Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa mwongozo
wa Qur'ani na mtindo wa maisha ya Kiislamu vinapaswa kutawala katika jamii ya
Kiislamu.
Ayatullah
Khamenei aliyasema hayo jana alasiri baada ya majlisi ya qiraa ya Qur'ani
iliyoendelea kwa kipindi cha zaidi ya masaa matatu. Alisema kuwa kusoma na
kuhifadhi Qur'ani Tukufu ni utangulizi na mwanzo wa kufika kwenye jamii
inayotakikana ya Qur'ani. Amesisitiza kuwa, mwongozo wa Qur'ani na mtindo wa
maisha ya Kiislamu vinapaswa kutawala jamii ya Kiislamu.
Ayatullahil
Udhmaa Ali Khamenei amesema kuwa, kusoma na kuhifadhi Qur'ani Tukufu
hutayarisha uwanja mzuri wa kuelewa kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu na
kujipamba kwa maadili yake. Ameongeza kuwa utamaduni wa jamii ya Kiislamu
unapaswa kuoana na akhlaki na maadili ya Qur'ani pamoja na mafundisho ya
maasumu.
Ameashiria
baadhi ya njama za kutaka kuathiri utamaduni, mtindo wa maisha ya jamii na
mahusiano yake ya kijamii kwa kutumia utamaduni wa Kimagharibi na akasema:
Kufuatwa utamaduni wa Magharibi na watu wengi duniani hakuwezi kuwa kigezo na
hoja ya kufuatwa utamaduni huo katika jamii ya Kiislamu.
Amesema dini,
akili timamu na semi za maasumina ndiyo vigezo vilivyoainishwa na Qur'ani
ambavyo vinapaswa kuwa mizani na kigezo.
Ayatullahil
Udhmaa Khamenei ameelezea kufurahishwa kwake na jinsi vijana wanavyovutiwa
zaidi na Qur'ani, kusoma na kuhifadhi kitabu hicho na amesisitiza kuwa: Watu
wote wa jamii wanapaswa kujenga uhusiano na Qur'ani Tukufu kwa sababu kusoma na
kuielewa Qur'ani ni mwanzo wa kutadabari na kuzama ndani ya maana ya aya za
kitabu hicho.
No comments:
Post a Comment