Friday, 25 September 2015

HISTORIA YA MUHAMMAD ABDULWAHABI (2)

HISTORIA YA MUHAMMAD ABDULWAHABI (2)
Muhammad bin Abdul Wahhab alikuwa haraka sana. Alibaleghe kabla hajatimiza miaka kumi na mbili. Wakati huo huo baba yake alimposea mke.  Inasemekana kuwa alihifadhi Qur’an kabla hajafikia  umri wa miaka kumi (10). Alijifunza elimu ya Fiqhi kwa Babake Sheikh Abdul Wahhab bin Sulayman, mwanachuoni mcha Mungu wa madhehebu ya  Hambal. Kadhalika alijifunza elimu za Tafsiri ya  Qur’an na hadithi n.k.
Baadaye alisafiri kwa njia ya biashara na kujifunza  elimu katika miji ya Madina, Basra na Baghdad (Iraq) na akafika Iran kwa madhumuni ya kujifunza  Tasawwuf.
Baba yake pamoja na Masheikh zake walikuwa wakimtabiri kuwa atatokea kuwa mtu  mpotoshaji kutokana na mwenendo wake wa kubishana  nao katika masuala mbali mbali ya kidini, na kwa kuwa alikuwa hana nidhamu wala adabu ya kidini. 
Masheikh zake pamoja na baba yake walikuwa wakiwatahadharisha watu kuwa wasikae pamoja naye wala kusikia maneno yake kwa kuwa yalikuwa ni ya  kupotosha. Kaka yake, Sheikh Sulayman bin Abdul  Wahhab, aliandika kitabu “AL-SAWAA’IQ AL- ILAHIYAH FI AR-RADD ALA AL-WAHHABIYYAH” kupinga mafundisho ya uchafuzi na uzushi ya  mdogo wake.
Kila alipozusha hoja ya upotovu mbele ya Masheikh zake walimfedhehesha. Katika kitabu chao kinachoeleza maisha yake, Mawahhabi wenyewe wanakiri kuwa alikuwa amegombana na kubishana na baba yake na pia kaka yake. Soma katika kitabu “SHEIKH MUHAMMAD ABDUL WAHHAB” uk. 26 na tena katika kitabu “FITNAT-UL-WAHHABIYYAH” uk. 4.
Katika kitabu “MAAL-WAHHABIYYIN” uk. 18, Al-Allamah Jaafar Subhaniy ameandika yafuatayo: “Hakika Muhammad bin Abdul Wahhab hakuwa wa mwanzo katika kuanzisha mwenendo huu. Isipokuwa yeye alichukua fikara zilizotawanywa na Ibn Taimiyya  na mwanafunzi wake Ibn Qayyim na Ibn Abdul Hadi; akajengeka katika mfumo wa maelekezo yao  kutokana na kupitia vitabu vyao mara kwa mara, hivyo akaibuka kuwa kielezeo cha uhakika wa mafunzo yao.

Ibn Taimiyya ni mmoja kati ya wanachuoni wa madhehebu ya Hambal katika karne ya nane. Yeye  alihukumiwa kwenda jela mjini Damascus (Syria) mwaka 728 A.H. kwa ajili ya kuonyesha itikadi na maoni yanayotofautiana na rai ya Waislamu wote”.

No comments:

Post a Comment