Thursday, 12 November 2015

HALI NA HAKI ZA MTOTO KATIKA UISLAMU

HALI NA HAKI ZA MTOTO KATIKA UISLAMU
Umoja wa mataifa umeanza kuonyesha kuvutiwa na suala la watoto kwa kufanya maadhimisho ya ‘Siku ya Watoto’ katika mwezi wa Novemba kila mwaka, ambayo inalingana na maadhimisho ya kutangazwa kwa haki za mtoto.
Ukweli ni kuwa mazingatio ya Uislamu kwa watoto yameanza zamani na yanarejea nyuma zaidi ya miaka elfu moja na mia nne.
Uislamu kwa mfululizo unaadhimisha na kuonyesha huruma yake kwa mtoto, si baada ya kuzaliwa tu, bali hata kabla ya kuzaliwa, na umeelezewa kwa makini haki zake.
Wakati wa utoto katika Uislamu umepewa picha ya ulimwengu mzuri wa furaha, uzuri, ndoto, mapenzi na ndoto njema.
Na aya za Qur’ani zinaonyesha mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa watoto, na ndipo akaapa Mwenyezi Mungu: “Naapa kwa mji huu, (wa Makkah).  Na wewe utahalalishwa katika mji huu. Na (kwa) mzazi na alichokizaa.” (90:1-3).
Watoto wameelezwa katika Qur’ani kuwa ni bishara njema. Amesema Mwenyezi Mungu:
 “Ewe Zakaria tunakupa habari njema ya (kupata) mtoto jina lake ni Yahya….” (19:7).
Pia watoto ni kiburudisho cha macho yetu. Amesema Mwenyezi Mungu:
 “Ewe Mola wetu, tupe katika wake zetu na watoto wetu watakaoyaburudisha macho yetu….”(25:74).
Na watoto ni pambo la maisha katika ulimwengu huu: “Mali na watoto ni pambo la maisha ya duniani….” (18:16).
Mtume (s.a.w.) anatudhihirishia ya kuwa ulimwengu wa utoto ni kama pepo, pale aliposema: “Watoto ni vipepeo vya Peponi.”
Kuwatunza watoto ni jambo la lazima, na kuwapenda humleta mtu karibu na Mwenyezi Mungu. Mtume (s.a.w.) amesema: “Lau kama si watoto wanyonyeshwao, na wazee wanaorukuu (kwa kuswali) na wanyama walishwao mashambani, basi mngelipatwa na adhabu kali.”
Inaonyesha wazi kwamba huruma na uangalifu wa Mwenyezi Mungu kwa watoto ndiyo uliofanya Mwenyezi Mungu kuzuia adhabu juu ya watu wake.
  1. Mapenzi Ya Mtume Kwa Watoto
Mapenzi ya Mtume (s.a.w.) kwa watoto yalijaa ndani ya moyo wake mwema, imeelezwa katika Hadith: “Siku moja Mtume (s.a.w.) alipanda juu ya mimbari akiwahutubia watu, (mara) akawaona Hasan na Husein (a.s.) wanakimbia na huku wakijikwaa, akakatiza hotuba yake, akashuka kutoka juu ya mimbari kwenda kuwapokea watoto hao wawili. Akawabeba mikononi mwake, kisha akapanda tena juu ya mimbari akasema: “Enyi watu, hakika mali zenu na watoto wenu ni fitina, Wallahi nimewaona wajukuu wangu wawili wakikimbia na kujikwaa, basi sikuweza kujizuia mpaka nimeshuka nikawabeba.”
Siku moja Mtume (s.a.w.) alikuwa anaswali, mara Hasan na Husein (a.s.) wakaingia ndani na kumpanda mgongoni kwake wakati alipokuwa amesujudu, Mtume (s.a.w.) akaendelea kusujudu tu. Alichukia kuwaharakisha washuke, mpaka waliposhuka wao wenyewe. Kisha alipotoa salaam na kumaliza Swala, akaulizwa na maswahaba wake sababu zilizomfanya asujudu kwa kitambo kirefu hivyo; akawajibu: “Wajukuu wangu wawili walikuwa wamepanda juu ya mgongo wangu nami nilichukia kuwahimiza washuke kwa haraka.”
Mtume (s.a.w.) alizoea kuharakisha Swala yake pindi asikiapo mtoto analia, na husema: “Mimi huchukia kumchosha mama yake.”
Siku moja alikuwa anapita nyumbani kwa Fatima (a.s.) (binti yake), akamsikia mjukuu wake Husein (a.s.) akilia, aliingia ndani na baada ya kumkemea Fatima akasema: “Je hujui kwamba nimsikiapo Husein akilia huwa nakereka?”
Siku moja Mtume (s.a.w.) alitembelewa na Al-Akraa Ibn Habis, ambaye alimwona Mtume (s.a.w.) akiwabusu wajukuu zake, Al-Akraa akasema: “Unawabusu watoto wa binti yako? Naapa kwa Mungu nina watoto kumi, na sijawahi kumbusu hata mmoja.”
Mtume (s.a.w.) akamjibu: “Je ni kosa langu kama Mwenyezi Mungu ameing’oa rehma kutoka moyoni mwako.”

No comments:

Post a Comment