Ewe Mwenyezi Mungu wanadamu tumekhitilafiana na kuwa
Wayahudi, Wakristo na Waislamu, ama wayahudi wamekhitilafiana na kuwa makundi
71, Wakristo wamekhitilafiana na kuwa makundi 72, waislamu nao wamekhitilafiana
na kuwa makundi 73 na yote yamo katika upotofu isipokuwa kundi moja tu, Kama
alivyosema Mtume wako Mohammad (S.A.W.W). Je huu ndio utaratibu uliouweka kama
wanavyosema baadhi ya waislamu kuwa Wewe ndiwe uliyeiandikia kila nafsi ikiwa
bado tumboni mwa mama yake; iwe Yahudi, Mkristo, Muislamu, mwizi, mshirikina,
mlafi, mcha Mungu, muuaji, mchawi n.k. na hatimaye mtu akawa hivyo alivyo?
Kwa hakika nafsi yangu haikubali fikra hizi ya kwamba Qadhaa
na Qadar ndiyo iliyoamua hatima ya mtu kimatendo yake, bali karibu nikate
shauri kwamba wewe Mwenyezi Mungu ndiwe uliyetuumba, ukatuongoza na
ukatufahamisha mabaya na mema, ukatuagiza tufanye mema na kuacha mabaya, na
ukawatuma Mitume wako ili watubainishie yanayotutatiza na watujulishe haki
kutokana na batili lakini mtu mwenyewe ndiye aliyezugwa na maisha ya dunia na
mapambo yake akasahau maelekezo yako.
Kwa ubinafsi na ujeuri wake, kwa ujinga wake na kujitosa
kwake katika mambo yasiyo na faida, na kwa inadi yake na uhasama wake, na kwa
dhulma yake na kuvuka kwake mipaka, ameiacha haki na kumfuata shetani na
akajitenga na wewe Muumba wake. Bila shaka Qur’an tukufu imekwisha lieleza hilo,
“Kwa hakika Mwenyezi Mungu hawadhulumu watu kitu chochote lakini watu
wanajidhulumu wenyewe (10:44).
Na Mtume wako alitutahadharisha sana pale aliposema, “sio
halali kwa muislamu kumnunia ndugu yake muislamu zaidi ya siku tatu,” lakini
bado tumegawanyika na kuwa vidola vidogo vidogo vinavyofanyiana uadui vyenyewe
kwa vyenyewe na kupigana wao kwa wao.
Umma huu unanini ewe Mwenyezi Mungu, baada ya kuwa ulikuwa
umma bora kuliko umati zote na ulipata nguvu duniani na kuwafikishia watu
uongofu, elimu, maarifa na maendeleo, ghafla leo hii umekuwa ni umma mdogo na
dhaifu mno, ardhi yao imeporwa na wananchi wake wametawanyika na msikiti wao
mtakatifu umekaliwa na kupokonywa na wazayuni na wala hawawezi kuukomboa. Hivi
na hii nayo umetuandalia tuwe hivi? La hasha kwani fikra inapingana na malengo
wako matukufu ya kuuinua Uislamu ili uiongoze dunia. Naomba ewe Mola wangu kama
fikra zangu ni sahihi niimarishe katika fikra hizi na niweke pamoja na watu
wenye fikra kama zangu. Na kama nimepotoka ninakuomba uniongoze njia
iliyonyooka kwani wewe ndiye mbora wa waongozaji.
No comments:
Post a Comment