Friday, 20 September 2013

Wamagharibi hawasiti kuua mamilioni ya watu kwa ajili ya kudhamini maslahi yao


Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa serikali, viongozi wa nchi, wanasiasa, wanadiplomasia na wananchi wote wanapaswa kuchambua kwa umakini harakati, mwenendo tata na madai ya kutetea haki za binadamu ya Magharibi.
Ayatullahil Udhmaa Khamenei ambaye leo alihutubia hadhara ya maimamu wa Swala za Ijumaa kote nchini waliokwenda kuonana naye ameeleza sababu za udharura wa kuwa na mtazamo mpana na wa kutilia maanani ukweli wa mambo kuhusu masuala ya Iran na dunia na akasema: Katika kipindi cha ukoloni, Magharibi ilieneza udhibiti wake wa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni katika eneo la mashariki mwa dunia ukiwemo ulimwengu wa Kiislamu, na kwa kutumia maendeleo ya sayansi na teknolojia, imewafanya watu waamini kuwa, ulimwengu wa Magharibi ndio kigezo na kituo kikuu cha mahesabu yote.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, hata mahesabu ya kijografia Wamagharibi wameyapanga kwa msingi wa kuitambua dunia ya Magharibi kuwa ndiyo bora zaidi na kuanzisha istilahi zisizo sahihi kama "Mashariki ya Karibu", Mashariki ya Kati" na "Mashariki ya Mbali".
Ameashiria udhibiti mutlaki wa nchi za Magharibi katika masuala ya dunia kwa kutumia kipindi cha ukoloni wao katika maeneo mbalimbali ya dunia na kusema: Katika hali hiyo ambapo nchi za kanda hii ikiwemo Iran, zilikuwa zimeathiriwa na udhibiri wa Magharibi na ulimwengu wa kimaada,
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yakijitegemea kikamilifu na kwa mujibu wa Uislamu na misingi ya Qur'ani, yalipata ushindi na kutoa pigo kubwa kwa misingi ya kihistoria ya Wamagharibi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia taathira za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika ulimwengu wa Kiislamu na vilevile utambulisho wa Kiislamu ulioletwa na mapinduzi hayo kwa watu wa mataifa mbalimbali na akasema: Kuenea hatua kwa hatua fikra na utambulisho wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuliwatia wasiwasi mkubwa Wamagharibi ambao walianza kupanga njama na mikakati kabambe ya kukabiliana na mapinduzi hayo.
Amesema kuwa hali ya sasa Katika Mashariki ya Kati na ulimwengu wa Kiislamu imewafanya Wamagharibi waamini kuwa, wamebaki nyuma katika mpambano wao na fikra za Mapinduzi ya Kiislamu na kwa msingi huo wanafanya kila wawezalo ili kufidia kubakia nyuma kwao.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, katika hali kama hiyo kumeanza harakati ya mwamko wa Kiislamu, na Wamagharibi ambao walikuwa wakijiona kuwa wamebakia nyuma katika mpambano wao na harakati ya fikra za Mapinduzi ya Kiislamu wameingia kwenye medani wakiwa na kiwewe kwa ajili ya kukabiliana na mwamko wa Kiislamu na Uislamu wa kisiasa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ndiye mshindi mkubwa katika mpambano wa ulimwengu wa kimaada dhidi ya Uislamu. Ameongeza kuwa, mshindi huyo mkubwa anaendelea kusimama kidete na mshikamano wa ndani na kushikamana na misingi na thamani zake kutalinda na kuimarisha zaidi ushindi huo.
Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza kuwa, Iran inapaswa kuwa imara na yenye nguvu mbele ya ulimwengu wa Magharibi kwa sababu Wamagharibi wameonesha kuwa, hawana huruma kwa mtu yeyote, na kinyume na madai yao ya kutetea haki za binadamu, hawawezi kuathiriwa na kuuliwa mamilioni ya wanadamu.
Amesema kuwa kusema uongo na kutaka kujionesha ni miongoni mwa sifa za wanasiasa za Kimagharibi. Ameongeza kuwa, ukweli wa mambo ni kuwa Wamagharibi hawaumizwi na mauaji ya watu wa Hiroshima, kuuliwa kwa mamilioni ya watu katika Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia na kuuliwa kwa watu wasio na hatia katika nchi za Pakistan, Afghanistan na Iraq na hawatasita kuua watu katika siku za usoni kwa ajili ya kutimiza maslahi yao. Amesisitiza kuwa: Kwa msingi huo Iran inapaswa kuzidisha uwezo wake wa ndani katika nyanja mbalimbali za kisaisa, kiserikali na kimaisha.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja Swala ya Ijumaa kuwa ni kanali yenye thamani kubwa ya kidini, ya wananchi na serikali na kuongeza kuwa, Sala ya Ijumaa ni mchanganyiko wa kuweka wazi hakika za kiroho na Kiislamu, mahudhurio ya wananchi katika medani na yenye mfungamano na serikali ya Kiislamu.
Kuhusu mfungamano wa Swala ya Ijumaa na serikali, Ayatullah Khamenei amesema kuwa tofauti na baadhi ya watu anavyodhania, wadhifa wa serikari hauishii katika kudhamini hali bora ya kimaisha, uhuru na kujitegemea kisiasa kwa wananchi, bali serikali inawajibika mbele ya masuala ya dini na itikadi za wananchi.
Ayatullah Khamenei pia amewausia maimamu wa Swala za Ijumaa kutoa hotuba fupi, zilizojaa maana na kuambatana na mawaidha na akasema: Hotuba za Swala ya Ijumaa zinapaswa kuzungumzia mahitaji ya watu na kujibu maswali yao hususan tabaka la vijana katika nyanja za kiitikadi, kielimu na kisaisa.   

No comments:

Post a Comment