BARUA YA WAZI
KWA MWANACHUONI WA INDIA, SAYYID ABUL-HASAN AN-NADAWI
Amani ya Mwenyezi Mungu ikushukieni na Rehema na Baraka zake
zikushukieni.
Amma Ba'ad:
Mimi Muhammad At-Tijani As-Samawi, Mtunisia, ambaye Mwenyezi Mungu
amenineemesha kwa uongofu na mafanikio, nayakubali Madh-hebu ya watu wa nyumba
ya Mtume baada ya uchunguzi (uliochukua muda) mrefu na kabla ya hapo nilikuwa
(mfuasi wa Madh-hebu ya) Malik. Si hivyo tu, bali nilikuwa miongoni mwa wafuasi
wa Tariqa mashuhuri ya Kisufi huko Afrika ya Kaskazini iitwayo "AT-TIJANIYYAH".
Hatimaye nikaufahamu ukweli wakati wa safari yangu iliyofana kwenda kwa
Wanachuoni wa Kishia, na niliandika kuhusiana na safari hiyo kitabu
nilichokiita, "THUMMAH-TADAITU", kilikamilika kuchapishwa huko kwenu
India kwa lugha nyingi kutokana na ukarimu wa Majimau Al-ilmiyyi Al islamiyyi,
na kwa ajili ya munasaba (huu) niliitwa kuitembelea India.
Ewe Bwana wangu mpendwa, nilifika India kwa matembezi mafupi, na matarajio
yangu yalikuwa ni kukutana nanyi kutokana na sifa zenu ninazozisikia na
kutokana na kufahamu kwangu kwamba ninyi ndio mategemeo kwa AH-LISSUNNAT
WAL-JAMA'A. Lakini nilishindwa kufanya hivyo kutokana na umbali na kukosa muda,
na nikatosheka kwa kuzuru Bombay,
Puna, Jabal Pur na miji mingine iliyoko Gujarat.
Nilihuzunika sana kutokana na mambo niliyoyaona huko India (hasa) kutokana na uadui na bughudha
iliyoko baina ya Ahli-Sunnah Wal-Jama'a, na ndugu zao Waislamu wa Kishia. Kwa
hakika nilikuwa nikisikia kwamba wao hupigana na hupata wakati mwingine
wakauana na kumwaga damu za watu wasio na kosa lolote kutoka pande mbili hizi
eti kwa niaba ya (kutetea) Uislamu.
Mimi nilikuwa siamini (haya) huku nikiitakidi kuwa habari hizo
zimepewa mno sura isiyo yake, lakini niliyoyaona na kuyasikia wakati wa ziyara
yangu kwa kweli yanashangaza na nimeyakinisha kwamba huko kuna makusudio mabaya
na ushauri wa hatari unaoundwa dhidi ya Uislamu na Waislamu ili kuwamaliza wote
Masunni na Mashia. Miongoni mwa mambo yaliyozidisha uwazi wa yakini yangu na
kuimarisha ufahamu wangu (juu ya hayo) ni ule mkabala uliopita baina yangu na
kundi la wanachuoni wa Kisunni wakiongozwa na Sheikh Azizur -Rahman Mufti wa
Al-Jamaatul-Islamiyyah, na mkutano wetu ulikuwa ndani ya Msikiti wao huko Bombay
na wao ndiyo walioniita.
Baada tu ya kufika, dharau, tuhuma na matusi na kuwalaani Mashia
(Wafuasi) wa kizazi cha nyumba ya Mtume vilianza, na walikuwa wamekusudia
kunitisha na kuniudhi kwa kuwa walikuwa wanajua kwamba mimi nimeandika kitabu
kinachotoa wito wa kushikamana na Madh-hebu ya Ahlul-Bait (a.s.). Lakini mimi
nilifahamu makusudio yao na nikaimiliki nafsi yangu na
nilitabasamu hali ya kuwa nikisema: "Mimi ni mgeni kwenu ninyi, nanyi
ndiyo mlioniita na nimekuja kwa haraka kuitika wito, basi je mumeniita ili
mnitukane na kunishutumu, na Je, hii ndiyo tabia ambayo Uislamu
umekufundisheni.
Basi walinijibu kwa kujiamini
kabisa kwamba, mimi hata siku moja sijapata kuwa Muislamu kwa sababu mimi ni
Shia na Mashia hawana Uislamu wowote, na waliapa kuthibitisha jambo hilo.
Mimi nilisema, "Mcheni Mwenyezi Mungu enyi ndugu zangu, Mola
wetu ni mmoja na Mtume wetu ni mmoja na Kitabu chetu ni kimoja na Qibla chetu
ni kimoja, na Mashia wanampwekesha Mwenyezi Mungu na wanautumikia Uislamu kwa
kumfuata Mtume na Watu wa nyumba yake, wanasali Sala (Tano) wanatoa zaka na
wanahiji kwenye nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu, basi vipi inajuzu kwenu ninyi
kuwakufurisha wao?
Walinijibu, "Ninyi Hamuamini Qur'ani, ninyi ni WANAFIKI
mnatumia TAQIYYAH, na Imam wenu amesema: "Taqiyyah ni Dini yangu na ni
Dini ya wazazi wangu" Nanyi ni kikundi cha Kiyahudi alichokianzisha
Abdallah ibn Saba'a Myahudi."
Niliwaambia hali ya kuwa nikitabasamu, "Hebu tuwaache Mashia
na zungumzeni nami binafsi, kwani mimi nilikuwa (wa Madhehebu ya) Malik kama
ninyi, na baada ya uchunguzi wa muda mrefu niliyakinisha kwamba Watu wa nyumba
ya Mtume ndiyo wenye haki na ndiyo bora kuwafuata. Basi Je, mnayo hoja ya
kunijadili au kuniuliza ni ipi dalili yangu na hoja yangu ili pengine tuweze
kuelewana miongoni mwetu?"
Walisema: "Ahlul-Bait (Watu wa Nyumba ya Mtume) ni wakeze
Mtume na wewe huna ukijuacho ndani ya Qur'ani." Nikasema: "Bila shaka
Sahih Bukhar na Sahih Muslim zinafundisha kinyume cha mlivyotaja!
Wakasema: "Yote yaliyomo ndani ya Bukhari na Muslim na vitabu
vingine vya Kisunni miongoni mwa hoja mnazozitoa ni katika uzushi wa Mashia
waliouweka vitabuni kwetu."
Niliwajibu hali ya kuwa nacheka; "Ikiwa Mashia wamefikia
kiasi cha kuingiza uzushi ndani ya vitabu vyenu, basi vitabu hivyo havina maana
tena na pia Madhehebu yenu ambayo yamesimama juu ya vitabu hivyo!!"
Walinyamaza wakakosa hoja, lakini mmoja wao alikusudia kuleta fujo
na chuki kwa mara nyingine akasema: "Ye yote asiyeamini Ukhalifa wa
Makhalifa waongofu (ambao ni) Sayyidina Abu Bakri, Sayyidna Umar na Sayyidna
Uthman, Sayyidna Ali, Sayyidina Muawiyyah na Sayyidna Yazid (r.a.) basi huyo
siyo Muislamu.
Nilishangaa kwa maneno haya ambayo sijasikia mfano wake maishani
mwangu nayo ni kumkufurisha asiyeamini Ukhalifa wa Muawiyyah na Yazid, na nilisema
kimoyo moyo: "Ni jambo linaloingia akilini Waislamu kumuombea radhi
Abubakar, Omar na Uthman jambo hili limezoeleka, ama kumuombea radhi Yazid
kabisa sijasikia (popote) isipokuwa India na niliwageukia nikawauliza: "Je
mnakubaliana na huyu juu ya maoni yake?
Wote kwa pamoja wakajibu "Ndiyo".
Hapo ndipo nilipofahamu ya kuwa hakuna faida ya kuendeleza
mazungumzo, na nikafahamu pia kwamba hakuna kingine isipokuwa wanataka kuniudhi
(nikasirike) ili wapate kunishambulia na pengine waniuwe kwa madai ya kuwatukana
Masahaba, nani ajuaye (nia zao)?
Niliona machoni mwao (ishara ya) shari, nikamuomba rafiki yangu
aliyenileta kwao anitoe haraka, akanitoa huku akisikitika na kunitaka radhi kwa
yaliyotokea. Mtu huyu hakuwa na kosa alikuwa akifuatilia mkutano huo kwa kutaka
kufahamu ukweli, ni kijana
mwenye heshima (akiitwa) Sharafud-Din ambaye anamiliki
Maktaba na Kiwanda cha uchapishaji cha Kiislamu mjini Bombay. Basi yeye ni shahidi wa yote
yaliyopita baina yetu katika majadiliano yaliyotajwa, na hakuficha kutoridhika
kwake na watu hawa ambao yeye alikuwa akiamini kwamba wao ni miongoni mwa
Wanachuoni wakubwa.
Niliwaacha hali ya kuwa nimechukia na kusikitika juu ya hali
ambayo imewafikia Waislamu na hasa wale wanaosimamia vituo vya uongozi na
kujiita kuwa ni Wanachuoni, na nilisema moyoni kuwa, ikiwa hali ya Wanachuoni
iko kwenye kiwango hiki cha ung'ang'anizi wa upofu, basi hali itakuwaje kwa
watu wa kawaida na wale wasiojua kitu?
Hapo ndipo nilipofahamu ni vipi yamekuwa yakizuka mapambano na
vita ambavyo ndani yake damu iliyoharamishwa humwagwa na kuvunja heshima na
utukufu (wa watu) kwa jina la kuutetea Uislamu, na nililia juu ya hatima ya
umma huu uliogawanyika na kuangamia, umma ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu
ameubebesha jukumu la uongofu na Mtume wa Mwenyezi Mungu vile vile ameubebesha
jukumu la kuifikisha nuru kwenye nyoyo zenye kiza zinazohitaji kupata nuru
inayong'ara na kwa wakati huo huo katika India peke yake kuna watu wapatao
milioni mia saba wanaabudia asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na wanamtukuza
Ng'ombe na Masanamu. Badala ya juhudi za Waislamu kuunganika ili wawaongowe na
kuwaongoza na kuwatoa kwenye kiza watu hao na kuwapeleka kwenye nuru ili
wasilimu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mola wa Walimwengu, tunawaona Waislamu leo
hii hasa India wao ndiyo wenye haja ya uongofu na kujisahihisha.
Kwa sababu hii wewe Bwana wangu (Sayyid Abul-Hasan An-Nadawi)
ninaleta kwenu barua yangu nikikulinganieni kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi
wa Rehma Mwenye kurehemu na kwa jina la Mtume wake Mtukufu na kwa jina la Uislamu Mtukufu na kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu (Aliposema)
"Shikamaneni katika Dini ya Mwenyezi Mungu na wala msifarakane."
(Qur'an 3:103)
Nakulinganieni msimame
msimamo wa Muislamu shujaa ambaye haogopi kutekeleza la Mwenyezi Mungu na (haogopi)
lawama ya mwenye kulaumu na wala ubinafsi haumchukui wala vikundi (havimchukui)
kumpeleka namna apendavyo shetani na wafuasi wake.
Nakulinganieni msimame msimamo safi ulio wazi, kwani ninyi ni miongoni mwa
wale ambao Mwenyezi Mungu amewabebesha jukumu (la uongozi) muda wote mtakaokuwa
mkizungumza kwa niyaba ya Uislamu katika nchi hiyo. Mwenyezi Mungu
hatakuridhieni iwapo mtasimama msimamo wa mtazamaji mwenye kuridhika na yale
yanayotokea huku na huko miongoni mwa misiba inayosababisha kupoteza (maisha ya
watu) wasio na makosa miongoni mwa Waislamu wa Kisunni na Kishia. Mwenyezi
Mungu atakuulizeni siku ya Qiyama kwa kila dogo na kubwa, na atakuhesabuni
kutokana na kila linalopita na linalokuja kwa kuwa Hawawi sawa wale wanaojua na
wale wasiojua, kwani kwa kiwango cha bidii mtu afanyacho ndivyo yatavyokuwa
mafanikio, na kwa kadiri ya kiwango cha utukufu ndivyo yajavyo mambo matukufu.
Na maadam ninyi ndiyo mnaowaongoza wanachuoni wa India, basi jukumu lenu ni
kubwa na bila shaka neno litokalo kwenu huenda ndani yake kukawa na mafanikio
kwa umma (wa Kiislamu) nchini India kama ambavyo huenda kukawa na maangamivu ya
mali na watu (likitumika vibaya), basi mcheni Mwenyezi Mungu enyi watu wenye
akili! Na kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewapa Wanachuoni daraja ya kwanza baada ya
Malaika akasema: "Mwenyezi Mungu ameshuhudia ya kwamba, hapana aabudiwaye
kwa haki ila yeye tu na Malaika na wenye elimu (wameshuhudia hivyo), (Yeye) ni
Mwenye kusimamia uadilifu." (Qur'an, 3:18).
Na ikiwa Mwenyezi Mungu anatuamuru sote kwa kusema: "Na
pimeni kipimo kwa haki na wala msipunguze kipimo". (Qur'an, 55:9).
Iwapo wafasiri wanaona umuhimu wa kufanya uadilifu katika vipimo
vya kimaadda ambavyo vina viwango maalum, basi mwaonaje hali ya kufanya
uadilifu katika mambo ya kiitikadi, ambayo yanamvutano baina ya haki na batili
na kwa mambo hayo ya kiitikadi ndipo mahala unapotegemea uongofu wa watu na
uokovu wa watu wote?
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema; "Na mtakapohukumu basi
hukumuni kwa uadilifu". Na amesema tena; "Ewe Daud bila shaka sisi tumekufanya
uwe Khalifa (msimamizi) katika nchi, basi hukumu baina ya watu kwa haki na wala
usifuate matamanio yatakupotosha kutoka njia ya Mwenyezi Mungu."
Hapana shaka Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Sema kweli
japokuwa ni dhidi ya nafsi yako, sema kweli japokuwa ni chungu."
Ewe Bwana wangu Mtukufu, nakuiteni kwenye Kitabu cha Mwenyezi
Mungu, na sunna ya Mtume wake, semeni kweli wazi wazi kwa sauti kubwa japokuwa
ni chungu itakushuhudieni mbele ya Mwenyezi Mungu.
Naapa kwa Mola wako hivi kwenu ninyi Mashia siyo Waislamu? Hivi
kweli mnaitakidi kwamba wao ni makafiri? Je wafuasi wa Watu wa nyumba ya Mtume
ambao wanampwekesha Mwenyezi Mungu na kumtukuza zaidi kuliko vikundi vyote kwa
usemi wao wa kuwa hafanani na chochote kwa kumtakasa kutokana na kufanana, na
kutokana na kuwa hana umbo na mwili. Si hivyo tu bali wanamuamini Mtume wake
Muhammad (s.a.w.w.) na wanamuheshimu mno kuliko vikundi vyote wasemapo kuwa,
"Yeye Mtume ni Maasum moja kwa moja hata kabla ya kupewa utume". Je,
hawa ndiyo munaowahukumu kuwa ni makafiri?
Je, wale wanaomtawalisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale
walioamini na wanawapenda kizazi cha Mtume na kuwatawalisha kama alivyowatambulisha
Ibn Mandhur ndani ya "Lisanul-A'rab" katika mada ya Shia, basi je
ninyi mwasema kwamba wao siyo Waislamu?
Je, Mashia hawa ambao wanatekeleza wajibu wa Sala kwa namna iliyo
bora, na wanatoa Zaka na kuzidisha juu yake Khumsi ya mali zao kwa ajili ya
kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wanafunga (saumu ya) mwezi wa Ramadhani
na nyingine na wanahiji nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu na kuyatukuza mambo
matukufu ya Mwenyezi Mungu, kadhalika wanawaheshimu Mawalii wa Mwenyezi Mungu
na kujiepusha na maadui wa Uislamu, hivyo kwenu ninyi watu hawa ni washirikina?
Je, hivi watu wasemao kuwa Uimamu hasa ni (haki) wa Maimamu kumi
na wawili kutoka katika watu wa nyumba ya Mtume ambao Mwenyezi Mungu
amewaondolea uchafu na amewatakasa sana sana, na Mtume wa Mwenyezi Mungu
aliwataja kama alivyotoa Bukhari na Muslim na wengineo katika Sahihi za
Ahlu-Sunnah, hivi watu hawa kwenu ninyi ni watu waliotoka nje ya Uislamu?
Je hivi kuna siku ambayo Waislamu wamekuwa hawautambui Uimamu na
wala hawakubali sawa sawa liwe hilo katika uhai wa Mtume au baada ya kufa
kwake mpaka kufikie kuihusisha nadharia ya Uimamu kwa Waajemi na Majusi?
Na je hivi mnasema kwa kujiamini kuwa, "Ni Kafiri asiyekubali
Uimamu wa Yazidi ibn Muawiyyah ambaye uovu wake unaeleweka kwa Waislamu wote?
Na itoshe uovu na udhalimu wa Yazidi kwa maelezo walioafikiana Waislamu wote
kutokana na yeye kuruhusu kufanyika maasi kwenye mji Mtakatifu wa Madina kwa
kutumia jeshi lake na askari wake kufanya wayatakayo mjini humo ili wachukuwe
viapo vya utii (kutoka kwa watu) kwa nguvu kama kwamba (watu hao) ni watumwa
wake. Si hivyo tu, bali wa Yazid waliwaua maelfu ya Masahaba watukufu na
Tabiina, wakavunja heshima za wanawake na wasichana wa Kiislamu waliojihifadhi
kiasi walizaliwa kutokana na uchafu huo idadi ya watoto ambao hakuna awezaye
kuidhibiti isipokuwa Mwenyezi Mungu.
Na yamtosha Yazidi aibu mbaya mno
na udhalim wa kudumu kule kumuuwa Bwana wa vijana wa peponi na kuwateka Mabinti
wa Mtume na kuyachokora meno ya Husein (a.s.) kwa kijiti kisha kuimba kwake
beti za ushauri ambazo ni maarufu akasema, "Laiti wazee wangu (waliouawa)
katika Badri wangeshuhudia..." Mpaka akafikia kusema: "Banu Hashim
walichezea Ufalme, hakuna habari yeyote iliyokuja wala Ufunuo ulioshuka."
Ni wazi kabisa kwamba hakuamini utume wa Muhammad (s.a.w.w.) wala
Qur'an Tukufu, basi je, ni kweli mnaafiki kumkufurisha anayejitenga na Yazid?
Na baba yake Muawiyyah ambaye alikuwa akimlaani Ali (a.s) na huamuru alaaniwe,
bali na (alikuwa) akimuuwa kila anayekataa kufanya hivyo miongoni mwa Masahaba
wema kama alivyomfanyia Hujr ibn Adiyy Al-Kindi na jamaa zake, na (tendo la
kumlaani Ali a.s.) aliliusia likawa ni sunna iliyofuatwa kwa miaka sabini hali
ya kuwa (Muawiyyah) anaijua kauli ya Mtume (s.a.w.w.) aliposema "Yeyote
atakayemtukana Ali, basi kanitukana mimi, na atakayenitukana mimi amemtukana
Mwenyezi Mungu". Kama ambavyo zilivyoandika Sahih za Ahli-Sunnah
kwa ziyada ya matendo aliyoyatenda miongoni mwa mambo yanayopingana na Uislamu
kwa kuwauwa watu wema wasio na kosa ili achukue kwao kiapo cha utii kwa ajili
ya mwanawe Yazid. Vilevile kumuua kwake, Hassani ibn Ali (a.s.) kwa kumtumia
Ju'da binti Ash-ath, na maovu mengine mengi yanatajwa na historia kwa Masunni
kama ambavyo pia yanashuhudiwa na wafuasi wa Imam Ali (a.s.).
Mimi, ewe Bwana wangu, sikudhani kwamba ninyi mnaafikiana na hayo,
vinginevyo basi na tuyaache kama yalivyo, na ikifika hapo basi
hapatabakia baada ya hayo kipimo wala akili, wala sheria na wala hekima pia
dalili. Na Mwenyezi Mungu anasema: "Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu
na kuweni pamoja na wakweli." (Qur'an, 9:119)
Namuapa Mwenyezi Mungu, bila shaka mwanachuoni wa Kipakistan Abul-A'ala Al-Maududi, Mwenyezi Mungu amrehemu amesema kweli alipotaja katika kitabu chake kiitwacho, "Ukhalifa na lifetime" katika ukurasa wa 106 akimnukuu Al-Hasan Al-Basri aliposema, "Mambo manne alikuwa nayo Muawiyyah, lau angekuwa na jambo moja miongoni mwa hayo lingetosha kumuangamiza.
1) Kuchukua ukhalifa bila ya mashauriano ya Waislamu
na hali wamo miongoni mwao waliobakia Masahaba na wenye nuru ya ubora.
2) Kumpa Ukhalifa baada yake mwanawe mlevi ambaye alikuwa
akivaa hariri na kupiga magitaa.
3) Kumfanya Ibn Ziyad kuwa ni mwana wa baba yake na hali Mtume
(s.a.w.) amesema "Mtoto ni wa kitanda na mzinifu mwanaume atapata
jiwe."
4) Kumuua kwake Hujr na Jamaa za Hujr, basi ole wake kwa kumuua
Hujr na jamaa zake Hujr (akakariri mara tatu).
Basi Mwenyezi Mungu amrehemu Abu A'ala Al-Maududi, aliyepasua
ukweli, na lau angetaka angeongeza zaidi ya mambo haya manne yakawa mambo
arobaini lakini aliona kwamba hayo yanatosheleza kumuangamiza Muawiyyah.
Huenda Maududi alikuwa akichelea hisia za watu ambao wamejifunza
kwa watangulizi wao kumtukuza Muawiyya, kumuheshimu na kumuombea radhi, bali
hata mwanawe Yazid vile vile (kutukuzwa n.k.) kama nilivyosikia mimi mwenyewe
binafsi toka kwa Wanachuoni wenu huko India.
Lahaula wala Quwwata Illa Billahil-l-'Aliyyil-Adhim.
Kutokana na yote hayo mimi pia nilichelea hisia za wale watu
walioniita wasije wakanivamia, basi sikuwatajia chochote katika matukio hayo.
Kwa hiyo ewe bwana wangu, ninakulinganieni muwe na msimamo ulio
wazi mkitafuta radhi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa msimamo huo, kwani Mwenyezi
Mungu haichelei haki, na wala sikutakeni mkiri makosa ya watu hawa wala
kuisambaza aibu yao kwa kuwa historia inatutosheleza sisi
na ninyi kutuhadharisha juu ya hayo.
Lakini kinachotakiwa kutoka kwenu ni kukiri na muwafahamishe
wafuasi wenu kwamba, "Watu ambao hawaukubali Uimamu wa watu hawa (Muawiyya
Yazid, Abubakr, Omar na Uthman) na wala hawawatawalishi, wao ni Waislamu
wanaostahiki heshima na jambo hilo halina shaka, museme ya kwamba Mashia ni
wenye kudhulumiwa siku zote kwani wao hawakuufuata na kuukubali Uimamu wa mti
uliolaaniwa ambao Mwenyezi Mungu ameupigia mfano ndani ya Qur'ani.
Basi ni lipi kosa la Mashia kwa Mola wenu, ikiwa Mtume (s.a.w.)
anawaamuru Waislamu kuwafuata Watu wa nyumba yake baada yake, mpaka akawafanya
wao kuwa ni kama Safina ya Nuh, anaokoka mwenye kupanda
ndani yake na anaangamia anayeikwepa.
Na ni lipi kosa la Mashia ikiwa walitekeleza amri ya Mtume
aliposema: "Nimekuachieni vizito viwili, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na
Kizazi changu, vitu ambavyo mkishikamana navyo kamwe hamtapotea baada
yangu." Kama ambavyo zinashuhudia Sihah za Sunni
ukiachilia mbali vitabu vya Kishia.
Badala ya kuwashukuru (Mashia) na kuwatanguliza na kuwaboresha juu
ya wengine kwa kufuata kwao maamrisho ya Mtume (s.a.w.w.), tunawashutumu na
kuwakufurisha na kujitenga nao, jambo hili siyo uadilifu wala haliingii
akilini.
Ewe Bwana wangu, hebu tuachane na kauli za kijinga na za uongo
ambazo haziwezi kusimamisha dalili wala hoja na hazina uzito kwa wanataaluma
miongoni mwa watoto wa umma wetu kwamba, "Eti Mashia wanayo Qur'ani yao, au eti wao wanasema kwamba
aliyepewa Utume ni Ali, au kwamba Abdallah ibn Sabaa' Myahudi ndiye muanzilishi
wa Ushia."Na mengineyo miongoni mwa kauli dhaifu ambazo Mwenyezi Mungu
anashuhudia kuwa hayo ni miongoni mwa uzushi wa maadui wa Uislamu na maadui wa
Ahlul-Bait na wafuasi wao. Na hayo ni mambo hayakuzushwa isipokuwa ni kutokana
na ubinafsi mpotovu na ujinga wenye kero iliyopita kipimo.
Ewe Bwana wangu mpendwa mimi nauliza, "Wana daraja iliyoje
wanachuoni wa India kuliko ile ya wanachuoni wa Az-Har
Tukufu waliotoa Fat-wa inayoruhusu kufanya Ibada kwa mujibu wa Madhehebu ya
Shia Imamiyyah tangu miaka thelathini iliyopita? Na miongoni mwa Wanachuoni wa
Az-Har kuna aonaye kuwa fiqihi ya Mashia ya Jaa'fari ambayo wanaitumia Mashia
ni pana yenye manufaa na iko karibu mno na Roho ya Uislamu kuliko Madhehebu
nyinginezo ambazo zinaitegemea. Na anayewaongoza Wanachuoni hawa (kwa fikra
hii) ni Mtukufu Marehemu Sheikh Mahmud Shal-Tut Mwenyezi Mungu amrehemu, ambaye
aliiongoza Az-har katika uhai wake.
Je hivi wanachuoni kama hawa hawaujui Uislamu na Waislamu? Au
wanachuoni wa India ni wajuzi mno kuliko wanachuoni hao?
Mimi siwadhanieni kabisa kwamba ninyi mnasema namna hiyo...!!
Ewe Bwana wangu Mtukufu, mategemeo yangu kwenu ni thabiti na moyo
wangu kwenu uko wazi kwa mapenzi na huruma, na hapo zamani nilikuwa kama ninyi
nimefunikwa sioni haki wala Ahlul-Bait (a.s.) na wafuasi wao. Mwenyezi Mungu
akaniongoza kuelekea kwenye haki ambayo hapana baada yake ila upotovu, na
nikawa huru kutokana na minyororo ya ung'ang'anizi na kufuata kama kipofu, na
nilifahamu kwamba wengi wa Waislamu bado wamefunikwa na habari zisizo na ukweli
na za uzushi. Kampeni zilizoandaliwa kuwapa baadhi ya watu utukufu wasiostahili
zinawazuwia (Waislamu) kuufikia ukweli ili wote wapate kupanda meli ya uokovu
na washikamane na kamba imara ya Mwenyezi Mungu, na hakuna tofauti kama mjuavyo
baina ya Sunni na Shia isipokuwa ni katika yale waliyotofautiana kwa ajili ya
Ukhalifa baada ya Mtume, na msingi wa tofauti ni itikadi yao kuhusu Masahaba,
nao Masahaba (r.a.) walitofautiana kati yao mpaka wakalaaniana, kupigana na
kuuana wao kwa wao. Ikiwa kutofautiana kati yao ni kutoka katika Uislamu basi Masahaba
ndiyo wa mwanzo kutuhumiwa kwa tuhuma hii na Mwenyezi Mungu apishe mbali.
Mimi siitakidi kwamba ninyi mnayaridhia hayo, na uadilifu
unakulinganieni msiridhiye Mashia kutolewa nje ya Uislamu, kama ambavyo
Mashia wana desturi ya kuwatukuza Ahlul-Bait (a.s.) na kuwaheshimu vile vile
Masunni wanayo desturi ya kuwatukuza Masahaba wote, na misimamo hii miwili iko
mbali mbali.
Basi ikiwa Mashia kwa desturi yao hiyo wanakosea, basi Masunni ndiyo
watakaokuwa wanakosea zaidi (katika desturi yao)
kwani Masahaba wote wanawatanguliza Ahlul-Bait (a.s.) kuliko nafsi zao, na
huwatakia rehma kama wamtakiavyo rehma Mtume (s.a.w.w.). Na
hatumfahamu yeyote miongoni mwa Masahaba (r.a.) aliyeitanguliza nafsi yake au
aliyejitukuza juu ya watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w.) katika elimu au matendo
mema.
Basi wakati umefika kuliondosha giza la kihistoria kwa wafuasi wa
Ahlul-Bait (a.s.), kushirikiana nao, kuunga udugu, kusaidiana
kwa mema na kumcha Mwenyezi Mungu na
imetosha kwa umma huu kumwaga damu na kusambaza fitna.
Huenda Mwenyezi Mungu Mtukufu akaunganisha kupitia kwenu kauli (ya
umoja) na kuuondoa utengano, akalitibu jeraha hili na akauzima moto wa fitina
na kumdhalilisha shetani na kundi lake na mtakuwa ninyi mbele ya Mwenyezi Mungu
ni wenye kufaulu hasa kwa kuwa ninyi mnatokana na kizazi kitukufu kama
ninavyosikia.
Basi fanyeni hayo ili mpate kufufuliwa pamoja nao. "Na hakika
umma wenu ni mmoja nami ndiye Mola wenu. " "Na waambie, fanyeni
Mwenyezi Mungu ataona matendo yenu na Mtume wake na waumini".
Mwenyezi Mungu akuwafikisheni ninyi na sisi kwa mambo ambayo
ndani yake kuna kheri ya nchi na waja, Mwenyezi Mungu akujaalieni ninyi na sisi
kuwa miongoni mwa wenye kutenda (mema) wenye utakaso kwa ajili ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu.
Nakutumieni kwa heshima yenu pamoja na barua hii nakala ya kitabu
changu "Thummah-Tadaitu" ambacho nilikitunga maalumu kuhusiana na
maudhui haya, hiyo ni zawadi yangu kwenu huenda kikapata kukubalika mbele yenu.
Was-salaam Alaikum Warahmatullahi Taala wa Barakatuh.
Muhammad Tijani As-Samawi At-Tunisi
No comments:
Post a Comment