Sunday, 15 July 2012

Kiongozi Muadhamu amteua Sheikh Araki kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Taqriib

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo amemteua Hujjatul Islam Walmuslimin Muhsin Araki kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu. Vilevile amemteuwa Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammad Ali Taskhiri kuwa mshauri wake mkuu katika masuala ya ulimwengu wa Kiislamu.
Matini ya barua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya kumteuwa Sheikh Araki ni hii ifuatayo:
Janabi Hujjatul Islam Walmuslimin Sheikh Muhsin Araki, Mwenyezi Mungu adumishe taufiki yake kwako.
Kwa sasa ambapo Hujjatul Islam Walmuslimin Sheikh Muhammad Ali Taskhiri amejiuzulu nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya kukurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu baada ya kuhudumu kwa kipindi cha muongo mmoja na kwa kutilia maanani pendekezo la Baraza Kuu la jumuiya hiyo, ninakuteua kuwa Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu kutokana na uzoefu na tajiriba yako ya elimu na amali.
Katika kipindi cha sasa ambapo mwamko wa Kiislamu na mabadiliko ya kustaajabisha yanayofuatia mwamko huo yameuweka ulimwengu wa Kiislamu katika mojawapo ya vipindi muhimu sana katika historia, umoja wa umma wa Kiislamu na suala la kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu ni nguzo muhimu ya kupatikana na kulindwa ushindi wa harakati hiyo.
Katika upande mwingine maadui wa Uislamu na vinara wa kufru na unafiki wakiongozwa na Marekani na Israel wanafanya mikakati ya kubadili jihadi na mapambano na kuvifanya harakati za kuwakufurisha Waislamu na kuua watoto wa dini hiyo tukufu, au kwa maneno mengine kuanzisha vita vya Shia na Suni katika ulimwengu wa Kiislamu kwa shabaha ya kuyashughulisha mataifa ya Waislamu na ugonvi wa wao kwa wao huku wakidhani kwamba wanaweza kudhibiti uwezo wote wa kimaada na kimaanawi wa ulimwengu wa Kiislamu kupitia njia hiyo.
Inatarajiwa kuwa katika kipindi muhimu cha sasa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu itaufanya udiplomasia wa umoja wa Kiislamu kuwa stratijia yake kwa kutumia uzoefu wenye thamani wa miaka iliyopita na ubunifu wa masuala yanayohitajika katika zama hizi ikishirikiana na wasomi wa Ulimwengu wa Kiislamu hususan wanafikra wa vyuo vya kidini na vyuo vikuu. Vilevile ni matarajio kuwa jumuiya hiyo itaweka misingi ya kuanzishwa umma mmoja wa Kiislamu mkabala wa kambi ya ubeberu.
Namuomba Mwenyezi Mungu SW akupe taufiki wewe na wafanyakazi wenzako.
Sayyid Ali Khamenei
20 Tir 1391
Wakati huo huo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemshukuru Hujjatul Islam Walmuslimin Sheikh Muhammad Ali Taskhiri kwa huduma zake kubwa za mwongo mmoja katika Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu na amemteuwa kuwa mshauri wake mkuu katika masuala ya ulimwengu wa Kiislamu.

No comments:

Post a Comment