Saturday, 7 July 2012
Mchakato wa katiba waendelea Tanzania, Wazanzibari wataka mamlaka kamili
Huku tume ya kutafuta maoni kuhusu katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba ikiwa imeanza kazi zake rasmi kwa kutuma wajumbe wake katika baadhi ya mikoa na Tanzania Bara na Zanzibar, baadhi ya Wazanzibari waliotoa maoni yao wamesisitizia haja ya Zanzibar kuwa na mamlaka kamili ya kujiamulia mambo yake na kushirikiana na Tanganyika kimkataba katika baadhi ya mambo.
Kwa upande wa Zanzibar, wajumbe wa tume hiyo wameanza kukusanya maoni yao katika mkoa wa Kusini Unguja kwenye viwanja vya Mtende Makunduchi ambapo baadhi ya watu waliopata fursa ya kutoa maoni yao wamependekeza kurejeshwa kwanza serikali za Tanganyika na Zanzibar na halafu kuungana katika baadhi ya masuala kimkataba.
Wametoa mfano wa kuzuiwa Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kwa sababu ya Muungano na pia kushindwa Zanzibar kuwa mwanachama wa Shirikisho la Soka la Dunia (Fifa) kwa sababu hizo hizo za Muungano, na kutaka ipewe mamlaka kamili ya kujiamulia mambo yake.
Katika upande mwingine, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar, Haji Omar Kheri amesema kwamba, kukosekana kwa uzalendo na tamaa ya kipato kikubwa ni moja ya sababu ya baadhi ya wananchi wataalamu kuacha kazi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kukimbilia ughaibuni.
Amesema hayo wakati alipokuwa anajibu swali katika Baraza la Wawakilishi, kutoka kwa Mwakilishi wa Jimbo la Wawi (CUF) Saleh Nassor Juma aliyetaka kujua sababu za wataalamu wa Zanzibar kukwepa kufanya kazi visiwani humo na badala yake kukimbilia ughaibuni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment