Friday 13 June 2014

Sheria za Kiislamu na demokrasia ndiyo misingi miwili mikuu katika aidiolojia ya Imam Khomeini

Wapenzi wa Imam Khomeini (MA) kutoka kila kona ya Iran wameshiriki katika kumbukumbu za mwaka wa ishirini na tano wa kufariki dunia muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, zilizofanyika katika eneo alipozikwa mwanachuoni huyo mkubwa, na kuonyesha taswira isiyo na kifani ya hamasa, kusimama kidete, heshima na mapenzi yao kwa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu na wakati huo huo kutangaza kwa mara nyingine tena utiifu wao kwa mwanachuoni huyo aliyetangulia mbele ya Haki.
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehudhuria hadhara hiyo kubwa iliyojaa nuru na kuhutubia hadhirina. Katika hotuba yake, amezungumzia asili na sababu ya kuongezeka kila leo hamu na mapenzi ya mataifa ya walimwengu ya kuusoma na kuzidi kuuelewa mfumo wenye nguvu kubwa na unaozidi kuimarika wa Jamhuri ya Kiislamu ambao umeiundwa juu ya msingi wa sheria za Kiislamu na demokrasia iliyotokana na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Amesema sheria za Kiislamu na demokrasia ni vitu viwili vikuu vilivyomo kwenye chuo na aidiolojia ya Imam Khomeini (MA).  Vile vile amesisitiza kuwa, wananchi na viongozi wa Iran wameshikamana vilivyo na nakala hiyo mpya ya kisiasa – kiraia na kuongeza kuwa: Usumbufu na njama za kila namna zinazofanywa na Marekani na kupungua kasi ymoyo wa kuelekea kwenye mwamko wa Imam Khomeini (MA) ni changamoto mbili kuu ambazo iwapo taifa la Iran litazitambua na kuzishinda, litaweza kuendeleza vizuri njia iliyojaa fakhari na ufanisi ya Imam (MA).
Katika sehemu ya kwanza ya hotuba yake mbele ya hadhara hiyo adhimu ya kitaifa, Ayatullahil Udhma Khamenei  amelitaja suala la kuzidi kuvutiwa walimwengu na hasa wa mataifa ya Waislamu na Imam Khomeini na Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni uhakika muhimu sana na kuongeza kuwa: Hivi sasa na baada ya kupita miaka 25 tangu afariki dunia Imam Khomeini (MA) matabaka mbali mbali ya watu hasa vijana na watu muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu wamezidi kuwa na hamu na shauku ya kuitambua zaidi aidiolojia ya demokrasia ya kidini, nadharia ya Fakihi Mtawala (Wilayatul Faqih) na masuala mengine yanayohusiana na Mapinduzi ya Kiislamu.
Ameyataja mashambulizi yasiyosita na makubwa mno wa kisiasa na kipropaganda ya maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni moja ya sababu zilizoongeza hamu ya mataifa ya walimwengu kutaka kuyajua zaidi Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kwamba: Fikra za walio wengi katika ulimwengu wa Kiislamu; hivi sasa na kuliko wakati mwingine wowote, zimekuwa na hamu kubwa zaidi ya kuujua wasifu na uhalisia wa mfumo wa kiutawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao unashambuliwa kwa mashambulizi makubwa kiasi chote hiki kutoka kila kona ya dunia na zina hamu na kuelewa siri ya taifa la Iran ya kuweza kusimama kidete na kupata mafanikio makubwa katika misimamo yake licha ya kukumbwa na dhoruba zote hizo za mashambulizi ya kila upande ya maadui.
Aidha ameutaja uwezo, nguvu na maendeleo yanayoongezeka kila leo ya taifa la Iran kuwa ni sababu nyingine inayoyafanya mataifa ya dunia yawe na shauku ya kuijua zaidi Jamhuri ya Kiislamu na mfumo wa demokrasia ya kidini unaotawala nchini Iran.
Ayatullah Khamenei ameutaja mwamko wa Kiislamu na hisia za kupinga uistikbari na ubeberu kuwa ni moja ya matunda ya shauku na hamu ya mataifa hasa ya Kiislamu ya kuyatambua zaidi Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kwamba: Kambi ya kibeberu, inaendelea kufanya makosa ya kiistrajitia kwa kudhani kuwa imeweza kung’oa mizizi ya mwamko wa Kiislamu kwani mtu anapoangalia kwa kina na kuelewa mambo yaliyopelekea kutokea mwamko wa Kiislamu atatambua vyema kuwa mwako huo si kitu kinachoweza kuondoka, na kwamba mwamko huo utachomoza tena na tena na kupanuka kwa nguvu za hali ya juu zaidi.
Amesema, kizazi cha vijana katika ulimwengu wa Kiislamu kinatafuta majibu ya maswali muhimu ya kihistoria kwamba kwa nini na kivipi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kusimama imara katika kipindi chote hiki cha miaka 35 licha ya kushambuliwa kutoka kila upande kiuadui, kijeshi, kisiasa na kipropaganda pamoja na kuwekewa mashinikizo na vikwazo vikubwa mno na Marekani ambavyo havijawahi kushuhudiwa mfano wake na wakati huo huo taifa la Iran kila leo likawa linazidi kupiga hatua za kimaendeleo na kuwa imara tena bila ya kuwa taifa la kihafidhina.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kutoa ufafanuzi kuhusu sababu zinazoifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa na mvuto wa aina yake akisema: Mataifa ya dunia na kizazi cha vijana na tabaka la watu wenye ushawishi katika ulimwengu wa Kiislamu wanayaona maendeleo mbali mbali ya taifa la Iran katika nyuga za anga na anga za mbali, wanaona namna Iran ilivyo katika orodha ya nchi kumi za dunia zilizo na maendeleo makubwa sana ya kielimu, wanaona jinsi kasi ya maendeleo ya kielimu ilivyo mara 13 zaidi nchini Iran ikilinganishwa na wastani wa kasi hiyo duniani na wanatambua kuwa taifa la Iran ni nambari moja katika siasa za eneo la Mashariki ya Kati na limesimama imara katika kupambana na utawala ghasibu wa Kizayuni na kuyahami na kuyatetea mataifa yanayodhulumiwa.
Ayatullahil Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Mambo hayo humfanya kila mtu awe na shauku na hamu ya kutaka kuijua zaidi na zaidi Jamhuri ya Kiislamu.
Vile vile amekutaja kufanyika uchaguzi wa 32 katika kipindi cha miaka 35 iliyopita tena kwa kujitokeza kwa wingi wa kupigiwa mfano wananchi wa Iran katika uchaguzi huo, na kujitokeza kwa hamasa kubwa na kwa wingi mno wananchi wa Iran katika maandamano ya Bahman 22 (Februari 11, zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu) na katika maandamano ya Siku ya Quds (Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani) kuwa ni uhakika mwingine unaozifanya fikra za walimwengu zivutiwe na Iran.
Ameongeza kuwa: Sisi tumezoea kushuhudia mambo hayo na hatuuoni uadhama na umuhimu wake machoni mwetu, lakini uhakika huo wenye mvuto unawafanya watu walioko nje na wa nchi nyinginezo kujiuliza maswali mengi na kustaajabishwa sana na mambo hayo…
Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, matukio na uhakika huu wote wa kuvutia umetokana na fikra za kipekee za mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaani Imam Khomeini (MA) na ameendelea na hotuba yake kwa kutoa taswira fupi lakini iliyobeba vitu vingi ya chuo na aidiliojia ya Imam Khomeini (MA).
Nukta kuu iliyokuwemo kwenye sehemu hiyo ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni uhakika huu kwamba kwa ajili ya kufikia kwenye lengo, inabidi tusipoteze njia ya lengo hilo na kwa ajili ya kupiga hatua katika njia sahihi pia tunamuhitajia mwasisi huyo (Imam Khomeini – MA) mwenye fikra za busara na anayeangalia mbali.
Ayatullah Khamenei amekutaja kujenga mfumo wa kiraia – kisiasa juu ya msingi mantiki ya Kiislamu ndiyo shabaha kuu ya Imam Khomeini na kuongeza kuwa: Kuporomoka utawala kibaraka, fasidi na wa kidikteta wa Shah na kung’oa mizizi ya utawala huo ulikuwa ni utangulizi wa ujenzi wa jengo adhimu ambalo Imam alilipigania kwa hima yake kubwa na kwa kushirikiana na wananchi wa Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu nguzo na misingi mikuu ya mfumo wa kisiasa wa wananchi uliokusudiwa na Imam Khomeini (MA) kwa kugusia nukta mbili kuu za kimsingi ambazo zimeshikamana kikamilifu akisisitiza kuwa: Kwanza kabisa ni sheria za Kiislamu ambazo ndiyo roho na msingi mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu na pili ni kuwakabidhi wananchi kazi za kuendesha nchi kupitia mfumo wa kidemokrasia.
Ameongeza kuwa: Hakuna mtu aliyefikiria kwamba Imam Khomeini (MA) angeliweza kuchukua uchaguzi kutoka katika utamaduni wa Magharibi na kuuchanganya na fikra ya Kiislamu kwani ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba, kama uchaguzi na demokrasia isingelikuwa inawezekana kuichukua ndani ya sheria za Kiislamu, basi Imam wetu aliyekuwa muwazi na mwenye misimamo isiyotetereka, angelilitangaza wazi suala hilo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kwa mujibu wa chuo na aidiolojia ya Imam Khomeini, sheria za Kiislamu ambazo ndio uhalisia na asili ya mfumo wa Kiislamu zinapaswa zizingatiwe kikamilifu katika masuala yote, katika utungaji sheria, katika utungaji wa sera katika kuteua na kuondoa viongozi, katika miamala ya kawaida ya watu na kwenye masuala mengineyo yote, na wakati huo huo mchakato wa kazi katika mfumo huo wa kisiasa na kiraia ufanyike kwa mujibu wa demokrasia inayozingatia sheria za Kiislamu; na wananchi nao imma kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja waweze kuchagua viongozi wa nchi yao.
Kiongozi Muadhamu amekutaja kutekelezwa kikamilifu sheria za Kiislamu kuwa kutapelekea kudhaminiwa misingi minne mikuu ambayo ni kujitegemea, uhuru, uadilifu na umaanawi.
Ameongeza kuwa: Kushikamana na sheria zilizojaa ufanisi za Kiislamu, mbali na kuleta uhuru wa watu binafsi na wa kijamii, unalikomboa pia taifa kutoka katika minyororo ya mabeberu yaani unaliletea taifa uhuru wa kitaifa na vile uadilifu unaoambatana na umaanawi na kuchunga mafundisho ya Mwenyezi Mungu.
Baada ya hapo Ayatullahil Udhma Khamenei amebainisha nukta nyingine ya kimsingi ya Imam Khomeini (MA) akisema: Katika chuo na aidiolojia ya Imam, nguvu na ushindi wowote unaopatikana kwa njia za mabavu na kutumia silaha haukubaliki, tab’an nguvu na uwezo unaotokana na chaguo la wananchi unakubalika na unaheshimiwa na mtu yoyote hapaswi kupinga maamuzi hayo ya wananchi na kama mtu atafanya hivyo basi ajue kuwa hiyo ni fitna.
Ayatullah Khamenei ameitaja nakala ya kisiasa - kiraia ya Imam Khomeini (MA) kuwa ni ukurasa mpya katika sarufi ya kisiasa duniani na katika kubainisha vipengee vingine vya nakala hiyo mpya amesema: Kuwasaidia watu wanaodhulumiwa na kupambana na dhulma ni miongoni mwa vipengee vikuu vya chuo na aidiolojia hiyo ya Imam.
Amefafanua zaidi kwa kuashiria uungaji mkono kamili na ambao haukusita hata mara moja wa Imam Khomeini (MA) kwa taifa madhulumu la Palestina na kuongeza kuwa: Kusimama kidete katika kupambana na dhulma na kuvunja wazi wazi haiba ya madhalimu ni msingi mkuu katika aidiolojia ya Imam Khomeini (MA) jambo ambalo inabidi viongozi na wananchi wote wa Iran walizingatie sana wakati wote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja ufanikishaji wa kivitendo vya vipengee vya nakala ya kisiasa – kiraia ya Imam kuwa ni moja ya tofauti kubwa na zawazi zilizopo baina ya aidiolojia hiyo ya Imam na aidiolojia nyingine zinazoishia kwenye maneno tu na hapo hapo akauliza swali hili la kimsingi akisema: Je, kazi kubwa iliyofanywa na Imam kwa mafanikio makubwa, itaendelea?
Amejibu swali hilo kwa kusema ndio, lakini kwa masharti.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwa kusema: Katika jedwali jamali na lenye mvuto la Imam, kwa kawaida na mara zote kunakuwa na vyumba vilivyo wazi ambavyo upo uwezekano wa kuvijanaza na kuendelea na njia hii muhimu mno lakini kwa sharti la kufanya hima na kuwa na welewa wa kitaifa na kuchunga njia nzuri za kuvijaza vyuma hivyo.
Ayatullahil Udhma Khamenei amesifu uaminifu na utiifu wa taifa la Iran kwa malengo matukufu ya Imam Khomeini (MA) akisisitiza kuwa: Mwenendo uliooneshwa na taifa la Iran katika kipindi chote hiki cha miaka 25 ya tangu kufariki dunia Imam mtukukfu unaonesha kuwa vyomba vyote vitupu na vilivyo wazi katika jedwali hilo vitaweza kujazwa na kwamba chini ya kivuli cha kuendeleza njia ya Imam, Iran azizi kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu itafikia kwenye vilele vya juu kabisa vya nguvu na uwezo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kuwakhutubu hadhirina na mataifa yote akiyasisitizia nukta moja ya kimsingi kwa kusema: Kuendelea na njia ya Imam Khomeini (MA) na kufanikisha malengo matukufu ya mwanachuoni huyo, ni mfano wa kila lengo jingine muhimu, lazima kutakuwa na vizuizi na changamoto za kila namna ndani yake, na kama vizuizi na changamoto hizo hatutazitambua na kuziondoa, basi kuendelea na njia hiyo kutakuwa kugumu au hata kutakuwa hakuwezekani.
Hapo hapo Ayatullahil Udhma Khamenei ametaja changamoto mbili za nje na ndani na kusema kuwa ndizo changamoto kuu ambazo inabidi vijana, watu wenye ushawishi na vipaji, watoa nadharia na wasomi na wanafikra wa Iran wazizingatie na kuzipa uzito wa hali ya juu.
Ametoa ufafanuzi kuhusiana na changamoto za nje kwa kugusia usumbufu, kero na ukwamishaji unaofanywa na uistikbari wa kimataifa na hasa hasa Marekani na kuongeza kuwa: Tab’an baadhi ya wanafikra wa kisiasa wa Magharibi wanasema wazi kuwa, usumbufu na kero hizo hazina faida yoyote lakini pamoja na hayo Marekani bado inaendelea kutekeleza njama zake hizo kuu.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Wamarekani wamezigawanya nchi za dunia na mirengo ya kisiasa na shaksia mbali mbali ulimwenguni katika mafungu matatu, kundi la nchi zinazotii amri, kundi la tawala na mirengo ambayo hivi sasa inakwenda nayo pole pole na tawala na mirengo isiyokubali kuburuzwa.
Ameongeza kuwa: Marekani inaziunga mkono kikamilifu na kwa kila namna tawala na nchi ambazo zinatii amri zake na ambazo zimejisalimisha kwake na haishughulishwi na uovu unaofanywa na tawala hizo katika jamii ya kimataifa, tab’an kupitia uungaji mkono wake huu wa kila upande, Marekani inajali tu maslahi yake na kuzibebesha tawala hizo ufanikishaji wa maslahi yake hayo.
Kiongozi Muadhamu amegusia baadhi ya mifumo ya tawala za kiimla na za kidikteta kupindukia zinazoungwa mkono na Marekani akisema kuwa: Kuhusiana na nchi hizo ambazo ndani yake hakuna uchaguzi hata mmoja unaofanyika na wala wananchi wake hawana nguvu za kusema hata neno moja, Marekani inakwepa kuziita nchi hizo kuwa ni za kiimla na kidikteta na badala yake inaziita kuwa ni nchi zinazotawaliwa na mfumo dume (kwa sababu zinatii amri za Marekani).
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja kundi la pili la nchi zilizomo kwenye mgao wa Marekani kuwa ni nchi ambazo kutokana na kuwa na maslahi ya pamoja na Marekani, Washington imeamua kwenda nazo pole pole lakini wakati wowote inapopata fursa haichelei kushindilia jambia lake kwenye moyo wa nchi hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja nchi za Ulaya kuwa ni mfano wa wazi wa nchi hizo na kusisitiza kwamba: Tab’an licha ya kwamba Marekani inakwenda pole pole na nchi hizo za Ulaya kwa kulinda maslahi yake, lakini wakati huo huo inafanyia ujasusi maisha binafsi ya wananchi wa Ulaya na hata viongozi wa nchi hizo na inafanya hivyo kijeuri kiasi kwamba haiko tayari hata kuomba radhi.
Ameongeza kuwa: Tab’an nchi za Ulaya zimefanya kosa kubwa la kihistoria kwa kukubali kwao kutumikia manufaa na maslahi ya Marekani jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa na maslahi ya mataifa yao.
Ayatullahil Udhma Khamenei amelitaja kundi la tatu la nchi za dunia kwa mujibu wa mgao huo wa Marekani kuwa ni lile la nchi ambazo hazikubali kuburuzwa na ubeberu wa Marekani.
Amesisitiza kuwa: Siasa za Marekani kuhusiana na nchi hizo ni kutumia bila mipaka wala kikomo uwezo wake wote kuhakikisha kuwa inatoa pigo kwa nchi hizo na inazisambaratisha.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu njia zinazotumiwa na Washington dhidi ya nchi ambazo hazikubali kuburuzwa na Marekani akisema: Tab’an hivi sasa uvamizi wa kijeshi si kitu kinachopewa kipaumbele na Marekani kutokana na dola hilo la kibeberu kupata hasara kubwa katika uvamizi wake wa kijeshi kwenye nchi za Iraq na Afghanistan.
Ameongeza kuwa, stratijia nyingine kubwa inayotumiwa na viongozi wa Washington kuhusiana na nchi zinazoendesha mapambano na zisizokubali kuburuzwa na Marekani ni kutumia vibaraka wake katika nchi hizo na kuongeza kuwa: Kufanya njama za mapinduzi ya kijeshi au kuwashawishi wananchi wamiminike barabarani kupinga tawala za nchi hizo ni miongoni mwa mbinu kubwa zinazotumiwa na Marekani kupitia vibaraka wake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Serikali yoyote ile katika nchi yoyote ile inayoingia madarakani kwa kura za wananchi, lazima watakuweko watu wachache ambao hawakuipa kura zao serikali hiyo na ambao ni wapinzani wa serikali hiyo. Sasa Marekani inatumia suala hilo kuwachochea wapinzani hao kuwaingiza baadhi ya watu mitaani kupinga serikali hiyo.
Ameongeza kuwa: Mifano ya siasa hizo za Marekani zinaonekana kwa uwazi katika baadhi ya nchi za Ulaya. Tab’an sisi hatuhukumu chochote katika suala hilo lakini tunajiuliza, wale maseneta wa Marekani wanaoonekana kwenye maandamano ya mitaani katika nchi hizo za Ulaya wanafanya nini kwenye maandamano hayo yasiyowahusu?
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kuanzisha na kuyatia nguvu makundi ya kigaidi kuwa ni mbinu nyingine inayotumiwa na Marekani kukabiliana na nchi hizo zisizotii amri zake na ambazo hazikubali kuburuzwa na dola hilo la kibeberu.
Amesema: Iraq, Afghanistan na baadhi ya nchi za Kiarabu pamoja na Iran yetu azizi ni wahanga wakuu wa mbinu hiyo ya Marekani dhidi ya nchi hizo.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia uungaji mkono wa Marekani kwa kijigenge cha kigaidi cha wanafiki (MKO) na namna wanachama wa kigenge hicho cha kigaidi walivyo na uhusiano wa moja kwa moja na taasisi za utawala wa Marekani likiwemo Baraza la Congress la nchi hiyo na kuongeza kuwa: genge la kigaidi la wanafiki (MKO) ambalo limewaua kigaidi maulamaa, wasomi, na shakhsia wakubwa wa kisiasa na kiutamaduni pamoja na wananchi wengi wa Iran, linafanya vitendo vyake vya kigaidi chini ya uungaji mkono kamili wa Marekani.
Kiongozi Muadhamu amezitaja mbinu nyingine zinazotumiwa na Marekani dhidi ya nchi huru duniani ambazo hazikubali kuburuzwa kuwa ni kuzusha mizozo na mifarakano kati ya viongozi wa juu wa tawala za nchi hizo na kuzusha upotofu katika imani na itikadi za kidini za watu wa nchi hizo.
Ameongeza kuwa: Kwa taufiki na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, Wamarekani wameshindwa katika njama zao zote hizo mbele ya taifa la Iran na kwamba njama zao zote likiwemo jaribio la mapinduzi ya kijeshi, kuunga mkono wafanya fitna na wachocheaji wake, njama za kuwamimina barabarani baadhi ya wananchi na kuzusha ufa na hitilafu kati ya viongozi zote zimeshindwa kutokana na imani na mwamko wa taifa la Iran.
Baada ya kumaliza kubainisha changamoto za nje, Ayatullahil Udhma Khamenei ameanza kuzungumzia changamoto za ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisema: Changamoto hizo na hatari kubwa itatokea wakati taifa na viongozi wa Iran watakapouweka mbali na kuusahau moyo na misimamo ya mwamko wa Imam mtukufu.
Kuhusiana na suala hilo Ayatullah Khamenei ameashiria kufanyika makosa katika kumjua rafiki na adui na kushindwa kumtambua adui wa asili na adui asiye wa asili na kuongeza kuwa: Watu wote wanapaswa kuzingatia kuwa, hawapaswi kughafilika na adui mkuu na wa asili katika matukio yote.
Kiongozi Muadhamu ametoa mfano mmoja wa wazi wa kushindwa kumtambua adui wa kweli na asiye wa kweli kwamba ni vitendo viovu na vya aibu vya makundi yasiyojua kitu na ya kijahili ya Kitakfiri, Kiwahabi na Kisalafi dhidi ya Ushia na kusisitiza kuwa: Watu wote wanapaswa kuzingatia kuwa, adui mkuu ni mashirika ya kijasusi ya mabeberu na watu ambao wanayachochea makundi hayo kwa kuyapa fedha na silaha.
Ameongeza kuwa: Tab’an kila mtu atakayefikiria kuichokoza Jamhuri ya Kiislamu kwa hakika atapata pigo na majibu makali sana kutoka kwa taifa la Iran, lakini pamoja na hayo sisi tunaamini kuwa, mkono wa adui ambao haukujificha sana na ambao unawachochea Waislamu kuuana wao kwa wao ndiye adui yetu mkuu na wa asili na si haya makundi yaliyodanganywa yakadanyika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kupoteza mshikamano wa kitaifa, kukumbwa na uvivu na kutokuwa na mori wa kufanya kazi, kufanya kazi chache, kutawaliwa na uvunjikaji moyo na kukata tamaa na vile vile kuwa na fikra ghalati na potofu ya kudhani hatuwezi au kwamba huko nyuma pia hatukuweza, kuwa ni vipengee vingine vya changamoto za ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Kama ambavyo Imam wetu azizi alisema, sisi tunaweza na kwamba azma na nia ya kweli ya kitaifa pamoja na uongozi na usimamiaji wa mambo kijihadi utaweza kuondoa mikwamo yote na kutatua matatizo yote ya usoni.
Mwishoni mwa miongozo yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba: Jina lenye baraka la Imam mtukufu na mipango ya mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu italisaidia taifa la Iran katika hatua zote na kuiletea Iran azizi mustakbali unaong’ara kupitia kuleta matumaini, hamasa, mori na uchangamfu katika masuala yote.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Hasan Khomeini, amewakaribisha wafanya ziara na wapenzi wa mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu na kuzitaja jitihada za kuwaondolea shida watu na maeneo yaliyoko nyuma kimaendeleo, kuwasaidia wanyonge na kung’oa mizizi ya umaskini kwamba ndiyo yaliyokuwa malengo na shabaha kuu za Imam Khomeini (MA) na kuongeza kwamba: Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei pia siku zote amekuwa akiyapa umuhimu na sisitizo la kipekee malengo na shabaha hizo za Imam, na hilo ni somo kwa watu wote.
Mfawidhi wa Haram Tukufu ya Imam Khomeini (MA) vile vile ameutaja utatuzi wa matatizo ya kiuchumi kuwa unahitajia tadibiri, mantiki, ushirikiano mkubwa kati ya Mihimili Mitatu Mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) na umoja na mshikamano wa kitaifa.
Ameongeza kuwa: Uchumi inabidi ufungamane kikamilifu na utamaduni wa kupambana na umaskini na kubaki nyuma kimaendeleo.


No comments:

Post a Comment