Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo amemkaribisha Waziri Mkuu wa Syria na
ujumbe anaoandamana nao ofisi kwake na kusema kuwa, sababu kuu ya matukio ya
kuumiza yanayoshuhudiwa kwa sasa nchini Syria ni Marekani na utawala ghasibu wa
Israel. Amesema Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote ina
haki ya kuingilia kisiasa masuala ya Syria na si Marekani, NATO na baadhi ya
nchi za Ulaya.
Amesema kuendelea hali ya sasa
nchini Syria na mauaji yanayofanywa dhidi ya wananchi havikubaliki. Ameongeza kuwa
wanaopaswa kulaumiwa katika masuala ya Syria ni wale wanaotayarisha uwanja wa
kutumwa silaha kwa wingi ndani ya Syria na kuyasaidia kwa fedha makundi ya
waasi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu amesema kuwa, kuyapa silaha makundi ya upinzani katika nchi yoyote na
kuyasaidia kwa fedha na kipropaganda kutasababisha hali kama ile inayoshuhudiwa
kwa sasa nchini Syria. Amesisitiza kuwa iwapo hii leo wapinzani wa siasa za serikali
za Ulaya wanaofanya maandamano watapewa silaha na fedha, hapana shaka kwamba
kutajitokeza hali kama inayoshuhudiwa nchini Syria.
Ayatullah Khamenei amesisitiza
kuwa serikali ya Syria imedhulumiwa katika kadhia ya sasa na kuongeza kuwa,
serikali ya Damascus inapaswa kuyafichulia mataifa ya Kiarabu hali ya mambo na
njama zinazofanyika nyuma ya pazia dhidi ya nchi hiyo kwa kuwanyima kisingizio
cha aina yoyote wapinzani wake na kudumisha mageuzi ya kisiasa.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa
Syria Wael Nader al-Halqi amesifu misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
kuhusu masuala mbalimbali na kutoa ripoti kuhusu hali ya nchi yake.
Al-Halqi amesisitiza juu ya kuhuishwa
nafasi ya Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM)
katika masuala ya Syria na akasema, serikali ya Damascus imeazimia kukabiliana
na makundi ya kigaidi na kusafisha kabisa maeneo mbalimbali yanakojificha
makundi hayo sambamba na kudumisha marekebisho ya kisiasa na mazungumzo ya
kitaifa.
No comments:
Post a Comment