USHIA asili yake ni sawasawa na Uislamu (kwa maana Ushia ni Uislamu na Uislamu ni Ushia). Ushia ulitofautiana na Usunni tokea mwanzo wa Uislamu kuhusiana na Khalifa atakayeuongoza Uislamu baada ya Mtume kufariki dunia. Sunni huamini kwamba Abubakar ndiye aliyekuwa khalifa wa kwanza lakini Shia huamini kuwa Imam Ali ndiye khalifa wa kwanza.
Kama msomi asiyekuwa na chuki atachunguza matangazo ya Mtume kama yalivyoandikwa na wanachuoni wa kisunni katika tafsiri zao za Qur'an, hadith za Mtume, elimurijali na tarekh (Historia), atalazimika kukubali kwamba alikuwa ni Mtume mwenyewe ndiye muanzilishi wa Ushia. Tangazo la kwanza la kubaathiwa liliambatana kwa wakati mmoja na tangazo la ukhalifa wa Imam Ali. Tukio hilo linajulikana kama, “Karamu wa ndugu wa karibu”. Vifungu vinavyohusu karamu hiyo vimenukuliwa hapa kutoka kitabu cha tarekh cha Tabari.
Ali (a.s) alisema, “wakati aya Na uwaonye jamaa zako wa karibu, iliposhukwa kwa Mtume wa Allah, Mtume aliniita mimi na kuniamrisha kuandaa karamu na kuwakaribisha ukoo wa Abdul-Mutalib ili apate kuzungumza nao. Walifika watu takribani 40, miongoni mwao walikuwepo ami zake Mtume yaani Abutalib, Hamza, Abasi na Abu Lahab. Kisha Mtume alitoa hotuba ifuatayo:
Enyi watoto wa Abdul-Mutalib, simjui mtu yeyote katika Bara Arabu yote ambaye amewaletea watu wake kitu kilicho bora zaidi yangu. Nimekuleteeni mema ya hii dunia na akhera. Na Allah (S.W.T) ameniamrisha nikuiteni ninyi kwayo. Ni nani basi miongoni mwenu atakaye nisaidia katika jambo hili, ili awe ndugu yangu, wasii wangu na khalifa wangu kwenu?
Ali aliendelea kusema kuwa hakuna hata mtu mmoja aliyejibu, hivyo mimi nilisema, “mimi, ewe Mtume wa Allah, nitakuwa msaidizi wako katika kazi hii. Basi Mtume akaweka mkono wake kwenye shingo yangu na kusema, “Hakika huyu ni ndugu yangu, wasii wangu na khalifa wangu miongoni mwenu, msikilizeni na mumtii. Mkutano wote ukaamka huku wakicheka na kumuambia Abu Talib kwamba Muhammad amemuamrisha yeye kumsikiliza mtoto wake na kumtii.
Soma, Tafsiri Tabari, ya Mohammad bin Jariri, Tarekh, Juzuu ya 3 uk. 1882 - 1885
No comments:
Post a Comment