Monday, 16 November 2015

BINTI WA NABII MUHAMMAD (s.a.w.w.)

BINTI WA NABII MUHAMMAD (s.a.w.w.)

Yeye  ni  Fatima  Zahra; Baba yake ni Rasulullah (Mjumbe na Mtume wake Mwenyezi Mungu) Muhammad bin Abdullah (s.a.w.w.); na mama yake ni Bibi Mtukufu Khadija Mama wa Waislamu, na mumewe ni bwana wa mawasii Ali Ameerul-Muuminiin, na watoto wake na wajukuze ni maimam watoharifu (juu yao Rehma na Amani).
Alizaliwa Bibi Fatima (a.s.) siku ya mwezi ishirini, mwezi wa mfungo tisa, mwaka wa arobaini na tano toka alipozaliwa Mtume (s.a.w.w).
Na akafa bibi huyo siku ya Jumanne mwezi tatu, mfungo tisa, mwaka wa kumi na moja wa Hijiria [5]. Na umri wake ni miaka kumi nanane.
Na akasimamia matendo ya kifo chake Amirul Muminiin Ali (a.s.), akamzika Madina Munawwara (Mji wenye nuru, mji wake Mtume, uliopo katika Saudia Arabia), na akalificha kaburi lake kama alivyo usia mwenyewe Bibi Fatima.
Alikuwa bibi huyo kama baba yake kwa ibada na kumcha Mungu na ubora, na zimeshuka katika sifa zake aya nyingi za Qur'ani al-Hakim.
Alikuwa Mtume (s.a.w.w.) akimwita "Bibi wa wanawake wa Ulimwenguni", na akimpenda mapenzi mazuri mpaka yeye akiwa anaingia kwa Mtume (s.a.w.w.) humkaribisha na kusimama na kumkalisha mahali pake, pengine humbusu mikono yake.
Na Mtume (s.a.w.w.) akasema: "Mungu huridhika analoridhika nalo Fatima na hukasirika Unalo mkasirisha Fatima."
Pia Mtukufu Mtume amesema: "Wabora wa wanawake wa peponi ni wanne: Mariam Binti Imrani, na Khadija Binti Khuwailid, na Fatima Binti Muhammad (s.a.w.w.) na Asia Bint Muzaahim.
Mtu mmoja akamwuliza bibi Aaisha "Mtu gani alikuwa mpenzi mno wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.)? Akajibu: Fatima.
Kisha akamwuliza: Ni gani kutokana na wanaume? Akajibu: Mume wake Bibi Fatima, yaani Ali bin Abi Talib (as.).
Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) akasema: "Hakika, Mwenyezi Mungu ameniamrisha mimi nimwoze Fatima kwa Ali (a.s.).
Kazaa bibi huyo kwa Amirul Muuminiin Ali (a.s.): Imam Hassan (a.s.), Imam Hussein (a.s.), Bibi Zainab (a.s.), Bibi Ummu Kulthum (a.s.) na Muhsin (a.s.)- Lakini bwana Muhsin kafa tumboni zama alipopata mama yake msukosuko wa maadui. Kwa hiyo jumla ya watoto wa bibi Fatima ni 5.
Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) amesema: "Kila mtoto huchukuwa ukoo wa baba yake isipokuwa vizazi vya Fatima, kwani mimi ndiyo walii wao na nasaba wao (yaani, vizazi vya Fatima wote ukoo wao unatokana kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Pia Mtume Mtukufu amesema:- "Kila ukoo na uhusiano utafutika siku ya qiyama isipokuwa ukoowangu na uhusiano wangu.

JANNAT AU PEPO

JANNAT AU PEPO
Assalaam alaykum.
Jannat ni mahala pema kabisa ambapo Allah (s.w) amewaandalia watendao mema na kujiepusha na maovu.
Katika ukurasa wa 279, juzuu 13 ya kitabu Lisan al-'Arab, twaambiwa kuwa pepo inaitwa Jannat 'Adan ikimaanisha kuwa ni "Mahala pa milele", Bustani ya Kati (al-awsat)."
Kitabu hichohicho kinatutambulisha katika uk.427, juzuu ya 7 kuwa al-awsat inaweza kumaanisha kuwa: iliyo Bora. Hakuna shaka kuwa tutaweza kuona na kupata maelezo na mafafanuzi zaidi juu ya Jannat 'adan kuliko kusema tu al-firdows, Jannat au Peponi, katika Qur'an Tukufu. Hali hii inatuacha sisi kwa kudadisi kuwa mahala bora kabisa, na iliyokuu, inayolengwa katika Jannat zote ni Jannat 'Adan.
Peponi, au al-Firdows kama vile inavyoitwa katika Kiarabu, ni neno la kuazimwa. Waarabu aliowatokezea Mtume Muhammad (s.a.w.w.) walikuwa hawana itikadi ya maisha baada ya kufa, na Jannat na Jahannam. Na kwa hakika swala hili lilikuwa gumu kwake Mtume (s.a.w.w.) alipoanza kuhubiri. Sura-i-Yasin, 36, Ayah ya 78 inatuelezea, 'Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake - akasema: "Nani atakayeihuisha mifupa na hali imesagika?"
Vile vile Qur'an inatujibu katika, Sura Ya-Sin, 36; Ayah 79: Sema: "Ataihuisha yule aliyeiumba mara ya kwanza, naye ni Mjuzi wa kila (namna ya) kuumba"
Hata mwandishi wa kazi nzuri kabisa za Kiarabu, Lisan Al-'Arab, hana uhakika iwapo neno hili la Firdaws limeazimwa kutoka Kilatini au Kiajemi, au ni al-Majlisi, kama mwandishi huyo anavyokubali katika uk. 91, Juzuu ya 8 kati ya Juzuu 110 ya Encyclopedia - bila ya kuihesabu Juzuu ya Sifuri - ijulikanayo kwa jina la Bihar al-Anwar. Wazo la tatu, ambalo linaweza kuwa sahihi zaidi ni kwamba inawezekana uasili wake ukawa Babilonia.
Neno lingine lililotumika katika Qur'an Tukufu ni Jannat au Bustani. Lakini kwetu sisi Jannat inamaanisha sana kuliko kutaja Bustani au shamba la miti ya matunda. Waarabu kamwe hawakuwa na tabia ya kuishi katika mshamba yao ya miti ya matunda.
Mtume (s.a.w.w) anasema, "Wakati Allah (sw) aliponiruhusu kwenda Jannat, Jibrail a.s. aliniambia, "Mimi nimeamrishwa kukutembeza na kukuonyesha yote yaliyomo ndani mwa Jannat na Jahannam." Hivyo mimi niliiona Jannat na baraka na mema yote yaliyokuwamo na vile vile nimeiona Jahannam pamoja na mateso yote yaliyomo. Jannat inayo milango minane, kila mlango unayo misemo minne, ambayo kila mojawapo ni bora kuliko ulimwengu mzima na kile ambacho kipo ndani mwake ni kwa ajili ya wale wanaotafakari na kufuatilia kwa kutenda kimatendo.
Na Jahannam inayo milango saba, na kila mlango inayo misemo mitatu, ambapo kila msemo ni afadhali kuliko dunia yetu hii na kilichomo ndani mwa kila msemo ni kwa ajili ya kutafakari na kuyatendea kazi. Malaika Jibraili (a.s.) aliniambia, "Ewe Muhammad! Soma yaliyoandikwa katika milango hii!" Na hivyo mimi niliyasoma yote.
Ufafanuzi zaidi utakujia baadaye Insha – Allah

Thursday, 12 November 2015

HALI NA HAKI ZA MTOTO KATIKA UISLAMU

HALI NA HAKI ZA MTOTO KATIKA UISLAMU
Umoja wa mataifa umeanza kuonyesha kuvutiwa na suala la watoto kwa kufanya maadhimisho ya ‘Siku ya Watoto’ katika mwezi wa Novemba kila mwaka, ambayo inalingana na maadhimisho ya kutangazwa kwa haki za mtoto.
Ukweli ni kuwa mazingatio ya Uislamu kwa watoto yameanza zamani na yanarejea nyuma zaidi ya miaka elfu moja na mia nne.
Uislamu kwa mfululizo unaadhimisha na kuonyesha huruma yake kwa mtoto, si baada ya kuzaliwa tu, bali hata kabla ya kuzaliwa, na umeelezewa kwa makini haki zake.
Wakati wa utoto katika Uislamu umepewa picha ya ulimwengu mzuri wa furaha, uzuri, ndoto, mapenzi na ndoto njema.
Na aya za Qur’ani zinaonyesha mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa watoto, na ndipo akaapa Mwenyezi Mungu: “Naapa kwa mji huu, (wa Makkah).  Na wewe utahalalishwa katika mji huu. Na (kwa) mzazi na alichokizaa.” (90:1-3).
Watoto wameelezwa katika Qur’ani kuwa ni bishara njema. Amesema Mwenyezi Mungu:
 “Ewe Zakaria tunakupa habari njema ya (kupata) mtoto jina lake ni Yahya….” (19:7).
Pia watoto ni kiburudisho cha macho yetu. Amesema Mwenyezi Mungu:
 “Ewe Mola wetu, tupe katika wake zetu na watoto wetu watakaoyaburudisha macho yetu….”(25:74).
Na watoto ni pambo la maisha katika ulimwengu huu: “Mali na watoto ni pambo la maisha ya duniani….” (18:16).
Mtume (s.a.w.) anatudhihirishia ya kuwa ulimwengu wa utoto ni kama pepo, pale aliposema: “Watoto ni vipepeo vya Peponi.”
Kuwatunza watoto ni jambo la lazima, na kuwapenda humleta mtu karibu na Mwenyezi Mungu. Mtume (s.a.w.) amesema: “Lau kama si watoto wanyonyeshwao, na wazee wanaorukuu (kwa kuswali) na wanyama walishwao mashambani, basi mngelipatwa na adhabu kali.”
Inaonyesha wazi kwamba huruma na uangalifu wa Mwenyezi Mungu kwa watoto ndiyo uliofanya Mwenyezi Mungu kuzuia adhabu juu ya watu wake.
  1. Mapenzi Ya Mtume Kwa Watoto
Mapenzi ya Mtume (s.a.w.) kwa watoto yalijaa ndani ya moyo wake mwema, imeelezwa katika Hadith: “Siku moja Mtume (s.a.w.) alipanda juu ya mimbari akiwahutubia watu, (mara) akawaona Hasan na Husein (a.s.) wanakimbia na huku wakijikwaa, akakatiza hotuba yake, akashuka kutoka juu ya mimbari kwenda kuwapokea watoto hao wawili. Akawabeba mikononi mwake, kisha akapanda tena juu ya mimbari akasema: “Enyi watu, hakika mali zenu na watoto wenu ni fitina, Wallahi nimewaona wajukuu wangu wawili wakikimbia na kujikwaa, basi sikuweza kujizuia mpaka nimeshuka nikawabeba.”
Siku moja Mtume (s.a.w.) alikuwa anaswali, mara Hasan na Husein (a.s.) wakaingia ndani na kumpanda mgongoni kwake wakati alipokuwa amesujudu, Mtume (s.a.w.) akaendelea kusujudu tu. Alichukia kuwaharakisha washuke, mpaka waliposhuka wao wenyewe. Kisha alipotoa salaam na kumaliza Swala, akaulizwa na maswahaba wake sababu zilizomfanya asujudu kwa kitambo kirefu hivyo; akawajibu: “Wajukuu wangu wawili walikuwa wamepanda juu ya mgongo wangu nami nilichukia kuwahimiza washuke kwa haraka.”
Mtume (s.a.w.) alizoea kuharakisha Swala yake pindi asikiapo mtoto analia, na husema: “Mimi huchukia kumchosha mama yake.”
Siku moja alikuwa anapita nyumbani kwa Fatima (a.s.) (binti yake), akamsikia mjukuu wake Husein (a.s.) akilia, aliingia ndani na baada ya kumkemea Fatima akasema: “Je hujui kwamba nimsikiapo Husein akilia huwa nakereka?”
Siku moja Mtume (s.a.w.) alitembelewa na Al-Akraa Ibn Habis, ambaye alimwona Mtume (s.a.w.) akiwabusu wajukuu zake, Al-Akraa akasema: “Unawabusu watoto wa binti yako? Naapa kwa Mungu nina watoto kumi, na sijawahi kumbusu hata mmoja.”
Mtume (s.a.w.) akamjibu: “Je ni kosa langu kama Mwenyezi Mungu ameing’oa rehma kutoka moyoni mwako.”

Thursday, 29 October 2015

MAWAHHABI WAMDHALILISHA MTUME KUWA HAKUJIELEWA KUWA YEYE NI MTUME

MAWAHHABI WAMDHALILISHA MTUME KUWA HAKUJIELEWA KUWA YEYE NI MTUME
Waandishi wa kiwahhabi wameeleza suala la mwanzo wa wahyi kwa njia nyingi tofauti zenye kugongana. Tunakusudia kudondoa kilitokea nini kwa Mtume Muhammad (sa.w.w) baada ya kufikiwa na malaika Jibril kwa mara ya kwanza. Hapa tutajaribu kuzitaja chache tu:
a.  Khadija na Abubakr walimpeleka Muhammad (s.a.w.) kwa Waraqa bin Nawfal baada ya kuelezwa Waraqa kuwa Muhammad amepata matatizo, Waraqa akamuuliza Muhammad ana nini? Muhammad (s.a.w.) akamwambia: "Ninasikia ninaitwa nyuma yangu, ewe Muhammad, ewe Muhammad, nikisikia hivyo mimi hukimbia ovyo." Waraqa akamkataza asiwe anakimbia bali akaze roho ili ayasikie anayoambiwa..." Muhammad alishika maelekezo hayo, mara aliposikia akiitwa: Ewe Muhammad! Sema, Bismillahir Rahmanir Rahim, Alhamdulillahi rabbil a'lamina.... mpaka mwisho wa suratul Fatiha. Akaambiwa: Sema: "Laa ilaha illallahu" Muhammad (s.a.w.) baada ya hapo alikwenda kwa Waraqa bin Nawfal, akamjulisha hali hiyo. Waraqa akambashiria habari njema ya kuwa: "Hali kama hiyo alipewa pia Nabii Isa bin Maryam".
Tazama; Albidayatu Wannihaya J. 3 Uk. 9, Assiratun Nabawiyya J. 1 uk 83, Assiratul Halabiyya J. 1 uk 250, Siiratu Mughlataya uk, 15.
b.  Khadija alipompeleka Muhammad (s.a.w.) kwa Waraqa na akamweleza yaliyomtokea. Waraqa alisema: "Huyu ni Nabii wa Umma huu, mwambie atulize moyo."
Tazama: Albidayatu Wannihaya J.3 uk, 12, Siiratu Ibn Hisham J. 1 uk. 238, Assiratul Halabiyya J. 1 Uk. 239.
c.   Khadija alimwambia Muhammad (s.a.w.) atakapokufikia huyo anayekusomesha, uniambie, Mtume (s.a.w.) alipofikiwa na hali hiyo akamjulisha mkewe. Khadija akampakata katika mapaja yake, kisha akavua shungi yake, mara Mtume (s.a.w.) akaona yule aliyemjia anaondoka haraka. Mtume akamjulisha mkewe hilo, Khadija akasema, "Huyo ni Malaika, na wala siyo shetani, basi kaza roho na furahi".
Tazama: Assiratul Halabiyya J. 1 Uk. 252.
d.  Waraqa bin Nawfal alimwambia Khadija: "Muulize Muhammad (s.a.w.), nani anaemjia! Ikiwa ni Malaika Mikaeli basi amemletea amani. Na ikiwa ni Malaika Jibril basi amemletea vita na mateka. Khadija Alipomuuliza Mtume (s.a.w.) akajibu: "Ni Jibril". Khadija akapiga uso wake.
Taz: Tarikhul Yaa'quby J. 2 Uk. 23.
e.  Khadija alipewa kipande cha karatasi na mganga mmoja ili ampe Muhammad (s.a.w.) kama hali hii (iliyomfikia Muhammad) inasababishwa na ugonjwa wa kichaa, basi atapona... Khadija aliporudi kwa mumewe akamkuta anasoma Qur'an, Khadija akamchukua akaenda naye kwa yule mganga, walipofika kwa mganga, akafunua mgongo wa Mtume akaona muhuri wa Utume uko kati ya mabega mawili!!!
Tazama: Tarikhul Khamisi J. 1 Uk. 284, Assiratul Halabiyya J. 1 Uk. 243, Assiratun Nabawiyya J. 1. Uk. 83.
f.    Muhammad (s.a.w.) alipofikiwa na hali hiyo (ya kujiwa na Malaika) alikuwa akipanda katika kilele cha mlima mrefu na akitaka kujitupa chini (ili afe).
Tazama: Almuswannaf J. 5 Uk. 323.
g.  Muhammad (s.a.w.) alirudi kwa mkewe (kutoka katika pango) akiwa nafuraha kubwa akamwambia mkewe: "Nataka kukueleza habari njema, mimi nimeona katika ndoto kuwa Jibril amenijulisha kwamba ametumwa na Mola wangu aje kwangu... Khadija akamwambia: "Furahi, wallahi Mwenyeezi Mungu hatakufanyia lolote ila lililokuwa la kheri... kisha Khadija akaenda kwa mganga wa kinasara, kuuliza uwezekano wa kumuona Jibril. Mganga alishangaa sana kusikia jina la Jibril katika nchi hiyo, kisha akasema kuwa: "Huyo ni Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu..."
Taz: Albidayatu Wannihaya J. 3 Uk. 13.

Nadhani umejionea mwenyewe uzushi wa mawahhabi, masalafi na answari sunnah dhidi ya Mtume wetu. Watu waongo na wazushi kama hawa, hawawezi kuaacha waislamu wa kawaida wakiishi kwa amani mustarehe bila kuleta chokochoko.

Lakini sisi waislamu sahihi, yaani Mashia tunaamini kuwa Mtume alikuwa Mtume bado akiwa tumboni mwa mama yake. Hivyo alipozaliwa tu alijulikana kuwa ni Mtume na miujiza mingi ilifanyika katika utoto wake na ujana wake. Kabla ya kufikisha miaka 40 ambapo utume wake ulizinduliwa rasmi na kuanza kazi ya kuueneza Uislamu duniani.

Monday, 19 October 2015

WAATHIRIKA WA KARBALA – AWN BIN JAAFAR IBN ABI TALIB (R.A)

WAATHIRIKA WA KARBALA – AWN BIN JAAFAR IBN ABI TALIB (R.A)
Aun ni mtoto wa Jaafar ibn Abi Talib (r.a) na Asma’a bint Amees (r.a)..
Alizaliwa ukimbizini Ethiopia (Uhabeshi) kwani baba yake yaani Jaafar alikuwa kiongozi wa wakimbizi wa kiislamu waliokimbilia Habash kutokana na dhuluma na mauaji waliokuwa akifanyiwa na makafiri wa Makkah wakati wa mwanzo wa Uislamu kutangazwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Uislamu ulipota nguvu baba wa Aun yaani Jaafar alirejea uarabuni na kwa kipindi hicho Mtume alikuwa amekwisha hamia Madinah. Miaka michache baadaye Jaafar aliongoza jeshi la waislamu katika mapambano yanayojulikana kama vita vya Mu’tah. Vita hivi vilikuwa vikali sana na waislamu wengi waliuawa ikiwa ni pamoja na kamanda wao, yaani Jaafar bin Abi Talib (r.a). Jaafar aliacha watoto wa kiume watatu yaani Awn, Muhammad na Abdullah.
Vijana hawa walifanana sana na mzee Abu Talib (r.a), hivyo Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Imam Ally waliwapenda sana. Baadaye Imam Ally aliwaozesha mabinti wake. Ummu kulthumu aliolewa na Aun na Zainabu aliolewa na Muhammad. Hapa utagundua kuwa wale wanaosema kuwa Imam Ally waliwaozesha mabinti wake kwa Umar bin Khatab ni uongo na propaganda kwa minajiri ya kuwapotosha watu.
Awn aliendelea kuwa Mtiifu kwa Imam Ally kama imam wake wa kwanza, kisha akawa mtiifu kwa Imam Hassan kama imam wake wa pili na hatimaye akawa mtiifu kwa imam Hussein kama imam wake wa tatu. Awn alichinjwa pamoja na Mashia na Ahlulbayt wengine katika eneo la Karbala, Iraq, akipigana vita upande wa Mashia, yaani katika jeshi dogo la imam Hussein (a.s). Innalillahi wainna ilayhi rajiuun.
Source: Ashura Encyclopedia

By Jawad Muhaddithy 

Monday, 12 October 2015

QURANI MUUJIZA WA MILELE QUR ANI WA MTUME (S.A.W)

QURANI MUUJIZA WA MILELE QUR ANI WA MTUME (S.A.W) 
Qur'ani ni muujiza wa Mtume (s.a.w) ulio hai na wa milele, kwani Qur'ani ndio kitabu pekee kutoka mbinguni ambacho utashi wa Mwenyezi Mungu ulitaka kibakie ni chenye kuhifadhiwa kutokana na mabadiliko, nyongeza, pia upungufu na kugeuzwa- pamoja na kukithiri kwa watu wenye nia na malengo ya kukibadilisha na wafanyao mipango ya kukizua na kukigeuza- ili kitabu hiki kiwe cha milele na katiba ya milele ya maisha hadi siku ya kiama, maadamu kuna mwanadamu anaye ishi juu ya ardhi hii na hilo ni kutokana na hukumu za hali ya juu zilizomo kwenye majalada yake mawili na mafunzo ya kiwango cha juu ambayo kuyatekeleza kwake yana mhakikishia mwanadamu saada na kumpatia maendeleo, kupea na kufikia kwenye daraja za juu mwanadamu huyo.
Hakika Qur'ani pamoja na kuwa ni kitabu cha kielimu, utamaduni hukumu, haki, maadili, adabu, siasa na uchumi, ni muujiza wa mbinguni na wa milele wenye athari kubwa ya kiroho na kimaaanawia ya hali ya juu, hakika kitabu hiki kiliwashinda wanafasaha wakubwa wa kiarabu waliokuwa na nyaraka au waandishi wa nyaraka saba zilizo kuwa zimetundikwa na kuwekwa kwenye kaaba tukufu, na hawakuweza kuleta mfano wa sura moja tu ya Qur'ani, bali kutokana na kushikwa na aibu walikuwa wakizitoa nyaraka walizo tundika juu ya kaaba kati ya zile nyaraka zao, na walifanya hivyo kutokana na kushindwa kwao na kudhalilika kwao, pia kutokana na aibu iliyo washika mbele ya Qur'ani ambayo ni muujiza katika fasaha na balagha yake na katika mfumo wake na utaratibu wake, na lau kama wangeliweza kuleta sura moja tu mfano wa Qur'ani kusinge kuwa na haja ya kutumia mapigano dhidi ya Uislamu na vile vita vibaya na vyenye kuangamiza ambavyo viliishia kuleta maafa kwao na waheshimiwa wao na watu wao na kuvunja utukufu na heshima zao na hadhi zao, pia utawala wao, na kuwavisha vazi la njaa, khofu, udhalili na taabu.
Hii ndio Qur'ani ambayo ni muujiza, na hiki ndio kitabu cha mbinguni cha milele, kitabu ambacho ndani yake kuna mambo yamfikishayo mwanadamu kwenye saada na maisha ya neema na raha, kitabu ambacho hueneza kheri na baraka kwa watu wote, na hutawanya amani na salama katika ardhi hii na katika nchii zote, kumepokelewa riwaya mbali mbali kuhusiana na ubora wa kujifunza kitabu hiki na kukisoma pia kukihifadhi na kutekeleza maamrisho yake, na kufanya matendo kwa mujibu wa maamrisho ya kitabu hicho na zingine nyingi ambazo zinazo muhimiza mwanadamu kukitilia umuhimu.

Sunday, 27 September 2015

SHIA NA QUR’AN TUKUFU

SHIA NA QUR’AN TUKUFU
Shia wanaitakidi kuwa Qur’an ni wahyi wa Mwenyezi Mungu uliteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika ulimi wa Nabii mtukufu kwa kubainisha kila kitu, nayo ni muujiza wa milele ambao wanadamu wameshindwa kupambana nao katika balagha, fasaha na katika ukweli na maarifa ya hali ya juu, haiguswi na mabadiliko, mageuzi wala upotovu, na hii ambayo iko mikononi mwetu tunayoisoma ndio ile ile Qur’an iliyoteremshwa kwa Nabii (s.a.w.w.) na atakaye dai yasiyokuwa hayo basi ni muongo au ni mwenye kukosea au amechanganyikiwa na wote hawako katika uongofu, hakika hayo ni maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo hayapatwi na upotovu kwa hali yeyote.
Sheikhul Muhadithiina Muhammad bin Ali Al-Qummiy ambaye amepewa lakabu ya Asuduuq amesema: Itikadi yetu katika Qur’an ambayo ameiteremsha Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Nabii wake Muhammad (s.a.w.w.) ni ambayo iko baina ya jalada mbili na ambayo iko kwa watu na sio zaidi ya hayo... na anayetunasibishia kuwa tunasema zaidi ya haya basi ni muongo.
Assayid Al-Khuiy ambaye ni mmoja wa marajii wakubwa wa kishia katika zama hizi anasema, “iliyomashuhuri baina ya Waislamu ni kutokuwepo opotoshaji katika Qur’an na iliyopo mikononi mwetu ni Qur’an yote iliyoteremshwa kwa Nabii (s.a.w.w.).
Ama Sheikh Muhammad Al-Ghazaaliy anasema katika kitabu chake Difau anil-aqiydati wa shariah dhidu matwa’inil-mustashiriqiyna “Nimesikia kutoka kwa hawa miongoni mwa watu ambaye anasema katika majilisi za hadhara: Hakika Shia wana Qur’an nyingine ambayo ni zaidi na inapunguza Qur’an yetu iliyo maarufu nikamwambia: Iko wapi hii Qur’an? na kwa nini majini na wanadamu hawakuona nakala yake kwa muda wote huu mrefu? Huu uongo ni wa nini?... kwa nini kusingizia wahyi na watu. Ama hadithi ambazo sio sahihi ambazo baadhi wanaweza kuzitegemea ambazo zinaeleza kupotoshwa kwa Qur’an na ambazo zipo katika vitabu vya hadithi katika Shia, hakika ni dhaifu na hazikubaliwi na mfano wake ni nyingi katika vitabu sahihi vya Ahlus-Sunna na tutaonyesha mifano ya hayo katika Sahih Bukhariy, tunatanguliza hadithi walizozipokea kuhusu kusahau Mtume (s.a.w.w.) katika baadhi ya Aya:-
Kutoka kwa baba yake kutoka kwa Aisha amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu alimsikia mwanaume anasoma sura usiku akasema! Mwenyezi Mungu amrehemu amenikubusha Aya kadha wa kadha nilikuwa nimezisahau katika sura kadha wa kadha. Vile vile katika Sahih Bukhariy ni kwamba, walipokuwa wanakusanya Qur’an hawa kupata sehemu ya Surat Tauba isipokuwa kwa Khuzaimah Al-Answariy na hii inapingana na ukweli unaosema kuwa Qur’an imepokewa kwa Tawatiri na wala sio kwa Riwaya za Ahadi (mtu mmoja):
Al-ahzaab nilikuwa namsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) anaisoma usiku kucha isipokuwa kwa mtu mmoja Khuzaimah Al-Answariy Khuzaima Al-Answariy ambaye Mtume wa Mwenyezi Mungu amejaalia ushahidi wake kuwa ni sawa na ushahidi wa waumini wawili. 
Nilifuatalia kukusanya Qur’an kutoka kwenye vipande vya nguo, mifupa, magome kwa watu waliohifadhi hadi nikakuta Aya mbili za sura ya Tawba kwa Khuzaimah Al-Answariy na sikuipata kwa yeyote asiyekuwa yeye.

Haya ni maelezo ya wazi kuwa Mashia tunaamini kuwa Qur’an tuliyonayo ni kamilifu kama ilivyoshuka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w). Na hadith zinazodai kuwa Qur’an ni pungufu au zaidi ni dhaifu na za uongo na zinapatikana zaidi katika vitabu vya Ahlulsunah waljamaa kuliko katika vitabu vya Shia. Hivyo tusisingiziane imani mbovu ili tu kuzua mtafaruku au kuzuia watu wasijue ukweli. 

UISLAMU UNAPINGA KILA AINA YA UBAGUZI

UISLAMU UNAPINGA KILA AINA YA UBAGUZI
Mtume wetu (s.a.w.w.) amesema: “Waarabu wasijigambe kwamba wao ni bora kwa wasio Waarabu na kinyume chake; na weupe wasijigambe kwa ubora kwa weusi na kinyume chake. Ubora uko tu katika elimu na uchaji.
Katika Qur’ani Tukufu Allah (swt) anasema:
 Enyi watu! Hakika tumekuumbeni ninyi mume na mke; na tumekufanyeni mataifa na makabila ili kwamba mpate kujuana; hakika aliye mbora sana miongoni mwenu mbele ya Allah ni yule amchae Allah zaidi…” (49:13).
Vile vile katika Sura hiyo hiyo ndani ya Qur’ani Anasema:
 Kwa hakika Waumini wote ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu na mcheni Allah ili mrehemiwe.” (49:10).
Kwa hiyo, watu wote, Waasia, Waafrika, Wazungu, Waamerika weupe, weusi, wekundu au manjano, makabila yote ambayo ni Waislamu ni ndugu, na hakuna hata mmoja anayeweza kudai ubora juu ya mwingine.
Kiongozi mkubwa wa Waislamu, Mwisho wa Mitume, alitenda juu ya msingi huu. Alionyesha mapenzi yake makhususi kwa Salman Farsi wa Iran, Suhaib wa Asia ndogo, na Bilal wa Abysinia (Uhabeshi – Ethiopia ya sasa).
Na kwa upande mwingine alimpuuza Abu Lahab (ambaye jina lake lina maana ya Baba wa Miali ya Moto), ami yake mwenyewe ambaye amelaaniwa katika Sura ya Qur’ani Tukufu ambayo inasema:
 Imeangamia mikono miwili ya Abu Lahab! Naye amekwisha angamia…” (111:1).
Ulimwengu umeshuhudia matatizo ya taratibu mbaya mno katika nchi za Maghribi ambayo yalikuwa ni matokeo ya ubaguzi wa rangi. Katika nchi hizo weusi hawaruhusiwi kwenye mahoteli, migahawa, makanisa, na sehemu nyingine za mikusanyiko iliyokusudiwa kwa weupe tu. Uislamu ulipiga marufuku taratibu hizo za kikatili miaka 1400 iliyopita na kutangaza kwamba Waislamu, bila kujali kabila, rangi, au utaifa wote ni ndugu. Hivyo Waarabu wakienda kombo, nitawalaumu, na nitakuwa rafiki wa Mashi’a wawe wa Iran au nchi yoyote duniani.

Kiukweli Uislamu hauruhusu kuwatendea maovu hata watu wasiokuwa waislamu na hivyo kuhimiza kuwafanyia uadilifu watu wasiokuwa Uislamu. 

KIINI CHA MACHAFUKO KATIKA UISLAMU

KIINI CHA MACHAFUKO KATIKA UISLAMU
Mpaka katikati ya karne ya kumi na saba (17) Uislamu ulikuwa na nguvu kubwa za kisiasa duniani. Nguvu hii ilitokana na mwenendo wa Serikali ya Wauthman (Dola ya Wauthmani) ambayo ilikuwa imetawala eneo kubwa la Afrika Kaskazini, Bara Arab, nchi za Ulaya Mashariki kama vile Bulgaria, Hungaria, Yugoslavia, Romania, na hata sehemu za Urusi n.k.
Lakini watawala wa mataifa ya Kikristo, hususan wa Ulaya Magharibi, walipoona Uislamu unazidi kuenea na kupanda mbegu safi ya utamaduni wake, wakaona vibaya kwa kuwa mwenendo wa Kiislamu una nguvu kubwa na ni vigumu kuwafanya watu kubadilika baada ya kuingiwa na silika ya Kiislamu. Kwa haraka kabisa wakaunda vikundi vya wataalamu mbali mbali vikiongozwa na Serikali zao kuzunguka katika mataifa ya Kiislamu kwa nia ya kutafiti njia itakayowasaidia kuondoa mshikamano wa Waislamu. 
Maadui walifanya uchunguzi kwa uyakinifu na wakabainikiwa kuwa nguvu za Waislamu hutokana na umoja wao ambao kwa hakika ndio msingi wa mafanikio ya kila tabaka. Pili, ni kuwa waliona wazi kuwa Waislamu ni wenye kujenga tabia ya kuaminiana wao kwa wao, kwa hali hiyo isingekuwa rahisi kuwaingia na kuwasaliti. 
Hatua ya kwanza ikawa kupenyeza baadhi ya watu wao ndani ya Waislamu na kujifanya Waislamu kusudi wapate imani ya Waislamu. 
Hatua iliyofuatia ilikuwa ni wao kuingia katika vyeo vya Kiislamu na kujifunza elimu humo. Inaripotiwa kuwa Napoleon alifika Misri na kujifunza katika kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Al-Azhar. 
Vikundi vingine vilijihusisha na kutafiti njia za kuingia ukoloni katika maeneo ya Kiislamu na kuziangusha Serikali zake. Waitaliano waliingia Libya na kuanzisha utawala wao huko. Waingereza waliuangusha utawala wa Tippu Sultan mwaka 1799 na kuondolea mbali matumaini ya kisiasa ya Waislamu katika Bara Hindi. Kuanzia hapo Ubeberu wa Kiingereza ulitashahari katika eneo hilo. Katika miaka ya 1894 Waingereza walifanikiwa kuwapata vibaraka ambao walijitolea kuutumikia utawala wao dhidi ya Uislamu. Ghulam Ahmad wa Kadian akaunyenyekea Ukafiri wa Kiingereza kufikia hadi ya kusema baada ya kumwamini Mwenyezi Mungu imani ya pili ni kumwamini Malkia.
Uturuki nako Serikali iliangushwa. Hii ilikuwa baada ya vibaraka kuingia katika ngazi za juu katika Serikali. Adhana ilipigwa marufuku baada ya mapinduzi. Katika utaratibu huu maadui wa Uislamu waliweza kufanikiwa kuuvunja umoja wa Waislamu kwa kuwatumia wanachuoni na watu maarufu katika wenye tamaa. Na huo basi ulikuwa mwanzo wa machafuko. Mpaka hivi sasa, na katika kila nchi zenye Waislamu na ambazo zinatawaliwa na watu wenye nia mbaya na Uislamu, wanawatumia Waislamu wenye mawazo ya kitumwa.
Miongoni mwa watu waliotumiwa kuvunja nguvu za waislamu kwa kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe katika kila kona ya bara Arabu alikuwa Muhammad Abdulwahhabi akishirikiana na mfalme wa Najdi, kazi ambayo wafuasi wake wanaendelea nayo mpaka sasa. Kila eneo lenye Mawahhabi amani imetoweka, anzia Urusi, Pakistan, Afghanistan, India, China, Iran, Iraq, Yemen, Kuwait, Saudi Arabia, Syria, Misri, Libya, Tunisia, Somalia, Lebanon, Jordan, Morocco n.k. kote kuna matukio yametokea ya kuwalipua na kuwashambulia watu wasiokuwa na hatia kwa madai tu ya kutetea madhahebu yao au kupambana na makafiri, cha ajabu utakuta wanaoitwa makafiri ni waislamu wenzao wa kishia na kisunni.

KIINI CHA MACHAFUKO KATIKA UISLAMU

KIINI CHA MACHAFUKO KATIKA UISLAMU
Mpaka katikati ya karne ya kumi na saba (17) Uislamu ulikuwa na nguvu kubwa za kisiasa duniani. Nguvu hii ilitokana na mwenendo wa Serikali ya Wauthman (Dola ya Wauthmani) ambayo ilikuwa imetawala eneo kubwa la Afrika Kaskazini, Bara Arab, nchi za Ulaya Mashariki kama vile Bulgaria, Hungaria, Yugoslavia, Romania, na hata sehemu za Urusi n.k.
Lakini watawala wa mataifa ya Kikristo, hususan wa Ulaya Magharibi, walipoona Uislamu unazidi kuenea na kupanda mbegu safi ya utamaduni wake, wakaona vibaya kwa kuwa mwenendo wa Kiislamu una nguvu  kubwa na ni vigumu kuwafanya watu kubadilika baada ya kuingiwa na silika ya Kiislamu. Kwa haraka  kabisa wakaunda vikundi vya wataalamu mbali mbali vikiongozwa na Serikali zao kuzunguka katika mataifa ya Kiislamu kwa nia ya kutafiti njia itakayowasaidia kuondoa mshikamano wa Waislamu.
Maadui walifanya  uchunguzi kwa uyakinifu na wakabainikiwa kuwa nguvu za Waislamu hutokana na umoja wao ambao kwa hakika ndio msingi wa mafanikio ya kila tabaka. Pili, ni kuwa waliona wazi kuwa Waislamu ni wenye kujenga tabia ya kuaminiana wao kwa wao, kwa hali hiyo isingekuwa rahisi kuwaingia na kuwasaliti.
Hatua ya kwanza ikawa kupenyeza baadhi ya watu wao ndani ya Waislamu na kujifanya Waislamu kusudi wapate imani ya Waislamu.
Hatua iliyofuatia ilikuwa ni wao kuingia katika vyeo vya Kiislamu na kujifunza elimu humo. Inaripotiwa kuwa Napoleon alifika Misri na  kujifunza katika kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Al-Azhar.
Vikundi vingine vilijihusisha na kutafiti  njia za kuingia ukoloni katika maeneo ya Kiislamu na kuziangusha Serikali zake. Waitaliano waliingia  Libya na kuanzisha utawala wao huko. Waingereza waliuangusha utawala wa Tippu Sultan mwaka 1799 na kuondolea mbali matumaini ya kisiasa ya  Waislamu katika Bara Hindi. Kuanzia hapo Ubeberu wa Kiingereza ulitashahari katika eneo hilo. Katika miaka ya 1894 Waingereza walifanikiwa kuwapata  vibaraka ambao walijitolea kuutumikia utawala wao dhidi ya Uislamu. Ghulam Ahmad wa Kadian  akaunyenyekea Ukafiri wa Kiingereza kufikia hadi ya kusema baada ya kumwamini Mwenyezi Mungu  imani ya pili ni kumwamini Malkia.
Uturuki nako Serikali iliangushwa. Hii ilikuwa baada ya vibaraka kuingia katika ngazi za juu katika Serikali. Adhana ilipigwa marufuku baada ya mapinduzi. Katika utaratibu huu maadui wa Uislamu waliweza  kufanikiwa kuuvunja umoja wa Waislamu kwa  kuwatumia wanachuoni na watu maarufu katika  wenye tamaa. Na huo basi ulikuwa mwanzo wa machafuko. Mpaka hivi sasa, na katika kila nchi zenye Waislamu na ambazo zinatawaliwa na watu wenye nia mbaya na Uislamu, wanawatumia Waislamu wenye mawazo ya kitumwa.

Miongoni mwa watu waliotumiwa kuvunja nguvu za waislamu kwa kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe katika kila kona ya bara Arabu alikuwa Muhammad Abdulwahhabi akishirikiana na mfalme wa Najdi, kazi ambayo wafuasi wake wanaendelea nayo mpaka sasa. Kila eneo lenye Mawahhabi amani imetoweka, anzia Urusi, Pakistan, Afghanistan, India, China, Iran, Iraq, Yemen, Kuwait, Saudi Arabia, Syria, Misri, Libya, Tunisia, Somalia, Lebanon, Jordan, Morocco n.k. kote kuna matukio yametokea ya kuwalipua na kuwashambulia watu wasiokuwa na hatia kwa madai tu ya kutetea madhahebu yao au kupambana na makafiri, cha ajabu utakuta wanaoitwa makafiri ni waislamu wenzao wa kishia na kisunni.

Saturday, 26 September 2015

NAMNA NABII IBRAHIM (A.S) ALIVYOFUNDISHA KUHUSU MWENYEZI MUNGU

NAMNA NABII IBRAHIM (A.S) ALIVYOFUNDISHA KUHUSU MWENYEZI MUNGU
Namna Nabii Ibrahiim (AS) alivyoonesha kuwa, nyota, mwezi na jua si miungu. Na hizi ni hoja zetu tulimpa nabii Ibrahiimu juu ya watu wake. Usiku ulipomwingilia akaona nyota. Akasema "hii ni Mola wangu" Ilipotua akasema " Siwapendi miungu wanaopotea" Na siku ya pili alipouona mwezi akasema: "Huu ndiye Mola wangu" Ulipotua akasema "Asiponiongoa Mola wangu, bila shaka nitakuwa miongoni mwa wapotofu. Na siku ya tatu alipoliona jua, akasema Hili jua ndilo Mola wangu. Huyu ni Mola wangu mkubwa, lilipotua akasema Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayoyashirikisha na Mwenyezi Mungu. Mimi nimeuelekeza uso wangu kwa yule aliyeumba mbingu na ardhi, hali ya kuwa nimewacha Dini ya upotevu. (6:74-83).
Namna nabii Ibrahiim (AS) alivyoonesha washirikina kuwa masanamu si miongu. "Wakasema: Je wewe umeifanya hivi miungu yetu, ee Ibrahiim? Akasema: Siyo bali amefanya huyu mkubwa wao, basi waulizeni kama wanaweza kunena! Basi wakajirudi nafsi zao na wakasema Hakika ninyi mlikuwa katika madhalimu" (26:58-64).
Namna Ibrahiimu alivyombwaga mfalme kwa hoja: "Hukumsikia yule aliyehojiana na Ibrahiim juu ya Mola wake kwa sababu Mwenyei Mungu alimpa ufalme? Ibrahiimu akasema "Mola ni yule anayehuisha na kufisha" Yeye akasema "Mimi pia nahuisha na kufisha" Ibrahiimu akasema: "Mwenyezi Mungu hulichomoesha jua mashariki, basi wewe lichomoze magharibi". Akafedheheka yule aliyekufuru na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu"(2:258).

Umuhimu wa kufikiri kwa kujenga hoja: Qur'an kwa nafsi yake inajieleza mara kwa mara kuwa hoja za ujumbe wake ziko wazi kwa watu wanaotumia akili, wenye kuzingatia, wenye kutafakari. "Na hakuna atakayeamini ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, naye hujaalia uchafu uwaendee wale wasiotumia akili zao"(10:100).
Katika aya hizi tunajifunza kuwa Mwenyezi Mungu ni wa milele, hafi hata kwa dakika moja, haonekani kwa macho, yeye ni muweza wa kila kitu. Na kwamba vingine vinauwezo kiasi walivyowezeshwa na Mwenyezi Mungu tu. Hivyo tumwabudu Mwenyezi Mungu muumba na sio miungu ya kubuni na watu wenzetu kama wafanyavyo wakristo wanao dai kuwa Yesu ni mwana wa Mungu na ni Mungu mwenyewe.

SIDDIQ (WAKWELI) NI WATATU TU, KATIKA UISLAMU

SIDDIQ (WAKWELI) NI WATATU TU, KATIKA UISLAMU
Imam Muhammad ibn Ismail al-Bukhari katika kitabu chake Tarikh al-Kabeer, ametaja maneno ya Mtume wetu (s.a.w.w.) yalioelezwa na Ibn Abbas kuwa watu watatu ni “Siddiq”: hakika bila shaka Hizqil  mwamini kati ya watu wa Firauni, Habib al-Najjar mwamini kati ya ukoo wa Yaseen na Ali Ibn Abi Talib ndio wa kweli.
Nawab Siddiq Hasan Khan wa Bhopal katika kitabu chake cha tafsir  kiitwacho Tafsir Fathul Bayan ameeleza hadithi kutokana na Ibn Abi Laila, na hadithi hiyo hiyo imetolewa na Tafsir Durr-e-Manthur  ya Jalaluddin Suyuti lakini iko tafauti ya baadhi ya maneno tu,  wanasema kwamba “Ni watukufu watatu tu ambao hawakukufuru au  kumuasi Mwenyezi Mungu kabisa hata kiasi cha kupepesa macho na  walikimbilia kuamini dini ya haki. Miongoni mwao na wa mwanzo na bora wao ni Ali Ibn Abi Talib; wa pili mwamini katika kaumu ya Firauni, na watatu wao anatokana na ukoo wa Yaseen. Na watatu hawa tu ni Siddiq (Washuhudiawo na kweli).”
Wa kweli au Siddiq hapa inakusudiwa, ni watu wa mwanzo kusilimu katika kaumu yao na tena hawakuwahi kufanya dhambi, bali walipousikia Ukweli wa Uislamu waliupokea mara moja bila kusita na wakaufuata moja kwa moja bila kuchanganya na mila zao zingine.

Nakuombeni tufuate nyendo zao, nasi tuingie katika Uislamu moja kwa moja bila kuchanganya na mila zingine za ajabu ajabu.

Friday, 25 September 2015

IMANI YA KUWEPO KWA MANABII WA MWENYEZI MUNGU

IMANI YA KUWEPO KWA MANABII WA MWENYEZI MUNGU
Inapothibitika kwamba Muumba wetu ni Mwenyeezi Mungu Mtukufu, na ni Muumba Mwenye Hekima, haiwezekani kwa viumbe wake kumuona, kumgusa, kumwenza au kuzungumza Naye, hivyo, ni lazima kwamba Manabii na Mitume Wake wawe ni miongoni mwa viumbe wake, ili kwamba waweze kuwawaidhi waja Wake yale mambo yenye manufaa kwao, na ambayo ni muhimu kwa kuwepo kwao, na ikiwa hatutawafuata, itatuongoza kwenye mauti.
Hivyo, ni lazima Mwenyeezi Mungu kwa ajuaye kuwapelekea viumbe vyake Mitume wake, ambao wanawaamrisha mema na kuwakataza maovu, nao watabaki na kuendelea kuwepo katika dunia hii kutoka Kwake. Wao ni Mitume na Manabii wake miongoni mwa viumbe wake. Wanawafundisha watu hekima, na wanajishirikisha pamoja nao katika mambo yao.
Mwenyeezi Mungu amewapa elimu, hekima, hoja na dalili, kwa mfano, wanawahuisha maiti, wanawaponyesha vilema n.k. Hivyo, dunia haiwezi kuwa tupu bila ya "Hoja"(Imamu) ya Mwenyeezi Mungu, ambaye ana elimu ni shahidi wa maneno na vitendo vya haki vya Mtume, na uadilifu wa Mwenyeezi Mungu.
Tunaamini kwamba dunia haiwezi kuwa tupu bila ya "Hoja" (Maimamu) Zake zinazotoka katika kizazi cha Mitume tu;
Vile vile Mwenyezi Mungu humchagua Mtume Wake miongoni mwa kizazi cha Mitume. Ni hivyo, kwa sababu Mwenyeezi Mungu ameweka njia imulikayo kwa wanaadamu. Ameumba kizazi tohara na kisafi, na miongoni mwao amewachagua Mitume na Manabii Wake ambao ni wateule wa Mwenyeezi Mungu na mfano bora kwa wanaadamu.

Walitoharishwa tangu kwenye manii ya wazazi wao na wakawekwa salama katika mifuko ya uzazi ya mama zao. Uchafu wa ujinga haukuwagusa, wala hawakuchanganyika nao baadaye, kwa sababu Mwenyezi Mungu amewapa daraja tukufu na adhimu kabisa.
Hivyo, yeye ambaye ni hazina ya elimu ya Mwenyeezi Mungu, mdhamini Wake wa yasioonekana, mwenye kujua siri Zake, Hoja Yake kwa viumbe Vyake, kinywa chake na ulimi Wake, lazima awe nazo sifa Zake. Kwa hivyo, Hoja (yaani Imamu) anatoka miongoni mwa vizazi vya Mitume, ili kwamba kwa kuwa nayo elimu ya Mtume aweze kuwa badala ya Mtume, na amrithi kama wasii wake, ili kwamba ikiwa watu watakataa kumkubali, aweze kuwanyamazisha.
Elimu ya Mtume wa mwenyeezi Mungu (s.w.t.) ambayo watu walikuwa nayo, ilidumu (baada ya Mtume Mtukufu) kwa muda mfupi, kwa sababu kwa haraka tofauti kati yao zikatokeza, na wakaanza kutumia maoni na fikara zao wenyewe. Kama wangelimkubali Hoja (Imamu au Khalifa) wakamtii na kumfuata, haki ingesimamiwa na Hoja, tofauti na mabishano yangeondoka, dini ingekuwa imara na salama, na imani ingeshinda shaka.
Baada ya kufariki kwa Mtume wa Mwenyeezi Mungu (s.w.t.), watu hawakuungana kumfuata Hoja huyo, wala kumtii. Kwa hakika, hakuna Mtume au Nabii wa Mwenyeezi Mungu, ambaye umati wake hawakutofautiana baada yake. Sababu ya tofauti zao miongoni mwao ni kwa ajili ya kupinga na kujitenga na Hoja, ambaye amechaguliwa baada ya Mtume wa Mwenyeezi Mungu.

HISTORIA YA MUHAMMAD ABDULWAHABI (2)

HISTORIA YA MUHAMMAD ABDULWAHABI (2)
Muhammad bin Abdul Wahhab alikuwa haraka sana. Alibaleghe kabla hajatimiza miaka kumi na mbili. Wakati huo huo baba yake alimposea mke.  Inasemekana kuwa alihifadhi Qur’an kabla hajafikia  umri wa miaka kumi (10). Alijifunza elimu ya Fiqhi kwa Babake Sheikh Abdul Wahhab bin Sulayman, mwanachuoni mcha Mungu wa madhehebu ya  Hambal. Kadhalika alijifunza elimu za Tafsiri ya  Qur’an na hadithi n.k.
Baadaye alisafiri kwa njia ya biashara na kujifunza  elimu katika miji ya Madina, Basra na Baghdad (Iraq) na akafika Iran kwa madhumuni ya kujifunza  Tasawwuf.
Baba yake pamoja na Masheikh zake walikuwa wakimtabiri kuwa atatokea kuwa mtu  mpotoshaji kutokana na mwenendo wake wa kubishana  nao katika masuala mbali mbali ya kidini, na kwa kuwa alikuwa hana nidhamu wala adabu ya kidini. 
Masheikh zake pamoja na baba yake walikuwa wakiwatahadharisha watu kuwa wasikae pamoja naye wala kusikia maneno yake kwa kuwa yalikuwa ni ya  kupotosha. Kaka yake, Sheikh Sulayman bin Abdul  Wahhab, aliandika kitabu “AL-SAWAA’IQ AL- ILAHIYAH FI AR-RADD ALA AL-WAHHABIYYAH” kupinga mafundisho ya uchafuzi na uzushi ya  mdogo wake.
Kila alipozusha hoja ya upotovu mbele ya Masheikh zake walimfedhehesha. Katika kitabu chao kinachoeleza maisha yake, Mawahhabi wenyewe wanakiri kuwa alikuwa amegombana na kubishana na baba yake na pia kaka yake. Soma katika kitabu “SHEIKH MUHAMMAD ABDUL WAHHAB” uk. 26 na tena katika kitabu “FITNAT-UL-WAHHABIYYAH” uk. 4.
Katika kitabu “MAAL-WAHHABIYYIN” uk. 18, Al-Allamah Jaafar Subhaniy ameandika yafuatayo: “Hakika Muhammad bin Abdul Wahhab hakuwa wa mwanzo katika kuanzisha mwenendo huu. Isipokuwa yeye alichukua fikara zilizotawanywa na Ibn Taimiyya  na mwanafunzi wake Ibn Qayyim na Ibn Abdul Hadi; akajengeka katika mfumo wa maelekezo yao  kutokana na kupitia vitabu vyao mara kwa mara, hivyo akaibuka kuwa kielezeo cha uhakika wa mafunzo yao.

Ibn Taimiyya ni mmoja kati ya wanachuoni wa madhehebu ya Hambal katika karne ya nane. Yeye  alihukumiwa kwenda jela mjini Damascus (Syria) mwaka 728 A.H. kwa ajili ya kuonyesha itikadi na maoni yanayotofautiana na rai ya Waislamu wote”.
WAISLAMU TUMTII NANI PAMOJA NA ALLAH?
Mwenyezi Mungu anasema: "Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na Ulul'amri katika nyinyi" (4:59). Katika Aya hii kuna mambo matatu muhimu: a. Kumtii Mwenyezi Mungu (b) Kumtii Mtume (c) Kuwatii Ulul'amri.
Kumtii Mwenyezi Mungu, maana yake ni kushika amri zake na kuacha makatazo yake. Kama ambavyo; kumtii Mtume (s.a.w.) maana yake ni kufuata uongozi wake.
Katika Aya hii mwenyezi Mungu anaamrisha wa atiiwe Ulul'amri na yeyote ambaye Mwenyezi Mungu anaamrisha atiiwe lazima awe maasum (Mwenye kuhifadhiwa na makosa). Basi, lazima Ulul'amri waliotajwa katika Aya hii wawe Maasum. Naam; kidogo tujikumbushe lile tukio Ia "KISAA" Mwenyezi Mungu aliposema: "Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba (ya Mtume) na (anataka) kukutakaseni sana sana." (33:33)
Hapa tutaangalia Nukta mbili katika Aya hii: (a) AR'RIJSU = Uchafu, matendo mabaya, Haramu, Laana, Kufru, Adhabu. Tazama: Al-Muujamal wasit (kamusi) Kwa mantik hii utaona kuwa: Ahlul Bait, Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na matendo mabaya. Amewaepusha haramu, hawana laana, wanarehema, amewaondolea kufru na adhabu.
(b). At'tuhru: Kutokuwa na uchafu wa aina yoyote. Taz: Al-muujamal wasit (Kamusi) Kwa hiyo; Ahlul Bait (a.s.) hawana uchafu wa aina yo yote. Natija inaonyesha kuwa: Ahlul Bait ni Watakatifu na ni Maasum.
Hawa wanaotiiwa hapa ni Ahlulbayt wa Mtume (saww) ambao Mtume aliwatangaza kuwa ni viongozi baada yake, nao ni Imam Ally (a.s) ambaye ni khalifa wa kwanza, Imam Hassan yaani khalifa wa pili, Imam Hussein yaani Khalifa wa tatu,... na khalifa wa 12 ni Imam Muhammad Mahdi (a.s). hawa ndio urul-amri waliowataja Mwenyezi Mungu katika aya hapo juu kwa tafsiri sahihi itokanayo na Mtume mwenyewe.
Sio kila kiongozi mwislamu anaingia katika kauli hii kwa sababu ziko aya nyingine ambazo Allah ametukataza kuwatii viongozi madhalimu, waovu na watenda dhambi.

MATENDO MATUKUFU KWA MUISLAMU {I}

MATENDO MATUKUFU KWA MUISLAMU {I}

{1}Kuwa na tabia nzuri:-
Mtukufu Mtume {s.a.w.w.} amesema:- "Hakika aliye kamilika imani miongoni mwa walioamini ni yule mwenye tabia nzuri".
{2}Kuwa na elimu:
Mwenyezi Mungu amesema:- "Kwa hakika wanaomwogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wale wataalamu {wanavyuoni}".   {Quran Sura ya 35 aya ya 28}.
Mtukufu Mtume {s.a.w.w} amesema:- "Mwenye kutafuta elimu {mwanafunzi} hupendwa na Mwenyezi Mungu, hupendwa na Malaika, hupendwa na Mitume, na wala hatapenda elimu {ya dini} isipokuwa yule mtu ambae ni mwema."
{3}Ushujaa:
MtukufuMtume {s.a.w.w.} amesema:-"Haimfai mwenye imani awe bahili wala mwoga'". Mwenyezi Mungu anawasifu wenye imani katika Qur'an hivi:

''Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na walio pamoja naye ni wenye nyoyo thabiti {mashujaa} mbele ya makafiri". {Qur'an Sura ya 48, aya ya 29}.

Wednesday, 23 September 2015

KUUMBWA KWA MWANADAMU

KUUMBWA KWA MWANADAMU
 Hatua ya awali ya uumbaji, pale ambapo Adam aliumbwa tunamwachia Allah.
Lakini kwa sasa hatua ya kwanza katika kuumbwa kwa Mwanadamu hurejea kwenye hali wakati Kijusu (Mimba) kinapowekwa kimpango katika tumbo la uzazi, ingawa imefungwa ndani ya aina tatu za sitiri zilizo wazi na aina tatu za viza. Ya kwanza ikiwa ni ile ya ukuta wa nje, ya pili ni ya tumbo la uzazi na ya tatu ni ya Kondo la nyuma. Huu ni wakati ambapo kijusu hakiwezi kujilisha wala kuondoa madhara yoyote yatokanayo nayo.

Mtiririko wa Hedhi umeadilishwa ili kutoa lishe kwa ajili yake, kama vile maji yanavyochukua lishe kupeleka kwenye mimea. Hivyo mpango huu huendelea mpaka kufikia wakati ambao viungo vyake vimekamilishwa, ngozi juu ya mwili wake huwa imara kiasi chakustahimili hali ya hewa - hivyo kwamba haiwezi kupata madhara yoyote kutoka kwenye hewa na macho yake yanapata uwezo wa kustahimili mwanga.
Wakati vyote hivi vinapokuwa vimekwisha fanyika, mama yake hupata uchungu wa uzazi, ambao kwa ukali humtikisa kumfikisha kwenye kuhangaika, kufikia upeo wa kuzaliwa mtoto.
Na kwa kuzaliwa mtoto, mtiririko wa heidhi uliokuwa ukipeleka lishe kwenye tumbo la uzazi unabadilishwa kwenda kwenye matiti ya mama.
Ladha yake inabadilishwa hivyo hivyo na rangi yake, na kuwa lishe aina ya pekee tofauti ambayo hufaa hasa kwa hali ya mtoto, kama na wakati ahitajiayo (hayo) hayo, kulinganishwa na mtiririko wa damu.

Wakati ule ule wa kuzaliwa kwake anaanza kutikisa na kulamba midomo yake kwa ulimi wake kuonyesha hamu yake ya (kunyonya) maziwa hukuta jozi ya matiti ya mama yake matamu mno yaliyohifadhiwa yakining'inia tayari kwa kumpatia lishe kwa ajili yake. Hupata lishe yake kutoka maziwa katika njia hii mpaka wakati huo, kwa vile mwili wake bado ni mororo, viungo vyake na matumbo yake ni laini na dhaifu.

Bila shaka Mwenyezi Mungu aliyeandaa utaratibu huu wa uumbaji anastahili kushukuriwa na kuabudiwa. 

BAHLUL NA WAZIRI WA KHALIFA HARUN RASHID

BAHLUL NA WAZIRI WA KHALIFA HARUN RASHID
Siku moja Waziri mmoja wa Harun alimwambia Bahlul, "Ewe Bahlul, Khalifa amefanya wewe uwe mtawala na Hakimu wa ufalme wa mbwa, kuku na nguruwe wote."

Bahlul alimjibu: "Basi kuanzia hivi sasa, wewe hauna budi kuzitii amri zangu kwani wewe pia upo miongoni mwa raia wangu."

Wote waliokuwa pamoja na Waziri walicheka mno na kulimfanya aondoke kimya kwa kuaibishwa.

FUNZO KUTOKANA NA HABARI HII.
1.  Watawala waache kuwanyanyasa na kuwakejeli wananchi walio chini yao, vinginevyo wananchi watakuwa na haki ya kujitetea na kuwafedhehesha watawala hao.

2.  Kila mtu anahaki zake, na anatakiwa alinde haki zake kwa kila hali. Hakuna sababu ya msingi ya kumfanya mwananchi awe mwoga katika nchi yake mwenyewe. 

Saturday, 19 September 2015

MAPINDUZI YA KIISLAMU NA HUJUMA ZA KIWAHHABI.

MAPINDUZI YA KIISLAMU NA HUJUMA ZA KIWAHHABI.
Asalaam alaykum.
Kwa hakika Mapinduzi ya Kiislam nchini Iran, yalileta mshituko mkubwa katika ghuba, na kuzisononesha tawala zote zilizoko sehemu hiyo na hasa hasa zinazohusiana na mataifa makubwa na kuyategemea kwa kila hali,na kwa upande mwingine madola hayo ya kikoloni yanazitegemea nchi hizo na miongoni mwa tawala hizi ni ule utawala wa Kiwahhabi unaotawala nchi kubwa miongoni mwa nchi za Kiislam, nchi ambayo inasifika kwa utajiri mkubwa wa asili na inanufaika kwa hali maalum ya kijiografia.

Basi ukoloni mbaya na vibaraka wake na watendaji wake wakiongozwa na walinganiaji wa Kiwahhabi wamekusudia kupinga mapinduzi ya Kiislam na kimbunga chake kwa njia mbalimbali, miongoni mwa upinzani huo ni kuzusha wasiwasi ndani yake na kuwasha mioto ya vita dhidi yake na kulazimisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Mapinduzi hayo.

Na njama zote hizi za upinzani dhidi ya mapinduzi ziliposhindwa, wakakusudia kuleta picha mbaya ya utamaduni wa mapinduzi na kuondosha Maf-humu yake na kuuzushia uongo na kuupakazia uzushi ili kuwazuia watu kufuata muongozo wake na kumfuata kiongozi wa mapinduzi hayo.

Kwa hakika njama hii ya kiuadui dhidi ya utamaduni wa mapinduzi ya Kiislam, inabainika ktk mambo yafuatayo:
1) Kueneza matangazo na magazeti aina nyingi katika nchi mbalimbali za ulimwengu ili kuzungumzia dhidi ya mapinduzi na kufanya ushawishi dhidi yake na kuonyesha sura mbaya ya utamaduni wake halisi.
2)Kuchapisha vijitabu na vitabu vingi mno kuhusu utamaduni huo kwa kupitia mikono ya watu na waandishi ambao wameuza nafsi zao na hawajali isipokua mlo wao na pengine vyeo vyao vya kidunia wakiongozwa na yule muongo mkubwa Ih-Sa'an ilahi Dharir (marehemu) ambae ni miongoni mwa watu waliokua wanapata mali nyingi kutoka Saudia.
Mtu huyu alisimama kidete kwa nguvu zake zote na kwa kila kitu ambacho Saudia inakitoa ili kuleta picha mbaya ya taaluma ya mapinduzi miongoni mwa Waislam.
Na huyu bwana alikua maskini kwa kila kitu hata katika madai yake kuwa anayafahamu madh-hebu ya Shia Imamiyyah, basi anachanganya na kuvuruga na wala hapambanui baina ya Asili na na Far-i. Wala baina ya Aqida na Riwaya, na anatoa ushahidi kwa kutumia riwaya kuwa eti ndiyo madh-hebu ya Shia yalivyo.
Yapo mengi zaidi ya hayo katika uongo wake na uzushi wake na natija mbovu alizotoa.
3)Kuyaeneza Madh-hebu ya Kiwahhabi miongoni mwa vijana katika eneo hilo kwa njia mbalimbali huku wakibainisha wazi kuwa Mawahhabi ndio Waislam na kwamba wao ndio wanaompwekesha Mwenyezi Mungu na ndio wanaoitumia Qur'ani na Sunna kwa usahihi, na wasiokua wao ni makafiri!!!
Waandishi wabaya wa aina hii wamepata washabiki wengi hata hapa Afrika ya Mashariki, na washabiki hawa humkufurisha kila mtu mwenye fikra tofauti na zile za uwahhabi.
Tunamwomba Allah atuepushe na ushabiki huu wenye maradha kwa Uislamu.

Allah Mtukufu Ndiye Mjuzi Zaidi

MTUME AAGIZA KUFUATA QUR’AN NA AHLULBAYT

MTUME AAGIZA KUFUATA QUR’AN NA AHLULBAYT
Imepokewa kutoka kwa Sahaba Zaid bin Arqam: Amesema Mtume (s.a.w.):- "Mimi ninakuachieni vizito viwili ambavyo mkishikamana navyo hamtapotea baada yangu, Qur’an na AhIul Bait wangu, viwili hivi havitaachana mpaka vitakaponifikia katika Haudh."
TAZAMA:
Tafsir Ibn Kathir J.4 Uk. 122
Tafsirul Khazin J.1 Uk. 4
Tarikh Bughdad J.8 Uk. 442
Sahihi Muslim J.4 Uk. 1873
Sahihi Tirmidh J.2 Uk. 308
Jamiul Usul J.1 Uk. 187
AIbidayatu Wannihaya J.7 Uk. 362
Majmauz Zawaid J.9 Uk. 163


Hadithi hii inathibitisha kuwa baada ya kuondoka Mtume watakaoshika mahala pake ni Ahlul Bait (a.s.) ambao tumekwisha waona katika tukio Ia "KISAA" na katika tukio la "MUBAHALA"

Mwenyezi Mungu ameamrisha kufuata uongozi wao aliposema: "Shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msitengane". 3:103 Tamko la kamba hapa ni AHLUL BAIT" na hapa tutaonyesha maneno ya Imam Shaafy "Na nilipowaona watu Madhehebu yao yamewapeleka katika bahari yao ya upotovu na ujinga, nikapanda kwa jina Ia Mwenyezi Mungu katika meli yenye kuokoa, nao ni watu wa nyumba ya Mtume mwisho wa Mitume. Na nikaishika kamba ya Mwenyezi Mungu nayo ni kuwatawalisha (Ahlul Bait) kama tulivyoamuriwa kushikamana na kamba, watakapo farakana katika dini makundi sabini na kidogo kama ilivyokuja katika Hadithi. Na asipatikane wa kuokoka miongoni mwao isipokuwa kundi moja, niambieni ni kundi gani hilo enyi wenye akili na maarifa je! Katika makundi yatakayoangamia mojawaponi ni lile kundi la watu wa Muhammad? Au wao ni katika kundi litakalo salimika, niambieni. Ikiwa utasema kundi la Muhammad ni katika kundi litakalookoka, basi huo ni msimamo wa kweli, na ukisema kundi hilo ni katika makundi yatayoangamia bila shaka umepotosha uadilifu, basi niachie Ali awe kiongozi wangu na kizazi chake, na wewe bakia katika mapambo ya ulimwengu."

Imam Shaafy hapa anatukumbusha tamko muhimu Ia Mtukufu Mtume (s.a.w.) aliposema: "Mfano wa Ahlul Bait wangu ni kama mfano wa Meli ya Nuhu, atakayepanda humo ataokoka, na atakayebaki nje atazama".

TAZAMA:
Manaqib Ali Uk. 132
Mustadrakus Sahihain J.2 Uk. 343
Majmauz Zawaid J.9 Uk. 168
Kanzul Ummal J.6 Uk. 216

Hilyatul Awliyaa J.4 Uk. 306