Sunday, 20 April 2014

MAULID (MAJLIS) YA KUZALIWA KWA BI FATUMA ZAHRAH

Assalaam alaykum warahmatullah wabarakatuh:
Jumuiya wa waislamu wa madhehebu ya Shia Kigoma inawakaribisha watu wote kuhudhuria sherehe za kukumbuka kuzaliwa kwa bint pekee wa Mtume Mohammad (S.A.W.W) aitwaye Fatuma bint Rasulillah. Hapa chini kuna maelezo kamili ya Historia ya bint huyu mtukufu:

Kimeandikwa na Mwalimu Kabavako, Rajabu Shaban
BSc. Applied Agriculrural Extension (SUA)
© 2014
  
Wasifu wa Bi Fatima Zahra (a.s.)

 this topic
Jina lake: Fatima bint Rasulillah (a.s)

Cheo chake: Kiongozi wa wanawake wa peponi

Majina (sifa) yake mengine:
az- Zahra (Mzuri)
Al- Mardhiah (Aliyeridhiwa na Allah (S.W))
Al- Mubarakah (Aliyebarikiwa)
At- Taherah (Aliyetakaswa na Allah yaani asiye na dhambi)
Az- Zakiyah (Muadilifu)
Ar- Radhiah (aliyeridhika)
Al- Batoul (Msafi)
Ummu 'l-A'immah (Mama wa Maimamu)

Jina la baba yake: Muhammad ibn 'Abdillah (S.A.W.W.)

Jina la mama yake: Khadijah bint Khuwaylid

Mahali na tarehe ya kuzaliwa: Makkah, 20 Jumada ' th-Thaniyah mwaka wa 5 baada ya kutangazwa Utume (615 AD).

Kufa: 14th Jumada ' l-ula 11 hijiria (632 AD);
Kuzikwa: Jannatu 'l-Baqi' huko Madina

Umri wakati anafariki dunia: miaka 18
Kuolewa: mwaka 2 hijiria

Watoto wa Fatima Zahra (A.S.) ni kama ifuatavyo:
(a) Imam Hassan (A.S.)
(b) Imam Hussain (A.S.)
(c) Bi Zainab (A.S.)
(d) Bi Um Kulthum (A.S)
(e) Mohsin (A.S) 

Bi Khadija mama wa Fatuma alifariki dunia wakati bint huyu mtukufu akiwa na umri wa miaka 5. Hivyo akabaki analelewa na baba peke yake.

Moja ya sifa nyingine ya Bibi Fatma ni kuishi maisha ya kawaida na yasiyo na fakhari hasa za kidunia. Siku moja Salman Farsi alifuatana na Bibi Fatimah hadi nyumbani kwa Bwana Mtume. Walipokuwa njiani kuelekea nyumbani kwa Bwana Mtume, Salman alisema: Samahani! Mabinti wa Kaisari na Qasir wanavaa nguo za Hariri lakini binti wa Muhammad (S.A.W.W), mwanaadamu bora kabisa amevaa abaa lililochakaa. Wakati walipofika nyumbani kwa Bwana Mtume SAW, Bibi Faatimah alimwambia baba yake kwamba: Baba yangu mpenzi! Salman amestaajabishwa na mavazi yangu. Bwana Mtume (SAW) akamwelekea Salman na kumwambia: Salman! Binti yangu (si binti wa Kaisari na wafalme wanaopenda fakhari za kidunia, bali binti yangu ni miongoni mwa walio mstari wa mbele katika mbio za kwenda kwa Mwenyezi Mungu.

Bwana Mtume Muhammad (SAW) alinukuliwa akisema: "Faatimah ni kipande cha mwili wangu, ni nuru ya jicho langu, ni tunda la moyo wangu, ni moyo na ni roho yangu. Yeye ni hurulaini katika sura ya mwanadamu... kila anaposimama kufanya ibada, Mwenyezi Mungu anawaambia malaika Wake: Mwangalieni mja wangu aliye bora - Faatimah - amesimama mbele Yangu na dhati yake yote inatetemeka kutokana na unyenyekevu wake mkubwa Kwangu na amesimama kuniabudu kwa moyo wake wote."

Bibi Fatimatuz Zahra SA ni bibi mtukufu ambaye sira na mienendo yake itabakia hai milele na itaendelea kuwa ruwaza njema kwa kila mpigania haki. Bibi Fatima SA hakuishi kwa zaidi ya miaka 18, lakini alikusanya fadhail na matukufu yote ya kibinadamu. Mtukufu huyo alifikia daraja kubwa ya kumtambua Muumba wake kiasi kwamba hadi leo hii amekuwa ni kigezo bora cha maisha yaliyojaa ufanisi. Dhati yake yote ilijaa welewa na utambuzi wa Muumba wake kadiri kwamba, hakuwa akifikiria kitu chochote katika maisha yake yote isipokuwa kumridhisha Muumba wake. Bwana Mtume Muhammad SAW anatoa ushahidi wa mapenzi hayo ya kweli aliyokuwa nayo Fatima (a.s) kwa Muumba wake kwa kumwambia mmoja wa masahaba wake wakubwa Salman kwamba: Ewe Salman! Mwenyezi Mungu amemimina na kutia imani thabiti katika moyo na roho na dhati yote ya Fatima ya kumuabudu Muumba wake kiasi kwamba hakujabakia sehemu hata ndogo tupu ya kuingia kitu kingine chochote katika moyo wake ghairi ya kumuabudu Mola wake.
Roho tukufu ya Fatima haikupenda kabisa mapambo na urembo wa dunia. Nyumba ya Ali na Fatima SA haikuwa kabisa na vifaa vya nyongeza na vya thamani kubwa. Lakini badala yake ilikuwa ni nyumba iliyojaa imani, mapenzi na unyofu wa moyo hali ambayo iliongeza moyo wa kutekeleza vizuri majukumu, kupigania uadilifu na kusimamisha haki. Fatima alikuwa mbora wa wanawake wacha Mungu, lakini si kwa maana ya kuachana kikamilifu na dunia bali kwa maana ya kwamba dunia haikuiteka roho yake na wala kuifanya mtumwa wake. Kwa kweli hakuna mwanamke aliyemfikia Fatima kwa ubora.

Chochote alichokipata alikitumia katika njia ya Mwenyezi Mungu na alikuwa mstari wa mbele wakati wote kujitolea kwa ajili ya kutafuta radhi za Muumba wake.
Maneno na matendo ya Fatima yalipambika kwa adabu na heshimu kiasi kwamba mmoja wa watu waliokuwa wakimhudumia mtukufu huyo anayejulikana kwa jina la Asmaa anasema: Mimi sijawahi kumuona mwanamke mwenye adabu na heshima kama Fatima. Yeye amejifunza adabu na heshima kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wakati Mwenyezi Mungu aliposhusha aya na kuwataka Waislamu na waumini wasimwite Bwana Mtume kwa jina lake, Bibi Fatima (a.s) naye aliacha kutumia neno "baba" kumwita baba yake, bali alianza kumwita Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hadi Bwana Mtume akalazimika kusema, aya hiyo haimuhusu mwanangu Fatima.

Katika maisha yake ya kifamilia pia, heshima na adabu pamoja na mapenzi ya Fatima yalijenga mfungamano mkubwa na mtukufu sana kati yake na mumewe Ali (a.s).
Katika muda wote wa uhai wa baba yake Bwana Mtume Muhammad (S.A.W.W) na baada ya kutangulia mbele ya haki baba yake mtukufu, akawa pamoja na mumewe Ali AS, Fatima wakati wote alikuwa bega kwa bega na watukufu hao katika kupigania haki, kueneza uadilifu na kuhakikisha kuwa nuru ya Uislamu haizimi. Mtukufu huyo alikuwa na moyo wa hali ya juu wa kutekeleza vilivyo majukumu yake.
Mtukufu huyo alikuwa akihimiza kwamba mtu mwenye ufanisi ni yule ambaye anatekeleza vizuri majukumu yake mema. Muhimu ni kwamba mtu huyo ajue wajibu wake na autekeleze inavyopasa. Kutekeleza vizuri jukumu lake mtu kunahitajia welewa na maarifa pamoja na muono wa mbali. Na ndio maana wakati wote mtukufu huyo alikuwa akifanya juhudi kutumia nguvu zake zote katika kutekeleza mambo yanayomridhisha Mola wake. Pamoja na kwamba alijua kuwa angeliweza kukaa pembeni na kutumia muda wake wote kufanya ibada na kunong'ona na Mola wake, lakini alitambua vyema pia kuwa, jukumu la mtu ni zaidi ya kufanya ibada, kwani siku ya Kiyama watu wote wataulizwa walitekeleza vipi majukumu yao yote.
Mtukufu huyo, kutokana na muono wake wa mbali na mtazamo wake wa kina wa mambo aliona hatari kubwa ya kurejea watu kwenye zama za ujahilia hasa baada ya kufariki dunia Bwana Mtume Muhammad (SAW). Alitumia hekima ya hali ya juu kuwalingania watu haki na hakumuogopa mtu yeyote katika kubainisha mafundisho ya Bwana Mtume (SAW) na kuulinda Uislamu.
Miongoni mwa urithi wenye thamani kubwa uliobakishwa na Bibi Fatimatuz Zahra (a.s) ni hotuba yake yenye umuhimu mkubwa aliyoitoa baada ya kufariki dunia baba yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW). Aliitoa hotuba hiyo baada ya kuhisi kuzuka mipasuko na kupotoshwa mambo katika jamii ya Waislamu mara baada ya kufariki dunia Mtume. Ndani ya hotuba hiyo, Bibi Fatima ametaja sifa za Waislamu wa kweli. Hotuba hiyo ilikuwa mithili ya nuru inayowaangazia njia wapenda haki na wanaotafuta njia sahihi. Bibi Fatimatuz Zahra (a.) anataja njia ya kuweza kumwokoa mwanadamu kuwa ni kushikamana na haki na kuwa mtiifu mbele ya amri za Mwenyezi Mungu.
Katika sehemu moja ya hotuba hiyo yenye thamani kubwa Bibi Fatimatuz Zahra (a.s) anasema: Enyi watu! Kumbukeni mlipokuwa ukingoni mwa shimo la moto! Kumbukeni mlivyokuwa duni na mkidharauliwa, na wakati wote mlikuwa mnaogopa wasije maadui kukushambulieni na kukutekeni! Hadi Mwenyezi Mungu alipomtuma Mtume Wake Muhammad (SAW) kwenu. Mtume wa Mwenyezi Mungu ameingiza nuru katika kiza cha kufru na shirki, akaondoa ugomvi na mizozo kati yanu na kufuta kwa nuru, vumbi lililokuwa limeyafunika macho yenu.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe taufiki ya kufuata njia ya haki, njia iliyooneshwa na waja wema wa Mwenyezi Mungu, njia ya watu Wake wateule na watoharifu.
Assalaamu Alayki Yaa Fatimatuz Zahra, Sayyidatu Nisail L'aalamin.
Amani iwe juu yako Ewe Fatima, Mbora wa wanawake wote duniani.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

No comments:

Post a Comment