Kiuchumi, Wayahudi ndio waliokuwa viongozi wa Arabia. Walikuwa
ndio wenye ardhi nzuri yenye kulimika katika Hijazi, na walikuwa wakulima
wazuri zaidi nchini humo. Walikuwa pia ndio wawekezaji wa vile viwanda
vilivyokuwepo katika Arabia wakati huo, na walikamata ukiritimba wa
utengenezaji wa zana za kivita.
Utumwa ulikuwa ni asisi ya kiuchumi ya Waarabu. Watumwa wa kiume
na wa kike waliuzwa na kununuliwa kama wanyama, na waliunda tabaka la
waliokandamizwa zaidi katika jamii ya kiarabu.
Tabaka lenye nguvu zaidi, la waarabu, liliundwa na mabepari na wakopeshaji
fedha. Viwango vya riba walivyotoza kwenye mikopo vilikuwa vikubwa mno, na
viliundwa maalum kuwafanya matajiri zaidi na zaidi, na wale wakopaji kuwa
masikini zaidi.
Vituo maarufu zaidi vya mjini katika Arabia vilikuwa Makka na
Yathrib, vyote katika Hijazi. Wakazi wa Makka zaidi walikuwa ni
wafanyabiashara, wachuuzi na wakopeshaji wa fedha.
Misafara yao ilisafiri wakati wa kiangazi kwenda Syria na wakati
wa kipupwe kwenda Yemen. Walisafiri pia kwenda Bahrain upande wa Mashariki na
Iraq upande wa Kaskazini Mashariki. Misafara ya biashara ilikuwa msingi wa
uchumi wa Makka, na kuiendesha kwake kulihitaji ujuzi, uzoefu na uwezo.
R.V.C. Bodley asema:
"Kuwasili na kuondoka kwa misafara kulikuwa ni matukio muhimu
katika maisha ya watu wa Makka. Karibu kila mmoja ndani ya Makka alikuwa na
namna ya kitega uchumi katika ile mali ya maelfu ya ngamia, mamia ya watu,
farasi na punda walioondoka na ngozi za wanyama, zabibu kavu na minara ya fedha
na kurudi na mafuta, manukato na bidhaa mbalimbali kutoka Syria, Misri na Fursi
(Persia/Iran), na viungo na dhahabu kutoka upande wa Kusini."
(The Messenger, 1946, Uk. 31)
Huko Yathrib, Waarabu waliendesha maisha yao kwa kilimo na
Wayahudi waliendesha maisha yao kama wafanyabiashara na wanaviwanda. Lakini
Wayahudi hawakuwa wafanyabiashara tu na viwanda; miongoni mwao pia walikuwepo
wakulima wengi, na waliileta ardhi nyingi mbovu kwenye kulimika. Kiuchumi,
kijamii na kisiasa, Hijazi ilikuwa ndio sehemu mashuhuri zaidi katika Arabia
mwanzoni mwa karne ya saba.
Francesco Gabrielli anasema:
"Katika mkesha wa Uislamu, watu wenye kujishughulisha mno na
walioendelea wa Arabia waliishi katika mji wa Maquraish. Wakati wa himaya za
Arabu ya Kusini za Petra na Palmyra ulikuwa umepita kwa muda kiasi katika
historia ya Arabia. Sasa hali ya baadae ilikuwa inaandaliwa hapo katika
Hijazi."
(The Arabs - A Compact History-1963)
Waarabu na Wayahudi wote walikula riba. Wengi miongoni mwao
walikuwa wala riba wajuzi; waliishi kwa riba waliyotoza kwenye mikopo yao.
E.A.Belyaev anaeleza:
"Riba ilitumika sana Makka, kwani ili kushiriki katika
msafara wenye faida, watu wa Makka wengi waliokuwa na kipato cha wastani
walikimbilia kwa wala riba; mbali na riba kubwa, angeweza kutegemea kupata
faida baada ya kurudi salama kwa msafara. Wafanyabiashara matajiri zaidi
walikuwa wachuuzi na wala riba.
Wakopeshaji fedha kwa kawaida walichukua dinari kwa dinari, dirham
kwa dirham, kwa maneno mengine, asilimia mia moja ya riba. Katika Qur'an 3:125,
Allah (s.w.t.) akiwaambia waumini, alisema: 'Msile riba mara mbili maradufu.'
Hii ingeweza kumaanisha kwamba riba ya asilimia mia mbili au hata mia nne
ilidaiwa.
Nyavu za riba ya Makka hazikuwakamata wakazi wenzao tu na wa
makabila yao bali pia watu wa makabila ya KiBedui ya Hijazi walioshugulika
katika biashara ya Makka. Kama katika Athens ya zamani "njia kuu za
kukandamiza uhuru wa watu zilikuwa ni pesa."
(Arabs, Islamu and the Arab Caliphate in Early Middle Ages, 1969)
No comments:
Post a Comment