Wednesday 19 September 2012

Kubakia nyuma kwa maadui wa Uislamu mbele ya taifa la Iran na mwamko wa Kiislamu ndiyo sababu iliyowafanya wamvunjie heshima Mtume (saw)

Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Iran Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amekagua gwaride na sherehe za kuapishwa na kupewa vyeo wanafunzi wa vyuo vikuu vya maafisa wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu. Ametoa hotuba katika hadhara ya jeshi hilo akiashiria jinai ya kumvunjia heshima Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kusema kuwa, mataifa mbalimbali yanayoelewa siasa za kuuhujumu Uislamu za ubeberu na Uzayuni yanaelekeza kidole cha tuhuma kwa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya, na viongozi wa nchi hizo wanapaswa kuzuia hatua kama hizo za kiendawazimu na kuthibitisha kwamba hawakushiriki katika jinai hiyo kubwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kwamba maadui wa Uislamu wanajihisi kubakia nyuma katika kukabiliana na taifa kubwa la Iran na harakati inayokwenda kwa kasi ya mwamko wa Kiislamu na kusema kuwa: “Suala hilo limewafanya maadui wa umma wa Kiislamu wachukue hatua ya  kiendawazimu kama tukio la hivi karibuni la kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw).
Amesema kuwa tukio hilo ni miongoni mwa ibra zinatazobakia katika historia. Ameongeza kuwa viongozi wa tawala za kibeberu ambao wamekataa kulaani jinai hiyo na hawakutekeleza wajibu wao mkabala wa uhalifu huo mkubwa wanadai kuwa hawakuhusika nayo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: “Hatun’gang’anii kuwahusisha na jinai hii lakini mbinu za wanasiasa wa Marekani na baadhi ya watu wa Ulaya zinawafanya watambuliwe na walimwengu kuwa wamehusika kwa njia moja au nyingine katika uhalifu huo na kwa msingi huo wanapaswa kujisafisha na hatia hiyo kubwa si kwa maneno bali kwa vitendo”.
Amezungumzia sababu na malengo ya hujuma za vyombo vya ubeberu dhidi ya Uislamu na kusema kuwa, ni kutokana na malengo hayo ndiyo maana mabeberu hawakuzuia na wala hawatazuia vitendo kama hivyo vya kuvunjia heshima Uislamu na matukufu yake.
Akithibitisha urongo wa viongozi wa Marekani na nchi za Magharibi kwamba “kuzuia harakati za kuvunjia heshima Uislamu kunapingana na uhuru wa kujieleza”, Ayatullah Khamenei amebainisha nikta kadhaa. Moja ya nukta hizo ni kuwepo mistari myekundu huko Magharibi kwa ajili ya kuzuia aina yoyote ya kushambuliwa misingi ya ubeberu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amehoji kwamba je, yuko mtu anayeamini kwamba katika nchi ambazo zinatumia ukatili mkubwa na nguvu zote kuzuia harakati yoyote inayopinga misingi ya ubeberu, suala la kupiga marufuku vitendo vya kuvunjiwa heshima matukufu ya Uislamu linatambuliwa katika nchi hizo kuwa linapingana na uhuru wa kujieleza?
Amesema katika nchi nyingi za Kimagharibi hakuna mtu mwenye ujasiri wa kuhoji tukio linalotiliwa shaka la holocaust au kuchapisha makala kuhusu siasa chafu za ubeberu katika masuala ya kimaadili kama vitendo viovu vya kujamiiana watu wenye jinsia moja na kuhoji, inakuwaje katika masuala hayo hakuna uhuru wa kusema na kujieleza, lakini uhuru huo unaruhusiwa na kutolewa katika kuvunjia heshima Uislamu na matukufu yake?
Ayatullah Ali Khamenei ameitaja Marekani kuwa ni mlezi wa madikteta. Ameashiria uungaji mkono na himaya kubwa ya miongo kadhaa ya Marekani kwa dikteta wa zamani wa Misri Hosni Mubarak, dikteta wa Iran Muhammad Reza Pahlavi na madikteta wa sasa wa Mashariki ya Kati  na kusema: “Kwa kuwa na historia hiyo nyeusi, Wamarekani hawawezi kutoa madai ya kutetea demokrasia na kuunga mkono uhuru.”
Ayatullah Khamenei amesema kuwa maandamano ya mataifa mbalimbali kuelekea kwenye vituo vya kisiasa na kijamii vya Marekani katika nchi mbalimbali ni ishara ya chuki kubwa ya mataifa hayo dhidi ya siasa za kibeberu na Kizayuni na kuongeza kuwa, nyoyo za mataifa mbalimbali zinaichukia mno Marekani na kwa sababu hiyo kunapojitokeza fursa kama tukio la hivi karibu (la kuvunjiwa heshima Mtume “saw”) chuki na hasira hizo hudhiriri na kujitokeza kwa kiwango kikubwa.
Mwishoni mwa sehemu hii ya hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, hapana shaka kuwa katika mpambano huu na mabeberu dhidi ya dini ya Mwenyezi Mungu, jua la Uislamu litang’aa zaidi na umma wa Kiislamu utapata ushindi.
Katika sherehe hiyo ya kuapishwa na kupewa vyeo wanafunzi wa vyuo vikuu vya maafisa wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu, Amiri Jeshi Mkuu amekutaja kuwepo katika vikosi vya jeshi kuwa ni fahari kubwa na kuongoza kuwa, vijana ambao wameingia katika medani hiyo kwa uelewa na mapenzi watapata heshima ya taifa, fahari ya hapa duniani na thawabu huko Akhera.
Ameitaja Iran ya leo kuwa ni bahari kubwa iliyojaa mawimbi ya ari ya maendeleo na hamu ya harakati na uvumbuzi. Ameongeza kuwa kadiri siku zinavyopita ndivyo umuhimu na thamani za kihistoria za juhudi zinazofanywa kwa ajili ya kuijenga Jamhuri ya Kiislamu na kuimarisha zaidi jengo hilo zinavyodhihiri zaidi, na katika upande huu vikosi vya jeshi vina wajibu mkubwa.
Kabla ya hotuba hiyo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alikagua gwaride la jeshi na kutoa shahada na vyeo kwa maafisa wa jeshi
Vilevile Meja Jenerali Ataullah Salehi kamanda wa jeshi la Iran alimkaribisha Amiri Jeshi Mkuu na kusisitiza kuwa jeshi hilo liko tayari kikamilifu kwa ajili ya kulinda mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alipewa ripoti kuhusu shughuli za Chuo Kikuu cha Masuala ya Baharini cha Imam Khomeini.

No comments:

Post a Comment