Monday 15 February 2016

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU
Assalaam alaykum:
Nafasi ya elimu na mwenye elimu katika uislamu inaonekana katika maeneo yafuatayo:
Kwanza, Elimu ndio takrima ya kwanza aliyokirimiwa mwanaadamu na Mola wake.Tunajifunza katika Qur’an kuwa jambo la kwanza alilotunukiwa Adam (a.s) mara tu baada ya kuumbwa kwake ni kupewa elimu. "Na (Mwenyezi Mungu) akamfundisha Adam majina ya vitu vyote..." (2:31) "Majina ya vitu vyote" katika aya hii inaashiria fani zote za elimu ambazo anahitajia mwanaadamu hapa duniani ili afikie kwa ufanisi lengo la kuumbwa kwake. Pia tunajifunza katika Quran kuwa mwenye elimu na hekima amepewa kheri nyingi. (Mungu) humpa hekima amtakaye, na aliyepewa hekima bila shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili. (2.269).

Kutafuta elimu (kusoma) ni amri ya kwanza kwa mwanaadamu. Tunajifunza kutokana na historia ya kushushwa Qur’an kuwa Wahay wa kwanza kumshukia Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambao ndio ulimtawazisha rasmi kuwa mtume ni ule unaopatikana katika aya tano za mwanzo za Suratul-'Alaq:
"Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Ambaye amemuumba mwanaadamu kwa 'Alaq (kitu chenye kuning'inia). Soma na Mola wako ni mkarimu sana. Ambaye amemfundisha mwanaadamu kwa kalamu. Amemfundisha mwanaadamu (chungu ya) mambo aliyokuwa hayajui".(96:1-5)
Kutokana na aya hizi, kwa muhtasari, tunajifunza yafuatayo:
1. Kusoma kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni jambo la kwanza waliloamrishwa wanaadamu na Mola wao.
2. Kusoma kwa jina la Mola wako ni kusoma kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu au ili kuweza kumwabudu Allah(s.w) inavyostahiki na kusimamisha Uislamu katika jamii.
3. Radhi za Mwenyezi Mungu zitapatikana pale mwanaadamu atakapoweza kufikia lengo la maisha yake la kumuabudu Allah (s.w) kwa kuzingatia maamrisho na mipaka ya Mwenyezi Mungu katika kila kipengele cha maisha.
4. Amri hii ya kusoma hailengi fani maalumu tu ya elimu; bali kila fani itakayomuwezesha mwanaadamu kufikia lengo la maisha yake kwa ufanisi.
5. Chanzo au chimbuko la fani zote za elimu ni Allah (s.w). Hivyo kwa Muislamu mlango wa kwanza wa elimu ni kusoma kwa mazingatio Qur’an na hadithi sahihi za Mtume (s.a.w) na kusoma maarifa ya Uislamu kwa ujumla kutokana na vyanzo hivi viwili.

Hivyo basi ninawahimiza waislamu wasome elimu zote tena kwa pupa kwa sababu hiyo ni moja ya ibada kubwa zitakazo tupelekea kuzawadia pepo ya milele kama malipo yetu ya kutenda mema hapa duniani.


Kwa hiyo tuwapuuzie wale wote wanaodai kuwa ni masheikh halafu kazi zao ni kuwazuia waislamu kujifunza elimu kadhaa wakidai kuwa ni za kimagharibi na zisizo na faida. Watu hawa ni wapotoshaji walio na lengo la kuwafanya waislamu tubaki nyuma kimaendeleo.

No comments:

Post a Comment