Tuesday 16 February 2016

UMUHIMU WA MTOTO KATIKA UISLAMU KABLA YA KUZALIWA

UMUHIMU WA MTOTO KATIKA UISLAMU KABLA YA KUZALIWA

Kutilia maanani kwa Uislamu kuhusu malezi ya mtoto hakuanzii baada ya kuzaliwa tu, bali hata kabla hajaanza kupata umbo (tumboni) kwani Uislamu unamuamuru mtu kuoa mke mcha Mungu na mtulivu. Mtume (s.a.w.w) amesema: “Jitahidi umpate mke mwenye kushikamana na dini, basi furaha zote ni zako.”
Uzuri, na utajiri si sifa pekee za kutosha kuchagua mke, sambamba na sifa hizo, pia mke ni lazima awe na sifa zingine, kwa mfano kumpata aliye na dini, na awe ametoka kwenye nyumba yenye mema.
Kwa sababu watoto wake atakaowazaa mke huyo watarithi tabia, adabu na mwenendo wake. Mwenyezi Mungu amekataza kuoa mwanamke mzuri tu asiye na tabia nzuri na nidhamu. Mtume (s.a.w.) amekataza: “Jihadharini na wanawake wazuri wenye sifa mbaya.”
Mtume (s.a.w.) pia ameweka mwongozo kwa mwanamke ambaye yu tayari kuolewa: atafute mume mcha Mungu, mwenye tabia za kidini, atakayeangalia jamii yake kwa ukamilifu, kutekeleza haki za mke, na kusimamia malezi ya watoto. Mtume (s.a.w.) amesema: “Atakapowajia mtu mtakayeridhishwa na jinsi alivyoshika dini, na tabia yake, basi muozeni, ama msipofanya hivyo, mtaleta fitina na ufisadi mkubwa duniani.”
Mtume (s.a.w.) ameonya pia kuhusu kuoana na ndugu wa karibu, ili watoto wasizaliwe wadhaifu, akasema: “Oeni walio nje ya jamii yenu, msiwadhoofishe watoto wenu.”
Qur’an imetaja ya kwamba, mwanadamu ameumbwa kutokana na tone la manii lililochanganyika: “Hakika tumemuumba mwanadamu kutokana na tone la manii lililochanganyika…” (76:2).
Hii inaonyesha kwamba, mtoto azaliwaye na wazazi ambao si ndugu wa karibu atakuwa na uwerevu, utambuzi na mwenye nguvu za kimwili kuliko mtoto aliyezaliwa na wazazi wenye uhusiano wa karibu.
Hii inaweza kuonekana kwamba Uislamu umezitangulia (kwa uvumbuzi) kanuni za kisayansi na elimu ya ‘tabia zinazorithishwa’ (Heredity) kwa kuonyesha umuhimu ulioko katika sehemu ya urithi wa tabia, na namna gani uteuzi mzuri wa watu wawili wanaooana utakavyopelekea kupata watoto ambao ni tuzo la Mwenyezi Mungu na furaha ya maisha.
Kwa kuwa mtoto atachukua mwenendo wa wajomba na shangazi zake, asili ya undani ya baba yake na mama yake, na akajifunza kupitia kwa urathi ambao umepitia kutokana kwa muungano wa baba yake na mama yake, na ndipo Uislamu ukazitengeneza asili hizi kwa njia hiyo ili kumhifadhi mtoto awe ni kiumbe mwenye heshima na nidhamu, na hivyo kuepukana na upungufu wowote.
Hivyo ninawahimiza wanadamu waingie katika Uislamu makundi kwa makundi kwa sababu ndio dini pekee duniani inayokubaliana na sayansi na teknolojia. Uvumbuzi wowote uujuao umo ndani ya Qur’an, kama hujasikia masheikh wakielezea haina maana kuwa kitu hicho hakipo bali itamaanisha kuwa masheikh hawajapata uwezo wa kulifafanua jambo hilo.
Ama mtoto ni muhimu sana katika kila jamii kwa sababu ndiye atakayeshika mikoba ya kuiongoza jamii. Endapo kama mtoto huyu asipoandaliwa vyema jamii nzima huharibika na kupoteza uelekeo.

No comments:

Post a Comment