Saturday 14 June 2014

MUISLAMU ANATAKIWA KUWA NA TABIA NJEMA.

Mtume Mohammad ametambulishwa katika Qur’ani kama ifuatavyo:
“Na hakika una tabia njema kabisa.” (68:4)

Mtume wetu ametajwa na Qur’an kuwa ni mtu mwenye tabia njema kabisa. Ni sunnah na lazima kwa kila muislamu kuwa na tabia njema na huruma kwa wanadamu wote kama alivyokuwa kiongozi na muombezi wa umma huu. Kuna aya nyingine ambao Allah anasema kuwa kama Mtume angekuwa ni mjeuri basi watu wangemkimbia. Sijui hawa watu wanaodhani kuwa Uislamu ni ubabe wamezisoma kweli aya hizi au wanacho kitabu kingine wanachokifuata tofauti na Qur’an?
Mwaka jana katika mahafali ya chuo kikuu cha SUA alisimama mhadhiri mmoja wa kiwahhabi na kutangaza hadharani kuwa muislamu lazima awe mbabe na kwamba anapokutana na kafiri katika njia nyembamba ni haramu kumpisha kafiri katika njia na kwamba kilicho sunnah na kumsukuma akupishe wewe Muislamu ndio upite njiani na yeye apite porini. Nilisikitika sana na sikubaliani na Uislamu bandia wa namna hii.

Kama hivyo wanavyodai waislamu hawa wa bandia itakuwa na maana gani ayah hii ambayo inasema:
 “Waite watu katika njia ya Mola wako kwa hikima na mauidha mema, na ujadiliane nao kwa nama iliyo bora…” (16:125)

Je inawezekana kufanya tabligh kwa ubabe na mauaji kama wanavyofanya Mawahhabi na magaidi wengine? 

No comments:

Post a Comment