Thursday 5 July 2012

IMAM MAHDI KWA MUJIBU WA WANAZUONI WA AHLI SUNNA


BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
Katika sehemu hii ninajaribu kuwaleteeni makala haya juu ya Uthibitisho wa kuwapo kwa Imam Mahdi a.s. kwa mujibu wa Wanazuoni wa Ahli Sunna1 kwa sababu yatasaidia kutoa utata juu ya swala hili la kuwapo kwake kwani wengi wanazua kuwa mambo yote juu ya Imam a.s. yapo yamezuliwa na Mashiah.
(1). HADITH YA KWANZA
"yeyote yule atakayekufa bila ya kumtambua na kumjua Imam wa zama zake basi mtu huyo atakufa mauti ya ujahili (yaani atakufa kifo cha ukafiri)."
Mwana wa khalifa wa pili Abdullah bin Omar alipopata habari kuwa Abdul Malik amekuwa khalifa na hizo habari zilipomfikia akiwa Madina wakati wa usiku, basi aliondoka wakati huo huo na kumwendea mdhalimu huyo Hajjaj nyumbani mwake. Hajjaj alimwuliza sababu ya kufika kwake wakati huo wa usiku na hapo alimwambia kuwa amefika kumtolea bay'a (ahadi ya utiifu) ya baba yake Abdul Malik.

Hajjaj alimwelezea kuwa hakuwa na fursa wakati huo hivyo amwijie kesho yake. Hapo Abdullah bin Omar alisikitika mno na kusema "je nikifa usiku wa leo, basi nitakuwa nimekufa bila ya kufanya bay'a ya imamu wa zama zangu na kwa mujibu wa kauli ya Mtume Mtukufu s.a.w.w., basi nitakuwa nimekufa mauti ya ujahiliyya ambavyo ni ukafiri. Hivyo vyo vyote vile, lazima chukua bay'a yangu."

Hajjaj alimwita ndani (hivyo inamaanisha kuwa mtoto wa khalifa Omar alikuwa bado yupo nje) ya nyumba yake na kumwambia kuwa alikuwa anashughulika na hivyo mikono yake ilikuwa na shughuli hivyo atoe bay'a yake miguuni mwake. Hivyo huyo masikini mtoto wa khalifa Omar aliifanya bay'a miguuni mwa Hajjaj kwa ajili ya utiifu wa Abdul Malik. Baada ya kufanya hivyo, alirejea nyumbani akiwa amefurahi mno.
(Sharh ya Nahjul Balagha - Ibn Abi al-Hadid,j.3,uk.362.Chapa ya Misri)

Jambo la kustaajabisha ni kwamba Abdullah ibn Omar katika zama za ukhalifa wa Amiral Muminiin Imam Ali ibn Abi Talib a.s. hakufanya bay'a na alikaa kimya na baada ya kupita miaka minne na nusu alipitisha kipindi hicho bila ya kumtambua Imam wa zama zake na wala hakuwa na khofu ya kufa mauti ya kafiri! Vyema Hadith hii inatuonyesha waziwazi kuwa katika kila zama kuna ulazima wa kuwapo kwa Imam wa zama hizo. Makala haya yametarjumiwa kutoka itmam-i-Hujjat cha S.S.Akhtar Rizvi katika lugha ya Urdu na yamewahi kuchapishwa katika Sauti ya Bilal no.6 Juzuu XXII Novemba 1988.

Zama zetu hizi pia yupo Imam ambapo inatuwia faradhi kuwa na ilimu na maarifa yake,ama sivyo atakayekufa bila ya kumjua na kufanya bay'a yake atakufa kifo cha kikafiri. Vile vile kuna wataalamu wa kuwapotosha watu kuwa wao wanadai kuwa neno Imam linamaanisha Quran Tukufu. Je watu kama hawa hawawezi kuelewa kuwa Mtume Mtukufu s.a.w.w. hakulitumia neno la Imam peke yake bali alitumia Imamu wa zama ? Yaani kusudi lililopo hapa ni kule kubadilika kwa Imam katika kila zama yaani baada ya Imam mmoja atafuatia Imam wa pili na kuendelea. Jee na Quran imekuwa ikibadilika katika kila zama au jee kuna taarifa yoyote ya kuja kubadilika? Jee baada ya Quran moja itafuatia ya pili na kuendelea? Kwa hakika sisi tusipotoshwe na wazushi kama hao kwa kutumia hila zao.
(2). HADITH YA PILI
Madhehebu yote ya Islam kwa pamoja yanaelezea Hadith ifuatayo na ambayo ni uthibitisho wa ukweli wa Kiislamu na vile vile Sahih Bukhari na vitabu vingine vyote vya Hadith pia vinaelezea kuwa Mtume Mtukufu s.a.w.w. alisema: "Baada yangu watakuwapo Maimamu kumi na wawili ambao watatokana na Maqureish."

Mashiah wanayo fakhari kwa kuwa na Makhalifa kumi na wawili tu kama vile alivyothibitisha Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na vile vile alibashiri majina, idadi na kabila lao pia.
(3). HADITH YA TATU
Allamah Syed Jamal ud-Din Muhaddath ambaye ni mwachuoni mkubwa wa Ahli Sunna, anaandika katika kitabu chake Rawdhat ul-Ahbaab kwa kumnakili Sahaba Ja'abir ibn Abdullahi Ansari wakati Allah swt alimfunulia Aya hii Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.:- "Enyi mlioamini! Mtiini Allah swt na Mtume wake na vile vile mumtiini 'ulil Amr'."

"Basi mimi (anaendelea Bwana Jaabir) niliuliza "Ewe Mtume wa Allah swt! Sisi tunaelewa Allah swt pamoja na Mtume wake. Lakini jee ni wakina nani hao ambao wanajulikana kama 'ulil Amr" ambao utiifu wao umefaradhishwa kwetu sisi?" Hapo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alitoa majibu haya yafuatayo:
"Wao watakuwa Makhalifa baada yangu na wa kwanza miongoni mwao ni Ali ibn Abi Talib na amfuataye atakuwa ni mwanae Hasan na atamfuatia Hussein na baadaye atafuatia Ali ibn al- Hussein na baadaye Mohammad ibn Ali na anatambulika katika Tawrati kwa umashuhuri wa jina la Baqir na ewe Jaabir! Karibu utafikia zama zake na hapo tafadhali naomba unifikishie salamu zangu.

Baada yake atakuja Ja'afer as-Sadiq bin Mohammad na baadaye Musa ibn Ja'afer na baadaye Ali ibn Musa na baadaye Muhammad ibn Ali na baadaye Ali ibn Mohammad na baadaye Hasan ibn Ali na baadaye Muhammad ibn al-Hasan ambaye atakuwa juu ya ardhi hii kama hujjatullah na bakiyallah katika wamchao Allah swt. Huyo ndiye atakayepata ushindi wa mashariki hadi wa magharibi wa dunia hii. Na yeye mwenyewe ambaye atakuwa hayupo mbele ya wafuasi (Mashiah) wake na wale wampendaye hadi kwamba hao hawatabakia katika itikadi ya Uimamu illa wale tu ambao Allah swt ameshawachukulia mitihani ya nyoyo zao." Jaabir r.a. anaelezea kuwa "mimi sikusita kumwuliza Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. "Ewe Mtume wa Allah swt! Je katika zama za Ghaibat, wafuasi (Mashiah) wake wataweza kufaidika naye?"

Hapo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alijibu:
"Naam ! Kwa kiapo cha Allah swt ambaye amenituma nikiwa Mtume wake, kuwa katika zama zake za Ghaibat, Mashiah wake watang'arika kwa nuru yake na kufaidika kwa Ukhalifa wake kama vile watu wanavyofaidika na jua hata kama litakuwa limejificha katika mawingu." Hadith hii tukufu ambayo imenakiliwa na mwanachuoni mashuhuri wa Ahli Sunna kutokea kwa Sahaba Jaabir ibn Abdullahi ansari r.a. ambaye ni mmaarufu na mwenye kuheshimiwa katika Islam.
(4). HADITH YA NNE
Imam Abu Dawud ameandika katika kitabu chake Sunan na Imam Tirmidhi anaandika katika Sahih Tirmidhi kwa kumnakili Abu Said Khudhri, kuwa:
" Mtume Mtukufu s.a.w.w. amesema:
' Mahdi anatokana nami na mwenye uso unaong'aa na pua yake iliyo ndefu ataijaza ardhi kwa uadilifu na haki kama vile itakavyokuwa imeshajaa kwa dhuluma na ufisadi, na atatawala kwa kipindi cha miaka saba.' "
(5). HADITH YA TANO
Imam Abu Dawuud katika Sunan amendika kwa kumnakili Sayyidina Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s :
"Mtume Mtukufu s.a.w.w. amesema kuwa iwapo kwisha kwa dunia hata kama ni siku moja itakayobakia,hivyo pia Allah swt atamtuma mtu mmoja kutokana na Ahlul Bayt yangu (kizazi changu) humu duniani ambaye ataijaza dunia kwa uadilifu na haki kama vile itakavyokuwa imejaa kwa dhuluma na ufisadi."

(6). HADITH YA SABA
Imam Bukhari katika Sahih Bukhari, Imam Muslim katika Sahih Muslim na Kadhi ibn Mas'ud Baghawi katika Tasnif Sharh al-Sunnah. Wote wanamnakili Abu Hurayrah akisema: "Amesema Mtume Mtukufu s.a.w.w. 'Je hali yenu itakuwaje wakati Mtume Issa a.s. atakapoteremka kwenu na Imam wenu atakuwapo ametokea miongoni mwenu?'"

No comments:

Post a Comment