Friday, 14 July 2017

MGOMO WA MWALIMU

MGOMO WA MWALIMU
Sayyid Jawad Amuli, alikuwa Aalimu (Faqih) mashuhuri sana, ambaye ndiye aliandika kitabu Miftahul Karamah (Kitabu maarufu sana).
Siku moja alikuwa akishughulika na kula chakula wakati aliposikia mlango ukibishwa. Mara alipojua kuwa alikuwa mfanyakazi wa mwalimu wake - Sayyid Mahdi Bahrul Uluum - haraka alifungua mlango. Mfanyakazi alimwambia, “Bwana, Mwalimu anakuita upesi. Chakula tayari kimeandaliwa mbele yake lakini hawezi kukigusa hadi ufike huko.”
Hakukuwa na muda wa kupoteza; hata kabla ya kumaliza chakula chake, Sayyid Jawad aliharakisha kwenda nyumbani kwa Sayyid Baharul-Uluum.
Punde tu mwalimu alipomwona Sayyid Jawad kwa hasira na huzuni kubwa alimwambia: “Ewe Sayyid Jawad! Wewe humwogopi Allah? Na huoni haya mbele ya Allah?”
Sayyid Jawad alipatwa na mshangao mkubwa. Alifikiria hata hivyo, ni nini kimetokea na ni tukio gani limejitokeza? Hadi kufikia wakati huu jambo kama hilo halijawahi kutokea kwamba mwalimu wake angemkaripia kiasi hicho. Alishughulisha akili yake kuweza kugundua sababu yake. Bila msaada wowote aliuliza: “Bwana wangu, kama inawezekana tafadhali nijulishe makosa yangu.”
Alijibiwa, Jirani yako fulani hakuweza kupata mchele na ngano kwa siku saba zilizopita na katika hizi siku amekuwa akila tende za kukopa kutoka kwa muuza duka ambaye yuko mwisho wa njia. Leo alipokwenda kuchukua mkopo, kabla hajauliza chochote, muuza duka alimhuzunisha kwa kumwambia: “Sasa hivi una deni kubwa sana.”
“Kwa kusikia hayo aliona haya na bila kunyanyua kichwa aliondoka na kurudi nyumbani bila ya kitu. Leo yeye na familia yake wana njaa.”
Sayyid Jawad Amuli akasema: “Wallahi naapa kuwa sikujua kuhusu jambo hili. Kama ningejua hivyo mimi bila shaka ningewasaidia.”
Mwalimu alisema: “Huzuni na hasira yangu vyote ni kwa sababu ya kutojua kwako. Zaidi ya hayo kwa nini hujui hali ya jirani yako? Na ni kwa nini wamemaliza siku saba usiku na mchana katika hali hiyo bila ya wewe kujua jambo hilo. Na kama ulijua jambo hili na ukawa hukuchukua hatua yoyote, haungechukuliwa kama Mwislamu, bali kama Myahudi.”
Sayyid Jawad akasema, “ Nieleze nifanye nini?”
Mwalimu akamjibu: “Mfanyakazi wangu atabeba sinia iliyojaa chakula. Wewe nenda naye kwenye nyumba ya yule bwana. Mfanyakazi atarudi afikapo mlangoni. Baada ya hapo utabisha mlango na uwaombe ule pamoja nao chakula chao cha usiku. Chukua hizi pesa na uziweke chini ya zulia au mkeka. Na umuombe akusamehe kwamba kwa kuwa jirani yao, hukuweza kuwajali. Iwache hii sinia hapo hapo na urudi hapa. Naketi hapa na siwezi kula chakula hiki hadi urudi na unieleze kuhusu huyo bwana mcha Mungu. “
Mfanyakazi akachukua hiyo sinia iliyojaa chakula kizuri na kufatana na Sayyid Jawad.
Walipofika karibu na mlango, mfanyakazi alirudi.
Baada ya kubisha hodi, aliingia ndani. Mwenye nyumba akamsikiza Sayyid Jawad akiomba msamaha na kwa maombi yake alikichukua chakula kutoka mikononi mwake.
Baada ya tonge la kwanza tu, aligundua kuwa hakikuwa chakula cha nyumba ya Sayyid Jawad. Mara moja aliacha kula na kusema: “Hiki chakula hakitengenezwi na mwarabu yeyote. Hivyo basi hakijatoka kwenye nyumba yako. Hadi wakati ambapo utanieleza chakula hiki kimetoka wapi ndio tutakila.
“Makisio ya yule bwana yalikuwa sawa. Chakula hicho kilikuwa kimetengenezwa nyumbani kwa Bahrul Uluum na alikuwa Muirani kutoka Burujard.
Sayyid Jawad alisisitiza kwa kusema, “Kwanini unajisumbua kutaka kujua kilipotayarishwa chakula hiki, wewe endelea chukua kula. “Lakini Bwana huyo hakukubaliana naye na akasema: “Mimi sitagusa chakula hiki hadi uniambie ukweli.”
Sayyid Jawad aliona hakuna kitakachowezekana hadi aseme ukweli. Hivyo basi akaeleza hadithi yote kutoka mwanzo hadi mwisho. Baada ya kumsikiliza Sayyid Jawad, bwana huyo alikila hicho chakula lakini alishangaa. Akasema: “Sisi hatukumueleza mtu yeyote siri hii. Bali hata hatukukubali jirani yetu wa karibu ajue kuhusu jambo hili, sijui ni vipi Sayyid alivyokuja kulijua hili.”

No comments:

Post a Comment