Saturday 27 October 2012

VURUGU ZA KIDINI TANZANIA

Nachukua fursa hii kulaani matukio ya vurugu yaliyotokea Jijini Dar es Salaam kwa kijana wa kikristo kukojolea Qur'an takatifu ambayo ni kitabu chetu kitukufu. Lakini ninalaani pia vurugu zilizofuatia tukio hilo ambazo ni pamoja na kuchomwa kwa makanisa.
Kwa kweli hapakuwa na ulazima wa kuendeleza vurugu kwani kipindi makanisa yanachomwa tayari mtuhumiwa alikuwa mikinoni mwa polisi. Ninawaomba waislamu wenzangu tujifunze kufuata sheria pindi tunapohisi kudhulumiwa haki zetu. Tanzania kama nchi inakatiba yake na sheria ambazo inahitajika kila mtanzania azifuate. Inaeleweka wazi mtu anapovunja sheria kitu muhimu cha kufanya kwa waliovunjiwa sheria kuripoti katika vyombo vya dola.
Na ni jukumu la vyombo vya dola kufuatilia tukio zima na kuwakamata wahalifu wote na kuwafikisha mahakamani. Hakuna njia nyingine ya mkato tofauti na kufuata na kutumia mahakama zilizopo.
Kama haturidhiki na katiba na sheria zilizopo dawa yake ni moja tu. Katika mchakato wa uandikaji wa katiba unaofanyika sasa tupeleke madai yetu yote. Kama wakigoma kuyaingiza katika katiba basi tuipigie kura ya hapana. Katiba haitopita na hivyo mchakato utaanza upya.

No comments:

Post a Comment