Ama katika amri za kimaumbile mhusika mkuu ni
Allah (s.w), kwani amri za kimaumbile na zile sifa na nyenendo maalumu za kimaumbile
zenye msukumo wa kimaumbile usiohitajia hiyari, bali inawezekana kukawepo
baadhi ya nyenendo za kimaumbile ambazo mwanaadamu anaweza kuzizuia na
kuzipeleka katika njia nyingine kwa kiasi fulani, huku Mitume wakionekana kuwa
na nguvu za moja kwa moja katika kuzisarifu zile nyenendo zote za kimaumbile
kwa idhini ya Mola Mtakatifu.
1. Kwa hiyo, dini ni kitu ambacho uhakika wake
tayari uko wazi na ni wenye kutambulika, uhakika ambao umekusanya ndani yake
mfumo mzima wa maisha ya mwanaadamu kijumla jumla, na sio kwa ajili ya kikundi
au watu maalumu.
Sio jambo lenye kukubalika kuwa dini ni
fikra maalumu za watu, wawe wanasiasa au wana elimu mbali mbali, kwa hiyo ni
Mwenyeezi Mungu tu anayeweza kutengeneza dini, na dini tayari imeshatengenezwa
kwa mujibu wa maisha na mahitajio ya wanaadamu, ni jambo lilsiloingilika
akilini kuwa watu waende kutafuta dini, kwa sababu dini iko tayari, na ni
wadhifa wa kila mwanaadamu kufuata dini na sio kutengeneza, mfumo wa haki wa
dini ni wa Allah (s.w) na sio watu wengine. Natija tunayoipata kutokana na
maelezo hayo ni kuwa :-
*Dini ni mjengeko uliopangwa kwa nidhamu maalumu
katika kipindi chote cha historia, kuanzia wakati alipoumbwa mwanaadamu hadi
zama hizi tunazokwenda nazo, dini imetumwa kwa watu kwa ajili ya kuwapa uwezo
wa kufahamu mambo mbali mbali yanayohusiana na maisha yao, na mambo mengine
yote, dini ambazo zimekuja kwa mujibu wa fikra au mifumo ya wanaadamu hizo sio
dini za Mwenyeezi Mungu na dini hizo zitakuwa ni nakisi na zenye upungufu, kwa
hiyo dini hizo sio sahihi.
Ikiwa patatokea – mbali na Mitume na Ahlulbayt-
mtu atakayekuja na madai au ujumbe wa kudai kuwa ujumbe huo amepewa na
Mwenyeezi Mungu, au ana uhusiano fulani na Mwenyeezi Mungu basi mtu huyo hana
dini, na hana mfumo wowote unaonasibiana na mfumo wa dini aliyoileta Mwenyeezi
Mungu (s.w).
Dini ni mfumo na mjengeko uliopangwa kwa nidhamu
maalumu, kwa ajili ya watu wote duniani katika kipindi chote cha historia ya
binaadamu, Mwenyeezi Mungu ameitengeneza dini na kuwapelekea waja wake
kulingana na mahitajio yao ya kila siku, kuanzia zama za Nabii Adam (a.s) hadi
zama atakazodhuhuru kiongozi muokozi wa Waislamu, hadharati Mahdi Ajjala llahu
Taala Sharifu.
Dini ni mfumo maalumu wa elimu, hukumu, na
taaluma mbali mbali za kitabu kitukufu cha Wahyi wa Mwenyeezi Mungu (Qur-an) ,
ndani ya kitabu hicho kuna mabainisho mbali mbali ya mambo yaliyopita, mambo
yaliyopo, yajayo na mambo yatakayokuja, ndani ya kitabu hicho mna kila kitu
anachokihitajia mwanaadamu na viumbe wote kwa ujumla cha dhahiri na cha batini.
Natuangalie Aya hii tukufu ya Mwenyeezi Mungu iliyonukuliwa na mmoja wa Maimamu
maasumu (a.s) Yeye kuhusiana na dini anasema hivi:-
Funguo za kila elimu ziko kwake Yeye Mola
Mtakatifu, na anayathibitisha hayo kupitia kauli yake Allah (s.w)
Yeye (s.w) anasema:-
" وَعِندَهُ مَفَاتِحُ
الْغَيْبِ لاَ يَعْلَمُهَا إِلاَّ هُوَ وَيَعْلَمُ مَا فِى الْبَرِّ وَالْبَحْرِ
وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلاَّ يَعْلَمُهَا وَلاَ حَبَّةٍ فِى ظُلُمَاتِ
الاَرْضِ وَلاَ رَطْبٍ وَلاَ يَابِسٍ إِلاَّ فِى كِتَابٍ مُّبِينٍ[3]".
Na ziko kwake funguo za
ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye anajua kilioko nchi kavu na
baharini. Na halidondoki jani ila analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo
katika Kitabu kinachobainisha.
Maana na ufafanuzi wa Aya hiyo ni kama ifuatavyo:-
Vitu vyote duniani vilivyo na uhai na visivyo na
uhai vimedhibitiwa ndani ya Qur-an na viko katika milki yake Yeye Allah (s.w),
yaani rikodi ya kila kitu iko kwa Allah (s.w).
Kuwepo kwa Qur-ani kwa ajili ya dini ya Kiislamu,
na pasitokee na mtu yeyote atakayeweza kukiharibu au kukiharifu kitabu hicho,
yote hayo yanathibitisha uwezo wake Allah (s.w) katika kuihifadhi dini na
kitabu chake kitukufu. Ikiwa patatokea mtu awezae kuipunguza au kuizidisha
herufi angalau moja ya Qur-an (na hakuna
anayeweza wala atakayeweza kufanya hivyo) basi kitabu hicho hakitakuwa kitabu
cha Wahyi wa Mwenyeezi Mungu, wala hakitakuwa kitabu cha dini.
Ufafanuzi wa paragrafu hiyo ni kwamba:-
Mwenyeezi Mungu amekiteremsha kitabu cha Qur’an
kikiwa ni nyenzo ya kumuongoza mwanaadamu katika saada kwa kufanya yale
aliyoamrishwa na Mola wake kupitia kitabu hicho, na kwa muongozo wa Mitume ya
Mwenyeezi Mungu na Ahlulbayt (a.s), kwa hiyo kama tukisema kuwa kitabu hicho
kina upungufu au kimezidishwa baadhi ya mambo ambayo Mwenyeezi Mungu hakuyatia
mambo hayo katika kitabu hicho, itamfanya mwanaadamu awe na udhuru wa
kumshitakia Mola wake kuwa yale aliyomtaka ayafanye yalizidishwa au kupunguzwa
katika kitabu hicho ambacho kilikuwa ndio muongozo wake.
Tunaweza kuufafanua ufumbuzi wa dini katika njia
mbili zifuatazo:-
1. kwa kuifanyia uhakiki nafsi ya mwanaadamu
mwenyewe.
2. Katika ulimwengu wa MIYTHAAQ (میثاق).
Ulimwengu wa Miythaaq unarejea katika kile
kipindi ambacho Mwenyeezi Mungu alimuumba mwanaadamu. Pale Allah (s.w)
alipowauliza waja wake,
وَإِذْ اَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِى آدَمَ مِن
ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَاَشْهَدَهُمْ عَلـٰي اَنفُسِهِمْ اَلَسْتَ بِرَبِّكُمْ قَالُواْ بَلَي شَهِدْنَا اَن تَقُولُواْ
يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَذَا غَافِلِينَ[4]
Na pale Mola wako Mlezi alipo waleta katika
wanaadamu kutoka migongoni mwao kizazi chao, na akawashuhudisha juu ya nafsi
zao, akawaambia: Je, Mimi si Mola Mlezi wenu? Wakasema: Kwani! Tumeshuhudia.
Msije mkasema Siku ya Kiyama sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo.
Maelezo kuhusiana na Aya:-
Mradi wa Aya hii ni kuwa; Mwenyeezi Mungu
amemtia kila Binaadamu ujuzi wa kujitambua kuwa yeye ameumbwa, na yuko
aliyemuumba, na huyo ndiye Mwenyeezi Mungu. Basi hana hoja ya kusema kuwa
alipotezwa na wazee wake wala nani. Sio hoja hiyo kwani kila mmoja amepewa
akili na utambuzi, kwa nini anajifuatia tu.
No comments:
Post a Comment