Kwa upande wa Shia, neno sahaba halina maana ya kistilahi kama
lilivyo kwa Sunni. Kwa hivyo wao hulitumia neno hili kama linavyotumika
kilugha.
Kwa mujibu wa lugha ya_Kiarabu (taz. Lisanul Arab na Mufradat
ar-Raghib chini ya neno 'sahaba'), neno sahaba ni wingi wa neno sahib. Na neno
sahib maana yake ni 'mwenye kuingiliana na kushikamana na (mwingine).' Wala neno
hilo 'hatumiliwi isipokuwa yule ambaye mshikamano wake (na mwenziwe) ni mwingi.' Na ili kuwa sahib wa
mtu yahitajia 'kukaa naye kwa muda mrefu.' Pia kwa kuwa suhba (usahibu) huwa ni
baina ya wawili, neno hili — katika sentensi—siku zote huunganishwa na jina
moja au jingine; na hivyo ndivyo lilivyotumiwa katika Our'ani Tukufu: k.m.
sahibayis sijn (Sura 12:39) na as'habu Musa (Sura 26:61); na katika zama za
Bwana Mtume s.a.w.w. pia: k.m. sahibu rasulillahi au as'haburasuli llahi.
Kwa hivyo kwa Shia 'sahaba wa Mtume s.a.w.w.' ni yule anayetimiza
yaliyotajwa katika taarifa ya neno hilo hapo juu.
Daraja yao
Baada ya kuona jinsi taarifa ya neno sahaba inavyotofautiana,
baina ya Sunni na Shia, tumebakiwa na swali moja; nalo ni: jee, wote ni
waadilifu? Wote wamehifadhiwa na kufanya makosa?
Majibu ya Sunni hapo ni: Ndiyo; sahaba wote ni waadilifu, na wote
wamehifadhiwa na kufanya makosa. Hivyo ndivyo anavyotwambia Sheikh M. al-Khatib
katika kitabu chake.
Lakini Shia wasema: La; sio hivyo. Na wana hoja zao ambazo, japo
kwa muhtasari, tumezidondoa katika mjadala huu, na ambazo tafadhali zitazame na
uzizingatie. Juu ya hoja hizo, kuna na nyingine mbili:
(i) imani hiyo inapingana na misingi
inayoelezwa katika Qur'ani Tukufu kuhusu wale waliokuwa karibu zaidi
na Mitume wa Mwenyezi Mungu kwa jumla kuliko sahaba zao, na Mtume Muhammad
s.a.w.w. hasa kuliko sahaba zake; na
(ii) inapingana na maumbile ya Binadamu yalivyo.
Inavyopingana na Qur'ani Tukufu
Tunapozingatia kwa makini taarifa ya Kisunni, tunaona
kwamba kitu cha pekee kililchofanya sahaba wapawe daraja waliyopawa ya
utakatifu, na kuhifadhiwa na kufanya makosa, ni kule kuwa karibu na Mtume
s.a.w.w. na kuweza kumwona-japo ni kwa mbali! Hakuna jingine.
Kama ni hivyo basi, hilo halitoshi. Maana tunapoisoma Qir'ani
Tukufu tunaona watu waliokuwa karibu zaidi na Mtume Muhammad s.a.w.w. kuliko
walivyokuwa sahaba zake kwake, na hata wale wa Mitume wengine, na bado Mwenyezi
Mungu hakuwapa daraja ambayo sahaba wamepawa na kina Sheikh M. al-Khatib! Bali
tunaona jinsi wanavyo onywa na kukemewa! Kwa mfano:
(i) tunapofungua Sura 11:45-46, tunasoma: 'Nuhu akamlingana Mola
wake. Akasema: Mola wangu! Hakika mtoto wangu ni katika watu wangu; na hakika
ahadi Yako ni kweli, na Wewe ni Mbora wa wenye kuhukumu. (Mwenyezi Mungu)
akasema: Ewe Nuhu! Hakika huyo si katika watu wako. Yeye ni (mwenye) mwendo
usiokuwa mwema. Basi usiniombe usilokuwa na ujuzi nalo. Mimi nakunasihi usiwe
miongoni mwa wajinga.'
Jee, kama mkuruba tu na Mtume wa Mwenyezi Mungu ndio unaompa mtu
utakatifu, yuko aliye karibu zaidi kuliko mtoto wa kumzaa mwenyewe? Mbona hapo
Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume Wake, Nuhu a.s., kwamba huyo mtoto wake si
miongoni mwa watu wake? Kama mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu aweza kuambiwa
kuwa hayumo miongoni mwa watu wake, kwa sababu tu amemwasi babake, vipi
tunawapa utakatifu sahaba (hata kama maasia yao yamethubutu) kwa sababu tu
walimwona Bwana Mtume s.a.w.w.? Jee, aliyetokana na damu ya Mtume wa Mwenyezi
Mungu, na aliyemwona tu, yupi yuko karibu naye zaidi?
Pengine wanafunzi wa Mawahhabi watatwambia kuwa mtoto wa Nabii
Nuhu a.s. alikuwa kafiri. Kwa hivyo si sawa kumlinganisha na sahaba waliokufa
wakiwa Waislamu. Sawa! Jee, Mwana Fatima, binti ya Mtume Muhammad s.a.w.w.?
Hakuwa Mwislamu? Hakumwona Bwana Mtume s.a.w.w.? Hakufa katika Uislamu? Kama
alikuwa na yote hayo, juu ya kuwa alikuwa kipenzi cha babake, kwa nini babake
s.a.w.w. akamwambia (kama tuelezwavyo katika Hadith mashuhuri): 'Niombe
unachotaka katika mali yangu. Lakini, kwa Mwenyezi Mungu, mimi sitokufaa kitu'?
Au kwa nini Bwana Mtume s.a.w.w. kusema: 'Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Lau Fatima
binti Muhammad angaliiba, ningalimkata mkono wake'? Jee, hayo yote si kuonyesha
kwamba kuwa karibu na Mtume wa Mwenyezi Mungu peke yake hakutoshi, kama
hakukuandamana na amali njema? Kama Mwana Fatima a.s. anaambiwa kwamba
kitakachomfaa kwa Mola wake ni amali yake, na kwamba akiasi ataadhibiwa, vipi
na kwa kipimo gani tunawapa utakatifu huo sahaba kwa sababu tu walimwona Bwana
Mtume s.a.w.w.? Na hata kama maovu ya baadhi yao yamethubutu?
(ii) tunapofungua Sura 66:10-11, tunasoma: 'Mwenyezi Mungu amepiga
mfano wa wale waliokufuru -mke wa Nuhu na mke wa Luti. Walikuwa chini ya waja
Wetu wawili wema miongoni mwa waja Wetu; lakini (wanawake hao) wakawafanyia
hiana hao (waume zao), na wao (hao waume) hawakuweza kuwafaa chochote kwa
Mwenyezi Mungu. Pakasemwa: Uingieni Moto pamoja na wenye kuuingia. Na Mwenyezi
Mungu amepiga mfano (mwingine) wa wale walioamini mke wa Firauni; pale
aliposema: Mola wangu! Nijengee Kwako nyumba katika Pepo, na uniokoe na Firauni
na vitendo vyake (viovu), na uniokoe na watu madhalimu.'
Haya! Hao hapo wake wawili wa Mitume wa Mwenyezi Mungu: Nabii Nuhu
a.s. na Nabii Luti a.s. Kwa sababu hawakuwa na mwendo mzuri, ukuruba wao na
Mitume hao haukuwafaa kitu, bali watatiwa Motoni! Sasa ikiwa ni hivyo kwa wake
wa Mitume, kwa nini tuambiwe haiwi hivyo kwa rafiki (sahaba) zao?
Kwa nini tuambiwe tusiwatuhumu sahaba kwa ubaya hata kama
wamefanya ubaya? Angalia kwenye aya hizo jinsi Mwenyezi Mungu alivyomhukumu kwa
wema mke wa mtu mwovu mno (Firauni), akawahukumu kwa uovu wake wa watu wema mno
(Mitume)! Yote hayo ni kutuonyesha kwamba kuwa karibu na mtu mwema hakufai kitu
kama wewe mwenyewe si mwema, kama ambavyo kuwa karibu na mtu mwovu hakudhuru
kitu kama wewe mwenyewe si mwovu. Na hivyo ndivyo inavyotakikana tuwapime
sahaba wa Bwana Mtume s.a.w.w. Wale waliothubutu kuwa ni wema, tuwape haki yao.
Na wale waliothubutu kuwa ni waovu, tuwape stahili yao. Hivyo ndivyo Kishia, na
ndivyo ki-Qur'ani, kama tunavyoona. Maana kama ukuruba peke yake haukuwafaa
watoto na wake za Mitume wa Mwenyezi Mungu, walio karibu zaidi nao, vipi
utawafaa sahaba zao kwa sababu tu waliwaona?
No comments:
Post a Comment