Friday, 14 July 2017

UBORA WA MTU MBELE YA ALLAH (S.W) UNATEGEMEA UCHAMUNGU NA SIO UKARIBU WA MTU KWA MTUME (S.A.W.W)

UBORA WA MTU MBELE YA ALLAH (S.W) UNATEGEMEA UCHAMUNGU NA SIO UKARIBU WA MTU KWA MTUME (S.A.W.W)
Kuna watu wanasema kuwa masahaba wote wa Mtume (s.a.w.w) walikuwa ni wachamungu. Sielewi labda ni kutokujua Historia yao au kutokufahamu maana ya sahaba.
Sahaba ni Mtu yeyote aliyezaliwa au kusilimu wakati Mtume (s.a.w.w) akiwa hai awe alimuona kwa macho au hakumuona kwa sababu ya upofu au umbali wa kutoka eneo analoishi huyo na eneo alilokuwa akiishi Mtume (s.a.w.w) na hivyo kusababisha wasionane kwa macho, lakini bado ni sahaba. Hii itakuwa na maana kuwa malaki ya watu waliokuwa wakiishi Uarabuni kipindi hicho walikuwa Masahaba. Wale waliozaliwa au kusilimu baada ya Mtume kufariki wanaitwa Tabiin, na kizazi kilichopatikana baada ya tabiin huitwa tabitabiin. Sasa hakuna uwezekano wa kuwasema wote kuwa wachamungu bila kuwatofautisha kulingana na matendo yao.
Jee wake wa Mtume Muhammad (s.a.w.w); hawakuwa Waislamu? Hawakuwa ma mama wa waumini? Mbona Mwenyezi Mungu amewawekea sharti ya ucha-Mungu (Sura 33:32) ndipo wapate daraja yao, kwa kuwaambia: 'Enyi wake wa Mtume! Nyinyi si kama yeyote kati ya wanawake, kama mtamcha Mwenyezi Mungu...' Hili ni kutuonyesha kwamba kama hawatakuwa na mwendo mwema (hawatamcha Mola wao), basi ile kuwa ni wake wa Mtume tu hakutawafaa kitu. Bali ikizidi, kama watafanya machafu yoyote, inatakikana adhabu yao iwe maradafu kama inavyoelezwa kwenye Sura 33:30. Na hivyo ndivyo inavyotakikana tuwe kwa masahaba.
Ili tupate mafunzo toka kwa Masahaba tunatakiwa tuchunguze mienendo yao, tutakao ona kuwa wana mienendo mizuri tuwafuate na tutakao ona kuwa wana mienendo mibaya tuambizani kukwepa kuwafuata.
Maana kama wao-waliokaa na Bwana Mtume (s.a.w.w.) na kupokea kwake maadili yote hawatatuwekea ruwaza njema, nani mwingine atatufanyia hilo? Na jee, kama hatutawatuhumu kwa yale maovu waliyoyatenda, watu wengine si watayachukulia kuwa ni mema kwa sababu tu yamefanywa na sahaba wa Mtume (s.a.w.w.), hasa kwa hivi ambavyo, Kisunni, mwendo wa baadhi ya sahaba [1] wa Bwana Mtume (s.a.w.w.) huhesabiwa kuwa ni sunna?!
Kutokana na aya mbili tatu tulizozitaja hapo juu, nataraji nimeweza kuthibitisha kwamba ule mtazamo wa kuwa sahaba wote ni waadilifu, baada ya kuambiwa kwamba sahaba ni yule aliyemwona Mtume (s.a.w.w) japo kwa mbali-na akafa ni Mwislamu, ni mtazamo unaopingana na Qur'ani Tukufu na mafunzo ya Bwana Mtume (s.a.w.w.).
Nitaendelea kutoa mada hii kuonesha kuwa imani ya kuwa Masahaba hawakosei na kwamba wote ni wachamungu unavyopingana na ukweli wa maisha yao wenyewe Masahaba. Kwa mfano masahaba walipingana vita na kuuana, hivi ni kweli kwamba aliyeua na aliyeuawa wote walikuwa wachamungu? Haitoshi baadhi ya ndugu wa Mtume ndio waliokuwa makafiri wakubwa na wakimpiga vita Mtume (s.a.ww.).
Marejeo:
[1] - Taz. uk. 74 wa Juzuu ya Nne ya al-Muwafaqat ya Shatibi.

No comments:

Post a Comment