Wednesday 23 April 2014

MAONI YA QUR’AN KUHUSU MASAHABA WA MTUME
Assalaam alaykum. Kwanza kabisa ninachukua nafasi hii kuwashukuru Masahaba wa Mtume waliokuwa wema na waliomsaidia katika ujumbe wake bila kuwa na ajenda za siri dhidi ya Uislamu. Bila shaka Qur’an imekuja na aya nyingi kuwasifu Masahaba hawa. Pamoja na kuwa na Masahaba wema, wapo vile vile Masahaba waliokuwa si wema na Qur’an imewalaumu katika aya zifuatazo:
1. Na Mohammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwishapita kabla yake mitume wengi. Je, akifa au akiuawa ndio mtageuka kurudi nyuma (kurtadi)? Na atakayegeuka na kurudi nyuma hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Na Allah atawalipa wanaoshukuru (Qur’an 3:144).
2. Wachache katika waja wangu ndio wenye kushukuru (Qur’an 34:13).
3. Enyi mlioamini mna nini mnapoambiwa: Nendeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, mnajitia uzito katika ardhi? Je mmeridhia maisha ya dunia kuliko ya akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia ni chache kuliko za akhera. Kama hamuendi atakuadhibuni adhabu chungu na atawaleta watu wengine wala ninyi hamtamdhuru chochote, na Allah ni Muweza wa kila kitu (Qur’an 9:38-39).
4. Na mkirudi nyuma, (Allah) atabadilisha (alete) watu wengine wasiokuwa ninyi kisha hawatakuwa kama ninyi (Qur’an 47:38).
5. Je, haujafika wakati kwa wale walioamini, nyoyo zao zinyenyekee kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kwa mambo ya haki yaliyotelemka, na wala wasiwe kama wale waliopewa kitabu hapo kabla na muda wao (wa kuondokewa na Mitume) ukawa mrefu, kwa hivyo nyoyo zao zikawa ngumu na wengi wao wakawa waasi (57:16).
6. Na wawepo miongoni mwenu watu wanaolingania wema na kukataza maovu, na hao ndio watakaotengenekewa. Na wala msiwe kama wale waliofarikiana na kukhitilafiana baada ya kuwafikia dalili zilizo wazi, na hao ndio watakao kuwa na adhabu kubwa. Siku ambayo nyuso zitanawiri na nyuso zingine zitasawajika, wataambiwa: je mlikufuru baada ya kuamini kwenu? Basi onjeni adhabu kwa vile mlivyokuwa mnakufuru. Ama wale ambao nyuso zao zitanawiri watakuwa katika rehema ya Allah. Wao humo watakaa milele (Qur’an 3: 104-106)
Ndani ya kitabu kiitwacho Ad-Durul Manthur cha Jalaludin As-Suyut imeandikwa: Pindi Masahaba walipofika Madina, wakapata maisha mazuri ambayo hawakuwa nayo kabla, wakazembea kutenda baadhi ya wajibu waliokuwa juu yao, hivyo wakakemewa kwa aya ya 5 iliyotangulia hapo juu.
Na katika riwaya nyingine itokanayo na Mtume Mohammad inasema kuwa Allah aliziona nyoyo za Muhajirina kuwa ni nzito (hata) baada ya miaka 17 ya tangu kushuka Qur’an, basi akateremsha kauli yake, “Je haujafika wakati kwa wale walioamini?
Aya hizi zinaonesha wazi kuwa kuna masahaba ambao hawakuwa wanyenyekevu mbele za Mwenyezi Mungu na Mtume wake, vinginevyo Mwenyezi Mungu asingewalaumu au kuwashauri wabadirike tabia zao.
Ama suala la Masahaba kukhitilafiana sidhani kama kuna mtu anaweza kupinga na kudai kuwa hawakukhitilafiana kwani walifikia mahala pa kupigana vita wao kwa wao. Mfano Sayyidina Uthuman aliuwawa na kundi la Masahaba. Imam Ally (a.s) akiwa na alipigana vita na kundi la Masahaba kama Aysha, Zuberi na Twalha. Vile vile alipigana vita na Muawiyyah bin Abusufian ambaye naye alikuwa sahaba wa Mtume.
Haiwezekani kwa makundi haya yenye kupigana kwamba yatakuwa yote katika haki. Hivyo kuna ulazima wa kutafuta haki iko wapi kabla ya kuliunga mkono kundi lolote miongoni mwa haya.
Kumbuka Mtume anasema pale watapokhitilafiana watu, tafadhali shikamaneni na Imam Ally kwani haki iko pamoja naye daima. Kwa mantiki hii kundi linalomfanya Imam Ally kuwa kiongozi wao wa kwanza baada ya Mtume kufariki tu huenda litakuwa katika njia sahihi zaidi. Kwani muda mfupi baada ya Mtume kufa ndio vurugu zilipoanza. Utakumbuka Sayyidna Umar alipotangaza kuwa Mtume hajafa hadi wakafiri waishe na kwamba atakayesema kuwa Mtume kafa atamkata kichwa. Hii sio imani ya kiislamu na khitilafu zilianzia hapa.

No comments:

Post a Comment