Tuesday 16 February 2016

MWENYEZI MUNGU ALIE TAKASIKA NA KUTUKUKA AMEEPUKIKA NA SIFA ZA UPUNGUFU:

MWENYEZI MUNGU ALIE TAKASIKA NA KUTUKUKA AMEEPUKIKA NA SIFA ZA UPUNGUFU: 

Mwenyezi Mungu si mwenye kiwiliwili na wala si murakkab (yaani hakuunganika kwa sehemu tofauti) hana sehemu wala mahala maalum. 

Na haiwezekani kumuona Mwenyezi Mungu mtukufu, si katika Dunia wala Akhera, na wala hatokewi na mabadiliko, hapatwi na kiu, hashikwi na njaa, hazeeki hamaliziki, hashikwi na mghafala wala kulala. Na hana mshirika wala mwenza, bali yeye ni mmoja na wa pekee, mmoja mwenye kutegemewa, hana mke wala mtoto. Na sifa zake ndio dhati yake yenyewe, hakuna uwili kati yake na sifa zake, yeye ni muweza mjuzi hadi mwisho wa sifa zake njema kuanzia tangu na tangu, si kama sisi, kwani tulikuwa ni wajinga kisha tukajifunza na hatukuwa ni wenye uwezo kisha tukawa ni wenye uwezo. 

Na yeye ni ghanii (tajiri na mwenye kujitosheleza) na hakihitajii chochote na yeyote, hahitaji ushauri wa yeyote, au msaidizi au waziri, au askari na mfano wa hayo.

ITIKADI YA KISHIA KUHUSU MUUMBA

ITIKADI YA KISHIA KUHUSU MUUMBA

Mashia wanaamini kuwepo kwa Mungu Mmoja, Mwumba wa Ulimwengu, Mwenye Kuruzuku, Mwenye Kuhuisha, Mjuzi, Muweza, Hai, Mdiriki, Mwenye enzi, Asiye na Mwanzo wala Mwisho, Msemi, Mkweli, Asiye na mwili, Asiyeonekana, Asiyebadilika, Asiye na mshirika,

Naye ni Mwadilifu katika vitendo, maamrisho na uumbaji, kama Anavyosema Mwenyewe katika Qur’an: “Hakika Mola wako si dhalimu kwa waja wake.” (Qur’an, 3:181).

MATENDO MATUKUFU KWA MUISLAMU {2}

MATENDO MATUKUFU KWA MUISLAMU {2}

Kama kweli wewe ni mwislamu wa kweli jilazimishe kuwa na matendo yafuatayo.
{1} Unyenyekevu:-
Mtume Mtukufu {s.a.w.w.} amesema: "Kwa hakika unyenyekevu humzidishia kiumbe daraja na cheo kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo nyenyekeeni, Mwenyezi Mungu atawahurumieni.

{2}Huruma na upole:
Mtukufu Mtume {s.a.w.w.} amesema: "Mwenye Imani, imechanganyika elimu yake na upole, kwani elimu bila kuwa na upole haina faida yoyote".


{3} Kukaa vyema na watu:
Amesema Imam Jaffer As-Sadiq {a.s.}:- "Muislamu ni ndugu wa Muislamu, asimdhulumu, asimdanganye, asimtupe na kumuacha, asimsengenye, asimfanyie hiyana wala asimnyime".

UMUHIMU WA MTOTO KATIKA UISLAMU KABLA YA KUZALIWA

UMUHIMU WA MTOTO KATIKA UISLAMU KABLA YA KUZALIWA

Kutilia maanani kwa Uislamu kuhusu malezi ya mtoto hakuanzii baada ya kuzaliwa tu, bali hata kabla hajaanza kupata umbo (tumboni) kwani Uislamu unamuamuru mtu kuoa mke mcha Mungu na mtulivu. Mtume (s.a.w.w) amesema: “Jitahidi umpate mke mwenye kushikamana na dini, basi furaha zote ni zako.”
Uzuri, na utajiri si sifa pekee za kutosha kuchagua mke, sambamba na sifa hizo, pia mke ni lazima awe na sifa zingine, kwa mfano kumpata aliye na dini, na awe ametoka kwenye nyumba yenye mema.
Kwa sababu watoto wake atakaowazaa mke huyo watarithi tabia, adabu na mwenendo wake. Mwenyezi Mungu amekataza kuoa mwanamke mzuri tu asiye na tabia nzuri na nidhamu. Mtume (s.a.w.) amekataza: “Jihadharini na wanawake wazuri wenye sifa mbaya.”
Mtume (s.a.w.) pia ameweka mwongozo kwa mwanamke ambaye yu tayari kuolewa: atafute mume mcha Mungu, mwenye tabia za kidini, atakayeangalia jamii yake kwa ukamilifu, kutekeleza haki za mke, na kusimamia malezi ya watoto. Mtume (s.a.w.) amesema: “Atakapowajia mtu mtakayeridhishwa na jinsi alivyoshika dini, na tabia yake, basi muozeni, ama msipofanya hivyo, mtaleta fitina na ufisadi mkubwa duniani.”
Mtume (s.a.w.) ameonya pia kuhusu kuoana na ndugu wa karibu, ili watoto wasizaliwe wadhaifu, akasema: “Oeni walio nje ya jamii yenu, msiwadhoofishe watoto wenu.”
Qur’an imetaja ya kwamba, mwanadamu ameumbwa kutokana na tone la manii lililochanganyika: “Hakika tumemuumba mwanadamu kutokana na tone la manii lililochanganyika…” (76:2).
Hii inaonyesha kwamba, mtoto azaliwaye na wazazi ambao si ndugu wa karibu atakuwa na uwerevu, utambuzi na mwenye nguvu za kimwili kuliko mtoto aliyezaliwa na wazazi wenye uhusiano wa karibu.
Hii inaweza kuonekana kwamba Uislamu umezitangulia (kwa uvumbuzi) kanuni za kisayansi na elimu ya ‘tabia zinazorithishwa’ (Heredity) kwa kuonyesha umuhimu ulioko katika sehemu ya urithi wa tabia, na namna gani uteuzi mzuri wa watu wawili wanaooana utakavyopelekea kupata watoto ambao ni tuzo la Mwenyezi Mungu na furaha ya maisha.
Kwa kuwa mtoto atachukua mwenendo wa wajomba na shangazi zake, asili ya undani ya baba yake na mama yake, na akajifunza kupitia kwa urathi ambao umepitia kutokana kwa muungano wa baba yake na mama yake, na ndipo Uislamu ukazitengeneza asili hizi kwa njia hiyo ili kumhifadhi mtoto awe ni kiumbe mwenye heshima na nidhamu, na hivyo kuepukana na upungufu wowote.
Hivyo ninawahimiza wanadamu waingie katika Uislamu makundi kwa makundi kwa sababu ndio dini pekee duniani inayokubaliana na sayansi na teknolojia. Uvumbuzi wowote uujuao umo ndani ya Qur’an, kama hujasikia masheikh wakielezea haina maana kuwa kitu hicho hakipo bali itamaanisha kuwa masheikh hawajapata uwezo wa kulifafanua jambo hilo.
Ama mtoto ni muhimu sana katika kila jamii kwa sababu ndiye atakayeshika mikoba ya kuiongoza jamii. Endapo kama mtoto huyu asipoandaliwa vyema jamii nzima huharibika na kupoteza uelekeo.

Monday 15 February 2016

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU
Assalaam alaykum:
Nafasi ya elimu na mwenye elimu katika uislamu inaonekana katika maeneo yafuatayo:
Kwanza, Elimu ndio takrima ya kwanza aliyokirimiwa mwanaadamu na Mola wake.Tunajifunza katika Qur’an kuwa jambo la kwanza alilotunukiwa Adam (a.s) mara tu baada ya kuumbwa kwake ni kupewa elimu. "Na (Mwenyezi Mungu) akamfundisha Adam majina ya vitu vyote..." (2:31) "Majina ya vitu vyote" katika aya hii inaashiria fani zote za elimu ambazo anahitajia mwanaadamu hapa duniani ili afikie kwa ufanisi lengo la kuumbwa kwake. Pia tunajifunza katika Quran kuwa mwenye elimu na hekima amepewa kheri nyingi. (Mungu) humpa hekima amtakaye, na aliyepewa hekima bila shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili. (2.269).

Kutafuta elimu (kusoma) ni amri ya kwanza kwa mwanaadamu. Tunajifunza kutokana na historia ya kushushwa Qur’an kuwa Wahay wa kwanza kumshukia Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambao ndio ulimtawazisha rasmi kuwa mtume ni ule unaopatikana katika aya tano za mwanzo za Suratul-'Alaq:
"Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Ambaye amemuumba mwanaadamu kwa 'Alaq (kitu chenye kuning'inia). Soma na Mola wako ni mkarimu sana. Ambaye amemfundisha mwanaadamu kwa kalamu. Amemfundisha mwanaadamu (chungu ya) mambo aliyokuwa hayajui".(96:1-5)
Kutokana na aya hizi, kwa muhtasari, tunajifunza yafuatayo:
1. Kusoma kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni jambo la kwanza waliloamrishwa wanaadamu na Mola wao.
2. Kusoma kwa jina la Mola wako ni kusoma kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu au ili kuweza kumwabudu Allah(s.w) inavyostahiki na kusimamisha Uislamu katika jamii.
3. Radhi za Mwenyezi Mungu zitapatikana pale mwanaadamu atakapoweza kufikia lengo la maisha yake la kumuabudu Allah (s.w) kwa kuzingatia maamrisho na mipaka ya Mwenyezi Mungu katika kila kipengele cha maisha.
4. Amri hii ya kusoma hailengi fani maalumu tu ya elimu; bali kila fani itakayomuwezesha mwanaadamu kufikia lengo la maisha yake kwa ufanisi.
5. Chanzo au chimbuko la fani zote za elimu ni Allah (s.w). Hivyo kwa Muislamu mlango wa kwanza wa elimu ni kusoma kwa mazingatio Qur’an na hadithi sahihi za Mtume (s.a.w) na kusoma maarifa ya Uislamu kwa ujumla kutokana na vyanzo hivi viwili.

Hivyo basi ninawahimiza waislamu wasome elimu zote tena kwa pupa kwa sababu hiyo ni moja ya ibada kubwa zitakazo tupelekea kuzawadia pepo ya milele kama malipo yetu ya kutenda mema hapa duniani.


Kwa hiyo tuwapuuzie wale wote wanaodai kuwa ni masheikh halafu kazi zao ni kuwazuia waislamu kujifunza elimu kadhaa wakidai kuwa ni za kimagharibi na zisizo na faida. Watu hawa ni wapotoshaji walio na lengo la kuwafanya waislamu tubaki nyuma kimaendeleo.

MATENDO YA MASAHABA KUHUSU SUNNAH

MATENDO YA MASAHABA KUHUSU SUNNAH
Ni jambo maarufu pia kwamba mengi katika matendo ya Masahaba baada ya Mtume (s.a.w.) yalikuwa kinyume cha Sunna yake, kwa hiyo imma Masahaba hawa walikuwa wanaifahamu Sunna ya Mtume (s.a.w.) na waliikhalifu kwa makusudi kutokana na ijtihadi zao dhidi ya Nassi (matamko, matendo na iqrari) za Mtume (s.a.w.), na kwa ajili hiyo Masahaba hawa inawakumba kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu pale aliposema: "Haiwi kwa Muumini wa kiume wala Muumini wa kike Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapoamua jambo wao wawe na hiyari katika jambo lao, na yeyote mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotevu ulio wazi." (Qur'an, 33:36)

Na labda (tuseme) walikuwa hawaijui Sunna ya Mtume (s.a.w.), kwani haistahiki kabisa kwa Mtume (s.a.w.) katika hali kama hii kuwaambia Masahaba wake nimekuachieni Sunna yangu hali yakuwa yeye Mtume anajua kwamba Masahaba wake ambao ni watu wa karibu mno kwake hawaifahamu Sunna yake, basi hali itakuwaje kwa watakaokuja baada yao wakati hata Mtume hawakumfahamu na wala hawakumuona?

Inafahamika pia kwamba Sunna ya Mtume haikuandikwa isipokuwa katika zama za dola ya Bani Abbas, na kwamba kitabu cha mwanzo kilichoandikwa kuhusu hadithi ni "Muwataa" cha Imam Malik, na hiyo ni baada ya fitna kubwa (kupita) baada ya tukio la Karbala na kushambuliwa mji wa Madina, kisha kuuawa kwa Masahaba hapo mjini Madina. Basi ni vipi baada ya matukio hayo mtu atakosa kuwatilia mashaka wasimulizi wa hadithi (za Mtume) ambao walijipendekeza kwa watawala ili waipate dunia? Kwa ajili hiyo hadithi za (Mtume) zimevurugika na kupingana zenyewe kwa zenyewe, nao umma wa Kiislamu umegawanyika kwenye Madhehebu mengi (kiasi kwamba) jambo ambalo limethibiti kwenye madhehebu haya, kwenye madhehebu mengine halikuthibiti, na kitu ambacho kwa hawa wanakiona ni sahihi, wale wanakipinga.
Ni vipi tutaamini kamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema kuwa "Nimekuachieni kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu, na hali ya kuwa yeye anafahamu kwamba wanafiki na wapinzani watakuja mzulia?

Hapana shaka Mtume (s.a.w.) alipata kusema,"Wako wengi wenye kunizulia, basi yeyote mwenye kunizulia na ajiandalie makazi yake motoni".
Hivyo basi iwapo wazushi walikuwa wengi katika zama za uhai wake, ni vipi Mtume aulazimishe umma wake kufuata Sunna yake na hali hawaifahamu Sunna iliyo sahihi kutokana na ile isiyo sahihi na dhaifu kutokana na ile yenye nguvu?

Katika hali hii endapo kama Mtume angekuwa ametuachia Qur’an na Sunnah pekee ndio miongozo yetu, basi tungeangukia pua kwa sababu licha ya Qur’an kuwa haina shaka lakini mwenziwe amesheheni uongo na uzushi kiasi kwamba hatuwezi kutofautisha kati ya Sunnah na uongo.
Alhamdulillah baadhi ya waislamu tumeligundua hilo na kuchukua hatua, nayo sio nyingine bali kushikamana na Ahlulbayt wa Mtume ili watuonyeshe Sunnah sahihi kwa sababu Mtume amesema watu hawa wako pamoja na haki na haki iko pamoja nao.