Friday, 16 August 2013

MASAHABA SIKU YA SULHU YA HUDAIBIYA



Katika mwaka wa 6 hijiria, Mtume na masahaba wake (1400) walitoka Madina kwenda Makah kuhiji. Walipofika eneo liitwalo Dhil-halifah walivaa Ihram na pia aliwaagiza waweke panga zao katika ala. Wakawatanguliza ngamia kwa ajili ya kuchinja ili kuwatambulisha Maquraish kuwa wamekwenda kwa ajili ya hija na wala sio vita.
Makuraish kwa kiburi chao walimtumia mjumbe aitwaye Suhail na ujumbe kuwa Mtume arudi alikotoka na kwamba mwaka ujao watamwachia Makkah kwa muda wa siku tatu. Ujumbe huu uliambatana na mkataba wenye masharti magumu lakini Mtume aliyakubali kwa kutegemea maslahi ambayo Mola wake mtukufu alimfunulia.
Hata hivyo baadhi ya Masahaba walimpinga kwa nguvu zao zote na Umar bin Khatab akamwendea Mtume na kumuuliza, “Je, wewe siyo Mtume wa Mwenyezi Mungu wa haki?” Mtume akajibu, “bila shaka mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu wa haki.” Umar akauliza tena, “je sisi hatuko kwenye haki na adui yuko kwenye batili?” Mtume akajibu, “bila shaka ndivyo.” Umar akauliza, “basi ni kwa nini tunaonesha udhaifu katika dini yetu?” Mtume akamwambia, “bila shaka mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na siwezi kumuasi Mola wangu, naye ndiye hunilinda.” Umar akauliza tena, “je, si ulikuwa ukituambia kuwa tutaingia kwenye nyumba tukufu na kuitufu?” Mtume akasema, “bila shaka nilisema, lakini, je nilikuambia tutaingia mwaka huu? Umar akasema, “hapana.” Mtume akasema, “bila shaka utaingia na utaitufu.”
Hatimaye Umar bin Khatabu hakuridhika na majibu ya Mtume hivyo akaenda kumuuliza maswali yale yale Abubakar bin Quhafah.
Basi Mtume alipomaliza kusaini mkataba wa hudaibiyyah aliwaambia Masahaba wake wasimame wachinje na wanyoe. Wallahi hakuna miongoni mwao aliyesimama mpaka akasema mara tatu na ilivyokuwa hapana aliyetekeleza amri yake, aliingia kwenye hema lake kisha akatoka na wala hakumsemesha yeyote kati yao, akachinja mnyama wake na akamuita kinyozi wake akamnyoa.
Masahaba walipoona hali hiyo, walisimama, wakachinja na wakawa wananyoana wao kwa wao, karibu wauane wao kwa wao. Kisa hiki kimeandikwa na waandishi wa Sira na Tarekh, kama ambavyo amekiandika Bukhari ndani ya sahihi yake katika Kitabus-Shurut fil-jihad, juz. 2 uk. 122. Pia Sahih Muslim katika babu Sul-hul-hudaibiyah juz. 2.
Hivi huu ndio utii wa Masahaba kwa Mtume wao? Je Masahaba hawa hawakuisoma Qur’an 4:65 ambapo Mwenyezi Mungu amesema, “Naapa kwa Mola wako, hawawi waumini mpaka wakufanye wewe uwe muamuzi katika yale wanayozozania baina yao. Kisha wasione uzito katika nafsi zao kwa yale uliyoyaamua na wasalimu amri mara moja.”
Je Umar bin Khatab alisalimu amri mara moja mahali hapo na hakuona uzito ndani ya nafsi yake kwa maamuzi aliyoyafanya Mtume? Bila shaka Umar na wenziwe walionesha mashaka makubwa juu ya hukumu aliyoifanya Mtume wao kinyume na maagizo ya Allah (S.W)

No comments:

Post a Comment