MATENDO YA MASAHABA
KUHUSU SUNNAH
Ni jambo maarufu pia
kwamba mengi katika matendo ya Masahaba baada ya Mtume (s.a.w.) yalikuwa
kinyume cha Sunna yake, kwa hiyo imma Masahaba hawa walikuwa wanaifahamu Sunna
ya Mtume (s.a.w.) na waliikhalifu kwa makusudi kutokana na ijtihadi zao dhidi
ya Nassi (matamko, matendo na iqrari) za Mtume (s.a.w.), na kwa ajili hiyo
Masahaba hawa inawakumba kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu pale aliposema: "Haiwi
kwa Muumini wa kiume wala Muumini wa kike Mwenyezi Mungu na Mtume wake
wanapoamua jambo wao wawe na hiyari katika jambo lao, na yeyote mwenye kumuasi
Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotevu ulio wazi."
(Qur'an, 33:36)
Na labda (tuseme)
walikuwa hawaijui Sunna ya Mtume (s.a.w.), kwani haistahiki kabisa kwa Mtume
(s.a.w.) katika hali kama hii kuwaambia Masahaba wake nimekuachieni Sunna yangu
hali yakuwa yeye Mtume anajua kwamba Masahaba wake ambao ni watu wa karibu mno
kwake hawaifahamu Sunna yake, basi hali itakuwaje kwa watakaokuja baada yao
wakati hata Mtume hawakumfahamu na wala hawakumuona?
Inafahamika pia kwamba
Sunna ya Mtume haikuandikwa isipokuwa katika zama za dola ya Bani Abbas, na
kwamba kitabu cha mwanzo kilichoandikwa kuhusu hadithi ni "Muwataa"
cha Imam Malik, na hiyo ni baada ya fitna kubwa (kupita) baada ya tukio la
Karbala na kushambuliwa mji wa Madina, kisha kuuawa kwa Masahaba hapo mjini
Madina. Basi ni vipi baada ya matukio hayo mtu atakosa kuwatilia mashaka
wasimulizi wa hadithi (za Mtume) ambao walijipendekeza kwa watawala ili waipate
dunia? Kwa ajili hiyo hadithi za (Mtume) zimevurugika na kupingana zenyewe kwa
zenyewe, nao umma wa Kiislamu umegawanyika kwenye Madhehebu mengi (kiasi
kwamba) jambo ambalo limethibiti kwenye madhehebu haya, kwenye madhehebu
mengine halikuthibiti, na kitu ambacho kwa hawa wanakiona ni sahihi, wale
wanakipinga.
Ni vipi tutaamini
kamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema kuwa "Nimekuachieni kitabu cha
Mwenyezi Mungu na Sunna yangu, na hali ya kuwa yeye anafahamu kwamba wanafiki
na wapinzani watakuja mzulia?
Hapana shaka Mtume
(s.a.w.) alipata kusema,"Wako wengi wenye kunizulia, basi yeyote mwenye
kunizulia na ajiandalie makazi yake motoni".
Hivyo basi iwapo
wazushi walikuwa wengi katika zama za uhai wake, ni vipi Mtume aulazimishe umma
wake kufuata Sunna yake na hali hawaifahamu Sunna iliyo sahihi kutokana na ile
isiyo sahihi na dhaifu kutokana na ile yenye nguvu?
Katika hali hii endapo
kama Mtume angekuwa ametuachia Qur’an na Sunnah pekee ndio miongozo yetu, basi
tungeangukia pua kwa sababu licha ya Qur’an kuwa haina shaka lakini mwenziwe
amesheheni uongo na uzushi kiasi kwamba hatuwezi kutofautisha kati ya Sunnah na
uongo.
Alhamdulillah baadhi
ya waislamu tumeligundua hilo na kuchukua hatua, nayo sio nyingine bali
kushikamana na Ahlulbayt wa Mtume ili watuonyeshe Sunnah sahihi kwa sababu
Mtume amesema watu hawa wako pamoja na haki na haki iko pamoja nao.
No comments:
Post a Comment