Saturday, 31 August 2013

MAANDIKO YANAYOHUSU UKHALIFA



Ukichunguza kwa makini Hadith za Mtume utakuta kuwa ukhalifa wa Imam Ally uko wazi kabisa na haupingiki.  Ebu soma hadith ya Mtume ifuatayo:
Yeyote ambaye mimi nikuwa mtawala wa mambo yake, basi huyu Ally naye ni mtawala wake.
Maneno haya aliyasema Mtume wetu baada ya kutoka katika Hijjah ya kuaga kiasi kwamba yalifanyika maandamano ya kumpa Imam Ally mkono wa kuonesha utii kwake (baia). Abubakar na Umar walikuwa miongoni mwa watu waliotoa pongezi kwa Imam Ally kwa kutangazwa kuwa kiongozi wao, wakisema, “Hongera ewe mwana wa Abu Talib, leo umekuwa mtawalia mambo kwa kila muumini wa kike na kiume”.
Tazama:
1.      Musnad Imam Ahmad ibn Hambal Juz. 4 uk. 281
2.      Sirul – Alamina cha Imam Ghazal uk 12
3.      Tarikh Ibn Asakir juzuu.2 uk. 50
4.      Ar-Riyaz Un-Nazrah cha Tabari juzuu. 2 uk. 169
5.      Kanzul Ummal juzuu.6 uk. 397
6.      Al-Bidaya wa-Nihaya cha Ibn Kathir j. 5 uk. 212
7.      Al-Hawi Lil-Fatawi cha Suyut j.1 uk. 112
Ama ile ijmai (makubaliano) inayodaiwa kuwa ilimchagua Abubakar pale Saqifah, kisha kumpa baia Msikitini haina ushahidi wa kutosha  kwani Masahaba wengi tu walipinga na baadhi yao ni: Ali, Abbas na banu Hashimu wengine, Usama bin Zaid, Zubair, Salman Farsii, Abudhar Ghiffar, Miqdad bin Aswad, Ammar bin Yasir, Hudhaifa ibn Yaman, Khuzaimah ibn Thabit, Abu Buraidah Aslam, Al-Barraa ibn Azib, Ubay ibn Kaab, Sahl ibn Hunaif, Saad ibn Ubadah, Qais ibn Saad, Abu Ayub Answar, Jabir ibn Abdillah na Khalid ibn Said.
Tazama: Tarekh Tabari, Tarith ibn Al-Athir, Tarikh Al-Khulafa, Tarikh Al-Khamis, Al-Istiiabu na kila aliyeandika kuhusu baia ya Abubakar.
Bila shaka Umar bin Khatab alishuhudia mwenyewe kuwa baia ile ilikuwa ya ghafla, Mwenyezi Mungu aliwakinga waislamu na shari yake, na akaendelea kusema, “Yeyote atakayerudia kufanya baia kama hiyo muuweni” na mahala pengine akasema, “yeyote mwenye kufanya kampeni kama hiyo asipewe baia wala Yule aliyembai”.
Tazama: sahihi Bukhar J. 4 uk. 127
Naye Saad ibn Ubadah, kiongozi wa Maanswar aliwapinga katika kampeni yao pale Saqifah kiasi kwamba alikuwa hasali pamoja na Abubakar na Umar, au nyuma yao wala hafuatani nao katika Arafah. Alibakia hivyo mpaka alipokufa huko Shamu katika ukharifa wa Umar bin Khatab.
Tazama; Tarikh Khulafah J. 1 uk. 17.
Kwa hiyo kauli ya Mashia kuhusu Ukhalifa ndio sahihi, kwani imethibiti kupatikana kwa maandiko juu ya ukhalifa wa Imam Ally kwa masunni wenyewe, na wameyafanyia taawili ili kulinda heshima ya masahaba, lakini kwa mtu muadilifu hana njia ya kukwepa, isipokuwa kukubali maandiko hayo, na hasa pindi atakapotambua utata uliomo ndani ya jambo hili.
Tazama: Saqifah wal-Khilafah cha Abdul-Fatah Abdul Maqsud na As-Saqifah cha Sheikh Muhammad Ridhaa Mudhafar. 

No comments:

Post a Comment