Saturday 21 June 2014

MAZUNGUMZO KATI YA KHALIFA HARUN RASHID NA IMAM MUSSA ALKADHIM (a.s): Kuhusu Ahlulbayt wa Mtume (s.a.w)

Abu Ja’far Muhammad Bin Ali, mwenye lakabu ya Sheikh Saduq, katika karne ya nne hijiria., katika kitabu chake Uyun-e-Akbar ar-Ridha (vyanzo vikubwa vya Ridha), na Abu Mansur Bin Ali Tabarsi, katika kitabu chake Ihtijajj, anatoa maelezo kinaganaga ya mazungumzo ambayo yalifanyika kati ya Harun ar-Rashid na Imamu Musa Ja’far katika baraza la Khalifa. Khalifa alimuuliza Imamu: “Unawezaje kudai kwamba wewe ni dhuria wa Mtukufu Mtume? Mtume hana dhuria. Inakubaliwa kwamba dhuria ni kutoka upande wa kiume na sio upande wa kike. Wewe ni kizazi cha bint yake.”

Imamu akasoma Aya ya 84-85 kutoka Sura ya 6 ya Qur’ani Tukufu:
 “Na tukampa (Ibrahim) Is’haqa na Yakuub, wote tukawaongoa. Na Nuhu tulimuongoa zamani, na katika kizazi chake Daudi na Suleimani na Ayub na Yunus na Musa na Harun. Na hivi ndivyo tuwalipavyo wafanyao mema. Na Zakaria na Yahya na Isa na Ilyasa, wote walikuwa miongoni mwa watu wema.” (6:84-85)
Imamu akamuuliza Khalifa: “Ni nani aliyekuwa baba wa Isa?” Harun akajibu kwamba Isa alikuwa hana baba. Imamu akasema: “Kulikuwa hakuna yeyote aliyekuwa baba yake, na bado Allah alimjumuisha Isa katika dhuria wa mitume kupitia Mariamu. Hivyo hivyo ametujumuisha sisi katika dhuria wa Mtume kupitia kwa bibi yetu Bi Fatima.”
Aidha, Imamu Fakhur’d-Din Razi, katika kitabu chake Tafsir-e-Kabir, juzuu ya 4, uk. 124, anasema kuhusiana na aya hii kwamba, inathibitisha kwamba Hasan na Husein ni watoto wa Mtume wa Uislamu.
Kwa vile katika aya hii Mungu amemdhihirisha Isa kama kizazi cha Ibrahim, na Isa hana baba, uhusiano huu ni kutoka upande wa mama. Katika hali hiyo hiyo, Hasan na Husein ni dhuria wa kweli wa Mtume. Imamu Musa alimuuliza Harun kama anataka uthibitisho zaidi.
Khalifa akamuambia Imamu aendelee. Imamu akasoma Aya ya 61 kutoka Sura ya 3 ya Qur’ani Tukufu: “Watakao kuhoji katika haya baada ya kukufikia ilmu, waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu, na sisi na ninyi, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo,”
Aliendelea, akisema kwamba hakuna mtu hata mmoja ambaye amewahi kudai kwamba katika tukio hilo la maapizano (Mubahila) dhidi ya Wakiristo wa Najran kwamba Mtume alimchukuwa pamoja na yeye mtu yeyote isipokuwa Ali Bin Abi Talib, Fatima, Hasan na Husein.
Kwa hiyo tukiifafanua aya hii tutaona kwamba “sisi” (anfusana) maana yake ni Ali Bin Abi Talib. “Wanawake” (nisa’ana) maana yake Fatima na “Watoto” (abna’ana) maana yake Hasan na Husein, ambao Allah amewatambulisha kama watoto wa Mtume mwenyewe. Kwa kusikia
hoja hii, Harun aliguta, “Hongera, Ewe Abu’l-Hasan.” Kwa uwazi mantiki hii huthibitisha kwamba Hasan na Husein (watoto wa Bibi Fatima) ni watoto wa Mtukufu Mtume.

No comments:

Post a Comment