Wapenzi wa Imam Khomeini
(MA) kutoka kila kona ya Iran wameshiriki katika kumbukumbu za mwaka wa
ishirini na tano wa kufariki dunia muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu,
zilizofanyika katika eneo alipozikwa mwanachuoni huyo mkubwa, na kuonyesha
taswira isiyo na kifani ya hamasa, kusimama kidete, heshima na mapenzi yao kwa
malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu na wakati huo huo kutangaza kwa mara
nyingine tena utiifu wao kwa mwanachuoni huyo aliyetangulia mbele ya Haki.
Ayatullahil Udhma Sayyid
Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehudhuria hadhara
hiyo kubwa iliyojaa nuru na kuhutubia hadhirina. Katika hotuba yake,
amezungumzia asili na sababu ya kuongezeka kila leo hamu na mapenzi ya mataifa
ya walimwengu ya kuusoma na kuzidi kuuelewa mfumo wenye nguvu kubwa na unaozidi
kuimarika wa Jamhuri ya Kiislamu ambao umeiundwa juu ya msingi wa sheria za
Kiislamu na demokrasia iliyotokana na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.
Amesema sheria za Kiislamu na demokrasia ni vitu viwili vikuu vilivyomo kwenye
chuo na aidiolojia ya Imam Khomeini (MA). Vile vile amesisitiza
kuwa, wananchi na viongozi wa Iran wameshikamana vilivyo na nakala hiyo mpya ya
kisiasa – kiraia na kuongeza kuwa: Usumbufu na njama za kila namna zinazofanywa
na Marekani na kupungua kasi ymoyo wa kuelekea kwenye mwamko wa Imam Khomeini
(MA) ni changamoto mbili kuu ambazo iwapo taifa la Iran litazitambua na
kuzishinda, litaweza kuendeleza vizuri njia iliyojaa fakhari na ufanisi ya Imam
(MA).
Katika sehemu ya kwanza ya
hotuba yake mbele ya hadhara hiyo adhimu ya kitaifa, Ayatullahil Udhma Khamenei amelitaja
suala la kuzidi kuvutiwa walimwengu na hasa wa mataifa ya Waislamu na Imam
Khomeini na Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni uhakika muhimu sana na kuongeza kuwa:
Hivi sasa na baada ya kupita miaka 25 tangu afariki dunia Imam Khomeini (MA)
matabaka mbali mbali ya watu hasa vijana na watu muhimu katika ulimwengu wa
Kiislamu wamezidi kuwa na hamu na shauku ya kuitambua zaidi aidiolojia ya
demokrasia ya kidini, nadharia ya Fakihi Mtawala (Wilayatul Faqih) na masuala
mengine yanayohusiana na Mapinduzi ya Kiislamu.
Ameyataja mashambulizi
yasiyosita na makubwa mno wa kisiasa na kipropaganda ya maadui wa Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran kuwa ni moja ya sababu zilizoongeza hamu ya mataifa ya
walimwengu kutaka kuyajua zaidi Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kwamba: Fikra
za walio wengi katika ulimwengu wa Kiislamu; hivi sasa na kuliko wakati
mwingine wowote, zimekuwa na hamu kubwa zaidi ya kuujua wasifu na uhalisia wa
mfumo wa kiutawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao unashambuliwa kwa
mashambulizi makubwa kiasi chote hiki kutoka kila kona ya dunia na zina hamu na
kuelewa siri ya taifa la Iran ya kuweza kusimama kidete na kupata mafanikio
makubwa katika misimamo yake licha ya kukumbwa na dhoruba zote hizo za
mashambulizi ya kila upande ya maadui.
Aidha ameutaja uwezo, nguvu
na maendeleo yanayoongezeka kila leo ya taifa la Iran kuwa ni sababu nyingine
inayoyafanya mataifa ya dunia yawe na shauku ya kuijua zaidi Jamhuri ya
Kiislamu na mfumo wa demokrasia ya kidini unaotawala nchini Iran.
Ayatullah Khamenei ameutaja
mwamko wa Kiislamu na hisia za kupinga uistikbari na ubeberu kuwa ni moja ya
matunda ya shauku na hamu ya mataifa hasa ya Kiislamu ya kuyatambua zaidi
Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kwamba: Kambi ya kibeberu, inaendelea
kufanya makosa ya kiistrajitia kwa kudhani kuwa imeweza kung’oa mizizi ya
mwamko wa Kiislamu kwani mtu anapoangalia kwa kina na kuelewa mambo
yaliyopelekea kutokea mwamko wa Kiislamu atatambua vyema kuwa mwako huo si kitu
kinachoweza kuondoka, na kwamba mwamko huo utachomoza tena na tena na kupanuka
kwa nguvu za hali ya juu zaidi.
Amesema, kizazi cha vijana
katika ulimwengu wa Kiislamu kinatafuta majibu ya maswali muhimu ya kihistoria
kwamba kwa nini na kivipi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kusimama imara
katika kipindi chote hiki cha miaka 35 licha ya kushambuliwa kutoka kila upande
kiuadui, kijeshi, kisiasa na kipropaganda pamoja na kuwekewa mashinikizo na
vikwazo vikubwa mno na Marekani ambavyo havijawahi kushuhudiwa mfano wake na
wakati huo huo taifa la Iran kila leo likawa linazidi kupiga hatua za
kimaendeleo na kuwa imara tena bila ya kuwa taifa la kihafidhina.
Kiongozi wa Mapinduzi ya
Kiislamu ameendelea kutoa ufafanuzi kuhusu sababu zinazoifanya Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran kuwa na mvuto wa aina yake akisema: Mataifa ya dunia na kizazi
cha vijana na tabaka la watu wenye ushawishi katika ulimwengu wa Kiislamu
wanayaona maendeleo mbali mbali ya taifa la Iran katika nyuga za anga na anga
za mbali, wanaona namna Iran ilivyo katika orodha ya nchi kumi za dunia zilizo
na maendeleo makubwa sana ya kielimu, wanaona jinsi kasi ya maendeleo ya
kielimu ilivyo mara 13 zaidi nchini Iran ikilinganishwa na wastani wa kasi hiyo
duniani na wanatambua kuwa taifa la Iran ni nambari moja katika siasa za eneo
la Mashariki ya Kati na limesimama imara katika kupambana na utawala ghasibu wa
Kizayuni na kuyahami na kuyatetea mataifa yanayodhulumiwa.
Ayatullahil Udhma Khamenei
ameongeza kuwa: Mambo hayo humfanya kila mtu awe na shauku na hamu ya kutaka
kuijua zaidi na zaidi Jamhuri ya Kiislamu.
Vile vile amekutaja
kufanyika uchaguzi wa 32 katika kipindi cha miaka 35 iliyopita tena kwa
kujitokeza kwa wingi wa kupigiwa mfano wananchi wa Iran katika uchaguzi huo, na
kujitokeza kwa hamasa kubwa na kwa wingi mno wananchi wa Iran katika maandamano
ya Bahman 22 (Februari 11, zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya
Kiislamu) na katika maandamano ya Siku ya Quds (Ijumaa ya mwisho ya mwezi
Mtukufu wa Ramadhani) kuwa ni uhakika mwingine unaozifanya fikra za walimwengu
zivutiwe na Iran.
Ameongeza kuwa: Sisi
tumezoea kushuhudia mambo hayo na hatuuoni uadhama na umuhimu wake machoni
mwetu, lakini uhakika huo wenye mvuto unawafanya watu walioko nje na wa nchi
nyinginezo kujiuliza maswali mengi na kustaajabishwa sana na mambo hayo…
Kiongozi Muadhamu ameongeza
kuwa, matukio na uhakika huu wote wa kuvutia umetokana na fikra za kipekee za
mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaani Imam Khomeini (MA) na ameendelea na
hotuba yake kwa kutoa taswira fupi lakini iliyobeba vitu vingi ya chuo na
aidiliojia ya Imam Khomeini (MA).
Nukta kuu iliyokuwemo
kwenye sehemu hiyo ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni
uhakika huu kwamba kwa ajili ya kufikia kwenye lengo, inabidi tusipoteze njia
ya lengo hilo na kwa ajili ya kupiga hatua katika njia sahihi pia tunamuhitajia
mwasisi huyo (Imam Khomeini – MA) mwenye fikra za busara na anayeangalia mbali.
Ayatullah Khamenei
amekutaja kujenga mfumo wa kiraia – kisiasa juu ya msingi mantiki ya Kiislamu
ndiyo shabaha kuu ya Imam Khomeini na kuongeza kuwa: Kuporomoka utawala
kibaraka, fasidi na wa kidikteta wa Shah na kung’oa mizizi ya utawala huo
ulikuwa ni utangulizi wa ujenzi wa jengo adhimu ambalo Imam alilipigania kwa
hima yake kubwa na kwa kushirikiana na wananchi wa Iran.
Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu nguzo na misingi mikuu ya
mfumo wa kisiasa wa wananchi uliokusudiwa na Imam Khomeini (MA) kwa kugusia
nukta mbili kuu za kimsingi ambazo zimeshikamana kikamilifu akisisitiza kuwa: Kwanza
kabisa ni sheria za Kiislamu ambazo ndiyo roho na msingi mkuu wa Jamhuri ya
Kiislamu na pili ni kuwakabidhi wananchi kazi za kuendesha nchi kupitia mfumo
wa kidemokrasia.
Ameongeza kuwa: Hakuna mtu
aliyefikiria kwamba Imam Khomeini (MA) angeliweza kuchukua uchaguzi kutoka
katika utamaduni wa Magharibi na kuuchanganya na fikra ya Kiislamu kwani ni
jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba, kama uchaguzi na demokrasia
isingelikuwa inawezekana kuichukua ndani ya sheria za Kiislamu, basi Imam wetu
aliyekuwa muwazi na mwenye misimamo isiyotetereka, angelilitangaza wazi suala
hilo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya
Kiislamu amesisitiza kuwa: Kwa mujibu wa chuo na aidiolojia ya Imam Khomeini,
sheria za Kiislamu ambazo ndio uhalisia na asili ya mfumo wa Kiislamu zinapaswa
zizingatiwe kikamilifu katika masuala yote, katika utungaji sheria, katika
utungaji wa sera katika kuteua na kuondoa viongozi, katika miamala ya kawaida
ya watu na kwenye masuala mengineyo yote, na wakati huo huo mchakato wa kazi
katika mfumo huo wa kisiasa na kiraia ufanyike kwa mujibu wa demokrasia
inayozingatia sheria za Kiislamu; na wananchi nao imma kwa njia ya moja kwa
moja au isiyo ya moja kwa moja waweze kuchagua viongozi wa nchi yao.
Kiongozi Muadhamu amekutaja
kutekelezwa kikamilifu sheria za Kiislamu kuwa kutapelekea kudhaminiwa misingi
minne mikuu ambayo ni kujitegemea, uhuru, uadilifu na umaanawi.
Ameongeza kuwa: Kushikamana
na sheria zilizojaa ufanisi za Kiislamu, mbali na kuleta uhuru wa watu binafsi
na wa kijamii, unalikomboa pia taifa kutoka katika minyororo ya mabeberu yaani
unaliletea taifa uhuru wa kitaifa na vile uadilifu unaoambatana na umaanawi na
kuchunga mafundisho ya Mwenyezi Mungu.
Baada ya hapo Ayatullahil
Udhma Khamenei amebainisha nukta nyingine ya kimsingi ya Imam Khomeini (MA) akisema:
Katika chuo na aidiolojia ya Imam, nguvu na ushindi wowote unaopatikana kwa
njia za mabavu na kutumia silaha haukubaliki, tab’an nguvu na uwezo unaotokana
na chaguo la wananchi unakubalika na unaheshimiwa na mtu yoyote hapaswi kupinga
maamuzi hayo ya wananchi na kama mtu atafanya hivyo basi ajue kuwa hiyo ni
fitna.
Ayatullah Khamenei ameitaja
nakala ya kisiasa - kiraia ya Imam Khomeini (MA) kuwa ni ukurasa mpya katika
sarufi ya kisiasa duniani na katika kubainisha vipengee vingine vya nakala hiyo
mpya amesema: Kuwasaidia watu wanaodhulumiwa na kupambana na dhulma ni miongoni
mwa vipengee vikuu vya chuo na aidiolojia hiyo ya Imam.
Amefafanua zaidi kwa
kuashiria uungaji mkono kamili na ambao haukusita hata mara moja wa Imam
Khomeini (MA) kwa taifa madhulumu la Palestina na kuongeza kuwa: Kusimama
kidete katika kupambana na dhulma na kuvunja wazi wazi haiba ya madhalimu ni
msingi mkuu katika aidiolojia ya Imam Khomeini (MA) jambo ambalo inabidi
viongozi na wananchi wote wa Iran walizingatie sana wakati wote.
Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja ufanikishaji wa kivitendo vya vipengee vya
nakala ya kisiasa – kiraia ya Imam kuwa ni moja ya tofauti kubwa na zawazi
zilizopo baina ya aidiolojia hiyo ya Imam na aidiolojia nyingine zinazoishia
kwenye maneno tu na hapo hapo akauliza swali hili la kimsingi akisema: Je, kazi
kubwa iliyofanywa na Imam kwa mafanikio makubwa, itaendelea?
Amejibu swali hilo kwa
kusema ndio, lakini kwa masharti.
Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwa kusema: Katika jedwali jamali na lenye
mvuto la Imam, kwa kawaida na mara zote kunakuwa na vyumba vilivyo wazi ambavyo
upo uwezekano wa kuvijanaza na kuendelea na njia hii muhimu mno lakini kwa
sharti la kufanya hima na kuwa na welewa wa kitaifa na kuchunga njia nzuri za
kuvijaza vyuma hivyo.
Ayatullahil Udhma Khamenei
amesifu uaminifu na utiifu wa taifa la Iran kwa malengo matukufu ya Imam
Khomeini (MA) akisisitiza kuwa: Mwenendo uliooneshwa na taifa la Iran katika
kipindi chote hiki cha miaka 25 ya tangu kufariki dunia Imam mtukukfu unaonesha
kuwa vyomba vyote vitupu na vilivyo wazi katika jedwali hilo vitaweza kujazwa
na kwamba chini ya kivuli cha kuendeleza njia ya Imam, Iran azizi kwa taufiki
ya Mwenyezi Mungu itafikia kwenye vilele vya juu kabisa vya nguvu na uwezo.
Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kuwakhutubu hadhirina na
mataifa yote akiyasisitizia nukta moja ya kimsingi kwa kusema: Kuendelea na
njia ya Imam Khomeini (MA) na kufanikisha malengo matukufu ya mwanachuoni huyo,
ni mfano wa kila lengo jingine muhimu, lazima kutakuwa na vizuizi na changamoto
za kila namna ndani yake, na kama vizuizi na changamoto hizo hatutazitambua na
kuziondoa, basi kuendelea na njia hiyo kutakuwa kugumu au hata kutakuwa
hakuwezekani.
Hapo hapo Ayatullahil Udhma
Khamenei ametaja changamoto mbili za nje na ndani na kusema kuwa ndizo
changamoto kuu ambazo inabidi vijana, watu wenye ushawishi na vipaji, watoa
nadharia na wasomi na wanafikra wa Iran wazizingatie na kuzipa uzito wa hali ya
juu.
Ametoa ufafanuzi kuhusiana
na changamoto za nje kwa kugusia usumbufu, kero na ukwamishaji unaofanywa na
uistikbari wa kimataifa na hasa hasa Marekani na kuongeza kuwa: Tab’an baadhi
ya wanafikra wa kisiasa wa Magharibi wanasema wazi kuwa, usumbufu na kero hizo
hazina faida yoyote lakini pamoja na hayo Marekani bado inaendelea kutekeleza
njama zake hizo kuu.
Ayatullah Khamenei
ameongeza kuwa: Wamarekani wamezigawanya nchi za dunia na mirengo ya kisiasa na
shaksia mbali mbali ulimwenguni katika mafungu matatu, kundi la nchi zinazotii
amri, kundi la tawala na mirengo ambayo hivi sasa inakwenda nayo pole pole na
tawala na mirengo isiyokubali kuburuzwa.
Ameongeza kuwa: Marekani
inaziunga mkono kikamilifu na kwa kila namna tawala na nchi ambazo zinatii amri
zake na ambazo zimejisalimisha kwake na haishughulishwi na uovu unaofanywa na
tawala hizo katika jamii ya kimataifa, tab’an kupitia uungaji mkono wake huu wa
kila upande, Marekani inajali tu maslahi yake na kuzibebesha tawala hizo
ufanikishaji wa maslahi yake hayo.
Kiongozi Muadhamu amegusia
baadhi ya mifumo ya tawala za kiimla na za kidikteta kupindukia zinazoungwa
mkono na Marekani akisema kuwa: Kuhusiana na nchi hizo ambazo ndani yake hakuna
uchaguzi hata mmoja unaofanyika na wala wananchi wake hawana nguvu za kusema hata
neno moja, Marekani inakwepa kuziita nchi hizo kuwa ni za kiimla na kidikteta
na badala yake inaziita kuwa ni nchi zinazotawaliwa na mfumo dume (kwa sababu
zinatii amri za Marekani).
Kiongozi wa Mapinduzi ya
Kiislamu amelitaja kundi la pili la nchi zilizomo kwenye mgao wa Marekani kuwa
ni nchi ambazo kutokana na kuwa na maslahi ya pamoja na Marekani, Washington
imeamua kwenda nazo pole pole lakini wakati wowote inapopata fursa haichelei
kushindilia jambia lake kwenye moyo wa nchi hizo.
Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja nchi za Ulaya kuwa ni mfano wa wazi wa nchi
hizo na kusisitiza kwamba: Tab’an licha ya kwamba Marekani inakwenda pole pole
na nchi hizo za Ulaya kwa kulinda maslahi yake, lakini wakati huo huo inafanyia
ujasusi maisha binafsi ya wananchi wa Ulaya na hata viongozi wa nchi hizo na
inafanya hivyo kijeuri kiasi kwamba haiko tayari hata kuomba radhi.
Ameongeza kuwa: Tab’an nchi
za Ulaya zimefanya kosa kubwa la kihistoria kwa kukubali kwao kutumikia manufaa
na maslahi ya Marekani jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa na maslahi ya
mataifa yao.
Ayatullahil Udhma Khamenei
amelitaja kundi la tatu la nchi za dunia kwa mujibu wa mgao huo wa Marekani
kuwa ni lile la nchi ambazo hazikubali kuburuzwa na ubeberu wa Marekani.
Amesisitiza kuwa: Siasa za
Marekani kuhusiana na nchi hizo ni kutumia bila mipaka wala kikomo uwezo wake
wote kuhakikisha kuwa inatoa pigo kwa nchi hizo na inazisambaratisha.
Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu njia zinazotumiwa na
Washington dhidi ya nchi ambazo hazikubali kuburuzwa na Marekani akisema:
Tab’an hivi sasa uvamizi wa kijeshi si kitu kinachopewa kipaumbele na Marekani
kutokana na dola hilo la kibeberu kupata hasara kubwa katika uvamizi wake wa
kijeshi kwenye nchi za Iraq na Afghanistan.
Ameongeza kuwa, stratijia
nyingine kubwa inayotumiwa na viongozi wa Washington kuhusiana na nchi
zinazoendesha mapambano na zisizokubali kuburuzwa na Marekani ni kutumia
vibaraka wake katika nchi hizo na kuongeza kuwa: Kufanya njama za mapinduzi ya
kijeshi au kuwashawishi wananchi wamiminike barabarani kupinga tawala za nchi
hizo ni miongoni mwa mbinu kubwa zinazotumiwa na Marekani kupitia vibaraka
wake.
Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Serikali yoyote ile katika nchi yoyote
ile inayoingia madarakani kwa kura za wananchi, lazima watakuweko watu wachache
ambao hawakuipa kura zao serikali hiyo na ambao ni wapinzani wa serikali hiyo.
Sasa Marekani inatumia suala hilo kuwachochea wapinzani hao kuwaingiza baadhi
ya watu mitaani kupinga serikali hiyo.
Ameongeza kuwa: Mifano ya
siasa hizo za Marekani zinaonekana kwa uwazi katika baadhi ya nchi za Ulaya.
Tab’an sisi hatuhukumu chochote katika suala hilo lakini tunajiuliza, wale
maseneta wa Marekani wanaoonekana kwenye maandamano ya mitaani katika nchi hizo
za Ulaya wanafanya nini kwenye maandamano hayo yasiyowahusu?
Kiongozi wa Mapinduzi ya
Kiislamu amekutaja kuanzisha na kuyatia nguvu makundi ya kigaidi kuwa ni mbinu
nyingine inayotumiwa na Marekani kukabiliana na nchi hizo zisizotii amri zake
na ambazo hazikubali kuburuzwa na dola hilo la kibeberu.
Amesema: Iraq, Afghanistan
na baadhi ya nchi za Kiarabu pamoja na Iran yetu azizi ni wahanga wakuu wa
mbinu hiyo ya Marekani dhidi ya nchi hizo.
Ayatullah Khamenei
ameashiria pia uungaji mkono wa Marekani kwa kijigenge cha kigaidi cha wanafiki
(MKO) na namna wanachama wa kigenge hicho cha kigaidi walivyo na uhusiano wa
moja kwa moja na taasisi za utawala wa Marekani likiwemo Baraza la Congress la
nchi hiyo na kuongeza kuwa: genge la kigaidi la wanafiki (MKO) ambalo limewaua
kigaidi maulamaa, wasomi, na shakhsia wakubwa wa kisiasa na kiutamaduni pamoja
na wananchi wengi wa Iran, linafanya vitendo vyake vya kigaidi chini ya uungaji
mkono kamili wa Marekani.
Kiongozi Muadhamu amezitaja
mbinu nyingine zinazotumiwa na Marekani dhidi ya nchi huru duniani ambazo
hazikubali kuburuzwa kuwa ni kuzusha mizozo na mifarakano kati ya viongozi wa
juu wa tawala za nchi hizo na kuzusha upotofu katika imani na itikadi za kidini
za watu wa nchi hizo.
Ameongeza kuwa: Kwa taufiki
na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, Wamarekani wameshindwa katika njama zao zote
hizo mbele ya taifa la Iran na kwamba njama zao zote likiwemo jaribio la
mapinduzi ya kijeshi, kuunga mkono wafanya fitna na wachocheaji wake, njama za
kuwamimina barabarani baadhi ya wananchi na kuzusha ufa na hitilafu kati ya
viongozi zote zimeshindwa kutokana na imani na mwamko wa taifa la Iran.
Baada ya kumaliza
kubainisha changamoto za nje, Ayatullahil Udhma Khamenei ameanza kuzungumzia
changamoto za ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisema: Changamoto
hizo na hatari kubwa itatokea wakati taifa na viongozi wa Iran watakapouweka
mbali na kuusahau moyo na misimamo ya mwamko wa Imam mtukufu.
Kuhusiana na suala hilo
Ayatullah Khamenei ameashiria kufanyika makosa katika kumjua rafiki na adui na
kushindwa kumtambua adui wa asili na adui asiye wa asili na kuongeza kuwa: Watu
wote wanapaswa kuzingatia kuwa, hawapaswi kughafilika na adui mkuu na wa asili
katika matukio yote.
Kiongozi Muadhamu ametoa
mfano mmoja wa wazi wa kushindwa kumtambua adui wa kweli na asiye wa kweli
kwamba ni vitendo viovu na vya aibu vya makundi yasiyojua kitu na ya kijahili
ya Kitakfiri, Kiwahabi na Kisalafi dhidi ya Ushia na kusisitiza kuwa: Watu wote
wanapaswa kuzingatia kuwa, adui mkuu ni mashirika ya kijasusi ya mabeberu na
watu ambao wanayachochea makundi hayo kwa kuyapa fedha na silaha.
Ameongeza kuwa: Tab’an kila
mtu atakayefikiria kuichokoza Jamhuri ya Kiislamu kwa hakika atapata pigo na
majibu makali sana kutoka kwa taifa la Iran, lakini pamoja na hayo sisi
tunaamini kuwa, mkono wa adui ambao haukujificha sana na ambao unawachochea
Waislamu kuuana wao kwa wao ndiye adui yetu mkuu na wa asili na si haya makundi
yaliyodanganywa yakadanyika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi
ya Kiislamu amekutaja kupoteza mshikamano wa kitaifa, kukumbwa na uvivu na
kutokuwa na mori wa kufanya kazi, kufanya kazi chache, kutawaliwa na uvunjikaji
moyo na kukata tamaa na vile vile kuwa na fikra ghalati na potofu ya kudhani
hatuwezi au kwamba huko nyuma pia hatukuweza, kuwa ni vipengee vingine vya
changamoto za ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Kama
ambavyo Imam wetu azizi alisema, sisi tunaweza na kwamba azma na nia ya kweli
ya kitaifa pamoja na uongozi na usimamiaji wa mambo kijihadi utaweza kuondoa
mikwamo yote na kutatua matatizo yote ya usoni.
Mwishoni mwa miongozo yake,
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba: Jina lenye baraka la Imam
mtukufu na mipango ya mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa uwezo wa Mwenyezi
Mungu italisaidia taifa la Iran katika hatua zote na kuiletea Iran azizi
mustakbali unaong’ara kupitia kuleta matumaini, hamasa, mori na uchangamfu
katika masuala yote.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi
Muadhamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Hasan Khomeini, amewakaribisha
wafanya ziara na wapenzi wa mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu na kuzitaja jitihada
za kuwaondolea shida watu na maeneo yaliyoko nyuma kimaendeleo, kuwasaidia
wanyonge na kung’oa mizizi ya umaskini kwamba ndiyo yaliyokuwa malengo na
shabaha kuu za Imam Khomeini (MA) na kuongeza kwamba: Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei pia siku zote
amekuwa akiyapa umuhimu na sisitizo la kipekee malengo na shabaha hizo za Imam,
na hilo ni somo kwa watu wote.
Mfawidhi wa Haram Tukufu ya
Imam Khomeini (MA) vile vile ameutaja utatuzi wa matatizo ya kiuchumi kuwa
unahitajia tadibiri, mantiki, ushirikiano mkubwa kati ya Mihimili Mitatu Mikuu
ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) na umoja na mshikamano wa kitaifa.
Ameongeza kuwa: Uchumi
inabidi ufungamane kikamilifu na utamaduni wa kupambana na umaskini na kubaki
nyuma kimaendeleo.