-Yasin, 36, Ayah ya 78 inatuelezea, 'Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake - akasema: "Nani atakayeihuisha mifupa na hali imesagika?"
Vile vile Qur'an inatujibu katika, Sura Ya-Sin, 36; Ayah 79: Sema: "Ataihuisha yule aliyeiumba mara ya kwanza, naye ni Mjuzi wa kila (namna ya) kuumba"
Hata mwandishi wa kazi nzuri kabisa za Kiarabu, Lisan Al-'Arab, hana uhakika iwapo neno hili la Firdaws limeazimwa kutoka Kilatini au Kiajemi, au ni al-Majlisi, kama mwandishi huyo anavyokubali katika uk. 91, Juzuu ya 8 kati ya Juzuu 110 ya Encyclopedia - bila ya kuihesabu Juzuu ya Sifuri - ijulikanayo kwa jina la Bihar al-Anwar. Wazo la tatu, ambalo linaweza kuwa sahihi zaidi ni kwamba inawezekana uasili wake ukawa Babilonia.
Neno lingine lililotumika katika Qur'an Tukufu ni Jannat au Bustani. Lakini kwetu sisi Jannat inamaanisha sana kuliko kutaja Bustani au shamba la miti ya matunda. Waarabu kamwe hawakuwa na tabia ya kuishi katika mshamba yao ya miti ya matunda.
Mtume (s.a.w.w) anasema, "Wakati Allah (sw) aliponiruhusu kwenda Jannat, Jibrail a.s. aliniambia, "Mimi nimeamrishwa kukutembeza na kukuonyesha yote yaliyomo ndani mwa Jannat na Jahannam." Hivyo mimi niliiona Jannat na baraka na mema yote yaliyokuwamo na vile vile nimeiona Jahannam pamoja na mateso yote yaliyomo. Jannat inayo milango minane, kila mlango unayo misemo minne, ambayo kila mojawapo ni bora kuliko ulimwengu mzima na kile ambacho kipo ndani mwake ni kwa ajili ya wale wanaotafakari na kufuatilia kwa kutenda kimatendo.
Na Jahannam inayo milango saba, na kila mlango inayo misemo mitatu, ambapo kila msemo ni afadhali kuliko dunia yetu hii na kilichomo ndani mwa kila msemo ni kwa ajili ya kutafakari na kuyatendea kazi. Malaika Jibraili (a.s.) aliniambia, "Ewe Muhammad! Soma yaliyoandikwa katika milango hii!" Na hivyo mimi niliyasoma yote.
Ufafanuzi zaidi utakujia baadaye Insha – Allah

Thursday, 12 November 2015

HALI NA HAKI ZA MTOTO KATIKA UISLAMU

HALI NA HAKI ZA MTOTO KATIKA UISLAMU
Umoja wa mataifa umeanza kuonyesha kuvutiwa na suala la watoto kwa kufanya maadhimisho ya ‘Siku ya Watoto’ katika mwezi wa Novemba kila mwaka, ambayo inalingana na maadhimisho ya kutangazwa kwa haki za mtoto.
Ukweli ni kuwa mazingatio ya Uislamu kwa watoto yameanza zamani na yanarejea nyuma zaidi ya miaka elfu moja na mia nne.
Uislamu kwa mfululizo unaadhimisha na kuonyesha huruma yake kwa mtoto, si baada ya kuzaliwa tu, bali hata kabla ya kuzaliwa, na umeelezewa kwa makini haki zake.
Wakati wa utoto katika Uislamu umepewa picha ya ulimwengu mzuri wa furaha, uzuri, ndoto, mapenzi na ndoto njema.
Na aya za Qur’ani zinaonyesha mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa watoto, na ndipo akaapa Mwenyezi Mungu: “Naapa kwa mji huu, (wa Makkah).  Na wewe utahalalishwa katika mji huu. Na (kwa) mzazi na alichokizaa.” (90:1-3).
Watoto wameelezwa katika Qur’ani kuwa ni bishara njema. Amesema Mwenyezi Mungu:
 “Ewe Zakaria tunakupa habari njema ya (kupata) mtoto jina lake ni Yahya….” (19:7).
Pia watoto ni kiburudisho cha macho yetu. Amesema Mwenyezi Mungu:
 “Ewe Mola wetu, tupe katika wake zetu na watoto wetu watakaoyaburudisha macho yetu….”(25:74).
Na watoto ni pambo la maisha katika ulimwengu huu: “Mali na watoto ni pambo la maisha ya duniani….” (18:16).
Mtume (s.a.w.) anatudhihirishia ya kuwa ulimwengu wa utoto ni kama pepo, pale aliposema: “Watoto ni vipepeo vya Peponi.”
Kuwatunza watoto ni jambo la lazima, na kuwapenda humleta mtu karibu na Mwenyezi Mungu. Mtume (s.a.w.) amesema: “Lau kama si watoto wanyonyeshwao, na wazee wanaorukuu (kwa kuswali) na wanyama walishwao mashambani, basi mngelipatwa na adhabu kali.”
Inaonyesha wazi kwamba huruma na uangalifu wa Mwenyezi Mungu kwa watoto ndiyo uliofanya Mwenyezi Mungu kuzuia adhabu juu ya watu wake.
  1. Mapenzi Ya Mtume Kwa Watoto
Mapenzi ya Mtume (s.a.w.) kwa watoto yalijaa ndani ya moyo wake mwema, imeelezwa katika Hadith: “Siku moja Mtume (s.a.w.) alipanda juu ya mimbari akiwahutubia watu, (mara) akawaona Hasan na Husein (a.s.) wanakimbia na huku wakijikwaa, akakatiza hotuba yake, akashuka kutoka juu ya mimbari kwenda kuwapokea watoto hao wawili. Akawabeba mikononi mwake, kisha akapanda tena juu ya mimbari akasema: “Enyi watu, hakika mali zenu na watoto wenu ni fitina, Wallahi nimewaona wajukuu wangu wawili wakikimbia na kujikwaa, basi sikuweza kujizuia mpaka nimeshuka nikawabeba.”
Siku moja Mtume (s.a.w.) alikuwa anaswali, mara Hasan na Husein (a.s.) wakaingia ndani na kumpanda mgongoni kwake wakati alipokuwa amesujudu, Mtume (s.a.w.) akaendelea kusujudu tu. Alichukia kuwaharakisha washuke, mpaka waliposhuka wao wenyewe. Kisha alipotoa salaam na kumaliza Swala, akaulizwa na maswahaba wake sababu zilizomfanya asujudu kwa kitambo kirefu hivyo; akawajibu: “Wajukuu wangu wawili walikuwa wamepanda juu ya mgongo wangu nami nilichukia kuwahimiza washuke kwa haraka.”
Mtume (s.a.w.) alizoea kuharakisha Swala yake pindi asikiapo mtoto analia, na husema: “Mimi huchukia kumchosha mama yake.”
Siku moja alikuwa anapita nyumbani kwa Fatima (a.s.) (binti yake), akamsikia mjukuu wake Husein (a.s.) akilia, aliingia ndani na baada ya kumkemea Fatima akasema: “Je hujui kwamba nimsikiapo Husein akilia huwa nakereka?”
Siku moja Mtume (s.a.w.) alitembelewa na Al-Akraa Ibn Habis, ambaye alimwona Mtume (s.a.w.) akiwabusu wajukuu zake, Al-Akraa akasema: “Unawabusu watoto wa binti yako? Naapa kwa Mungu nina watoto kumi, na sijawahi kumbusu hata mmoja.”
Mtume (s.a.w.) akamjibu: “Je ni kosa langu kama Mwenyezi Mungu ameing’oa rehma kutoka moyoni mwako.”