Friday, 13 June 2014

NDOA YA MUHAMMAD MUSTAFA NA KHADIJA

Khadija, binti ya Khuwaylid, alikuwa mkazi wa Makka. Naye pia alikuwa wa kabila la Quraishi. Aliheshimiwa sana na watu wa Makka kwa sababu ya tabia yake ya mfano na uwezo wake kifedha. Kama vile watu wa Makka walivyomuita Muhammad 'Sadiq' na 'Amin', walimuita Khadija 'Tahira', yenye maana ya "Aliye safi." Alikuwa akijulikana pia miongoni mwa Waarabu kama 'Malkia wa Wafanya biashara.' Wakati wote misafara ilipoondoka Makka au kurudi Makka, waliona kwamba mzigo wake ulikuwa mkubwa kwa ujazo kuliko mizigo yote ya wafanyabiashara wa Makka ikichanganywa pamoja.
Muhammad alipokuwa na umri wa miaka 25, ami yake na mlezi wake, Abu Talib, alimshauri Khadija, na kuelewa kwake kwa kimya, kwamba amchague yeye kama wakala wake katika mmoja wa misafara yake, uliokuwa uondoke kwenda Syria punde tu, mara.
Khadija kwa kweli alikuwa akihitaji wakala kwa wakati ule hasa. Alikubali kumchagua Muhammad kama wakala wake. Alichukua madaraka ya bidhaa za Khadija, na msafara ukatoka kwenda Syria. Mtumwa wa Khadija, Maisara, pia alifuatana naye na akamsaidia kama msaidizi wake.
Safari hii ya kibiashara kwenda Syria ilifanikiwa kupita matarajio, na Khadija alivutiwa sana na uwezo wa wakala wake na uaminifu wake kiasi kwamba aliamua kumpa madaraka ya shughuli zote za biashara zijazo baadaye. Safari hii pia ilithibitisha kuwa mwanzo wa ndoa yao.
Makubaliano ya ndoa, katika mfumo rahisi wa kizamani, yanaonyesha kupendana kwa Muhammad na Khadija; yanamuelezea yeye Muhammad kama mtu hodari zaidi wa kabila la Quraish; na anatamka mahari ya wakia kumi na mbili za dhahabu na ngamia ishirini, ambayo ilitolewa kwa ufadhili wa ami yake, Abu Talib.
Abu Talib alisoma khutba ya ndoa ya Muhammad na Khadija, na hotuba yake au waadhi unathibitisha bila shaka yoyote kwamba alikuwa akiabudu Mungu mmoja.
Alianza hotuba yake katika mfumo wa "Kiislam" kwa kutoa sifa na shukrani kwa Allah (s.w.t.) kwa rehma zake na baraka zisizoidadi na neema, na alimalizia kwa kumuomba Rehma na neema Zake juu ya maharusi wapya hao.
Ndoa ya Muhammad na Khadija ilifanikiwa sana. Imebarikiwa na furaha kuu isiyo na kifani kwa wote, mume na mke. Khadija alijitolea maisha yake kwenye huduma kwa mumewe na Uislamu. Alitumia utajiri wake mkubwa wote kwa kuimarisha Uislamu, na katika ustawi wa Waislamu.
Khadija alikuwa na hisia za ujumbe kama zile zile alizokuwa nazo Muhammad, na alikuwa na shauku kama aliyokuwa nayo ya kuona Uislamu unaushinda upagani. Kwa shauku yake ya kuuona ushindi wa Uislamu, aliongeza uwajibikaji na uwezo. Alimuondoa mumewe katika ulazima wa kutafuta maisha, na hivyo kumuwezesha kutoa muda wake wote katika ulazima wa kutafuta kujiandaa kwa kazi kubwa iliyokuwa imelala mbele yake.
Huu ndio mchango wa maana sana alioutoa kwenye kazi ya mumewe kama Mtume wa Mungu. Alikuwa ndio egemeo ambalo Muhammad alilihitaji katika miaka yote ya maandalizi kwa ajili ya Utume.

Ndoa ya Muhammad na Khadija ilibarikiwa pia na kuzaliwa kwa binti yao, Fatima Zahra. Ingawa neema ambazo Mungu amewajaalia juu yao zilikuwa nyingi, hapakuwa na yoyote waliyoithamini zaidi ya binti yao, Fatima Zahra. Alikuwa ni mboni ya macho ya baba yake, na "Bibi wa Peponi" wa baadaye. Baba na Mama walitoa kwa wingi mno mapenzi yao juu yake, na alileta matumaini ndani ya nyumba yao.

No comments:

Post a Comment