Assalaam alaykum. Kwanza kabisa ninachukua nafasi hii
kuwashukuru Masahaba wa Mtume waliokuwa wema na waliomsaidia katika ujumbe wake
bila kuwa na ajenda za siri dhidi ya Uislamu. Bila shaka Qur’an imekuja na aya nyingi
kuwasifu Masahaba hawa. Pamoja na kuwa na Masahaba wema, wapo vile vile
Masahaba waliokuwa si wema na Qur’an imewalaumu katika aya zifuatazo:
1. Na Mohammad hakuwa ila ni Mtume tu.
Wamekwishapita kabla yake mitume wengi. Je, akifa au akiuawa ndio mtageuka
kurudi nyuma (kurtadi)? Na atakayegeuka na kurudi nyuma hatamdhuru kitu
Mwenyezi Mungu. Na Allah atawalipa wanaoshukuru (Qur’an 3:144).
2. Wachache katika waja wangu ndio wenye
kushukuru (Qur’an 34:13).
3. Enyi mlioamini mna nini mnapoambiwa:
Nendeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, mnajitia uzito katika ardhi? Je
mmeridhia maisha ya dunia kuliko ya akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia
ni chache kuliko za akhera. Kama hamuendi atakuadhibuni adhabu chungu na
atawaleta watu wengine wala ninyi hamtamdhuru chochote, na Allah ni Muweza wa
kila kitu (Qur’an 9:38-39).
4. Na mkirudi nyuma, (Allah)
atabadilisha (alete) watu wengine wasiokuwa ninyi kisha hawatakuwa kama ninyi
(Qur’an 47:38).
5. Je, haujafika wakati kwa wale
walioamini, nyoyo zao zinyenyekee kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kwa mambo ya
haki yaliyotelemka, na wala wasiwe kama wale waliopewa kitabu hapo kabla na
muda wao (wa kuondokewa na Mitume) ukawa mrefu, kwa hivyo nyoyo zao zikawa
ngumu na wengi wao wakawa waasi (57:16).
6. Na wawepo miongoni mwenu watu wanaolingania
wema na kukataza maovu, na hao ndio watakaotengenekewa. Na wala msiwe kama wale
waliofarikiana na kukhitilafiana baada ya kuwafikia dalili zilizo wazi, na hao
ndio watakao kuwa na adhabu kubwa. Siku ambayo nyuso zitanawiri na nyuso
zingine zitasawajika, wataambiwa: je mlikufuru baada ya kuamini kwenu? Basi
onjeni adhabu kwa vile mlivyokuwa mnakufuru. Ama wale ambao nyuso zao
zitanawiri watakuwa katika rehema ya Allah. Wao humo watakaa milele (Qur’an 3:
104-106)
Ndani ya kitabu kiitwacho Ad-Durul Manthur cha Jalaludin
As-Suyut imeandikwa: Pindi Masahaba walipofika Madina, wakapata maisha mazuri
ambayo hawakuwa nayo kabla, wakazembea kutenda baadhi ya wajibu waliokuwa juu
yao, hivyo wakakemewa kwa aya ya 5 iliyotangulia hapo juu.
Na katika riwaya nyingine itokanayo na Mtume Mohammad inasema
kuwa Allah aliziona nyoyo za Muhajirina kuwa ni nzito (hata) baada ya miaka 17
ya tangu kushuka Qur’an, basi akateremsha kauli yake, “Je haujafika wakati kwa
wale walioamini?
Aya hizi zinaonesha wazi kuwa kuna masahaba ambao hawakuwa
wanyenyekevu mbele za Mwenyezi Mungu na Mtume wake, vinginevyo Mwenyezi Mungu
asingewalaumu au kuwashauri wabadirike tabia zao.
Ama suala la Masahaba kukhitilafiana sidhani kama kuna mtu
anaweza kupinga na kudai kuwa hawakukhitilafiana kwani walifikia mahala pa
kupigana vita wao kwa wao. Mfano Sayyidina Uthuman aliuwawa na kundi la
Masahaba. Imam Ally (a.s) akiwa na alipigana vita na kundi la Masahaba kama
Aysha, Zuberi na Twalha. Vile vile alipigana vita na Muawiyyah bin Abusufian ambaye
naye alikuwa sahaba wa Mtume.
Haiwezekani kwa makundi haya yenye kupigana kwamba yatakuwa
yote katika haki. Hivyo kuna ulazima wa kutafuta haki iko wapi kabla ya
kuliunga mkono kundi lolote miongoni mwa haya.
Kumbuka Mtume anasema pale watapokhitilafiana watu, tafadhali
shikamaneni na Imam Ally kwani haki iko pamoja naye daima. Kwa mantiki hii
kundi linalomfanya Imam Ally kuwa kiongozi wao wa kwanza baada ya Mtume
kufariki tu huenda litakuwa katika njia sahihi zaidi. Kwani muda mfupi baada ya
Mtume kufa ndio vurugu zilipoanza. Utakumbuka Sayyidna Umar alipotangaza kuwa
Mtume hajafa hadi wakafiri waishe na kwamba atakayesema kuwa Mtume kafa
atamkata kichwa. Hii sio imani ya kiislamu na khitilafu zilianzia hapa.
No comments:
Post a Comment