Friday 12 September 2014

ELIMU MIONGONI MWA WAARABU KABLA YA UISLAMU

Miongoni mwa Waarabu walikuweko watu wachache sana walioweza kusoma na kuandika. Wengi wao hawakuwa na shauku sana ya kujifunza fani hizi. Baadhi ya wanahistoria wana maoni kwamba elimu ya watu ya wakati ule takriban ilikuwa ya simulizi tu. Wayahudi na Wakristo walikuwa ndio watunzaji wa elimu kama hiyo ambayo Arabia ilikuwa nayo.
Elimu ya taaluma kubwa kamilifu ya wapagani wa Kiarabu ilikuwa ni ushairi wao. Walidai kwamba Mungu alijaalia Ubora usiokifani, wa kichwa, juu ya Wagiriki (ushahidi wake ni sayansi na falsafa yao); wa mikono, juu ya Wachina (ushahidi wake ni ufundistadi wao); na wa ulimi kwa Waarabu (ushahidi wake ni ufasaha wao). Fahari yao kubwa, nyakati zote kabla na baada ya Uislamu, ilikuwa ni ule ufasaha wao katika ushairi. Umuhimu wa mashairi unatathminiwa kama ifuatavyo:
(Arabs, Islam and the Arab Caliphate in the Early Middle Ages, 1969)
Mashairi ya Kiarabu yalikuwa na utajiri katika ufasaha na matumizi ya tamathali za usemi katika mazungumzo au maandishi, lakini yalikuwa na ukomo wa masafa, na yalikuwa na upungufu wa maana. Maneno yaliyomo yaweza kuwa ya kuvutia lakini yalikuwa chapwa! Kazi bora za mashairi yao takribani hufuatia kabisa utaratibu uleule wa fikira na mawazo. Hata hivyo yalikuwa ni kioo cha uaminifu katika maisha ya zamani ya uarabuni. Vile vile katika kuchimbua sanaa ya ushairi, washairi wa kiarabu kwa hadhari walikuwa wakiendeleza moja ya sanaa kubwa za binadamu - lugha ya Kiarabu.
Utungaji mkubwa wa mapagani wa Kiarabu ni ule ulioitwa "Golden Odes", mkusanyiko wa mashairi saba, yakidhaniwa ya ubora usiopitwa, yenye nguvu na ufasaha. Yalitundikwa ndani ya Al-Kaaba kama changamoto kwa yeyote mwenye kutamani kuyapita au kulin-gana nayo. Sir William Muir anaandika kuhusu mashairi Haya kama ifuatavyo:
"Mashairi saba yaliyotundikwa yalikuwa hai kuanzia hata kipindi kilichomtangulia Muhammad, kielelezo cha kushangaza cha ufasaha usio hila. Uzuri wa lugha na utajiri wa kuenea haraka wa matumizi ya tamathali za usemi katika mazungumzo na maandishi unakubaliwa na wasomaji wa ulaya, lakini somo la mshairi liliwekewa ukomo, na yale yasiyo ya kawaida yalikengeukwa.
Haiba ya kimada wake, baka la kuonewa wivu lililowekwa na dalili za karibuni za kambi yake, na upweke wa makazi yake (huyu kimada) yaliyotelekezwa, ukarimu na ushujaa (wa mwenye kimada), heshima isiyo na upinzani wa kabila lake, sifa nzuri za ngamia wake - hizi zilikuwa ndio mada ambazo, pamoja na tofauti ndogo katika utendaji, na bila hila yoyote ya njama au Hadith, zilitawala ndoto za Mwarabu - na baadhi ya hizo ziliongeza mafuta kwenye mazoea mabaya ya kudumu ya watu, makuu, uhasidi, kisasi na majivuno."
(The life of Mohammed, 1877)
Pamoja na kutokeza kwa Uislamu, msisitizo ulihamishwa kwa muda, kutoka ushairi kwenda nathari na ushairi ukapoteza nafasi yake ya ukubwa na hadhi kama vile "Malikia" wa sanaa za Arabuni. "Utungaji" mkubwa wa Uislamu ulikuwa ni Qura'n Tukufu, Kitabu cha Uislamu na kilikuwa katika nathari. Waislamu huamini kwamba Qur'an "iliandikwa" Mbinguni kabla ya kuteremshwa kwa Muhammad, Mjumbe wa Mungu.
Wanaamini kwamba kipaji cha mwanadamu kamwe hakiwezi kutoa kitu chochote ambacho kinaweza kulingana na mtindo wake au yaliyomo ndani yake. Kwa vizazi kumi na tano vilivyopita, imekuwa kwao mtindo wa maandishi, filosofia, theologia, sheria, metafisikia na mawazo ya kimafumbo.
Hii, inaonyesha kwamba Arabia kabla ya Uislamu ilikuwa haina vistawishi vya kijamii au historia ya kina, na Waarabu waliishi katika taflisi ya maadili na utumwa wa kiroho. Maisha kwao yalikuwa hayana maana, lengo na mwelekeo. Moyo wa ubinaadamu ulikuwa kwenye minyororo, na ulikuwa ukisubiri, kama ilivyokuwa, ishara ya kufanya jitihada kubwa mno, ya kujinasua na kuwa huru.
Ishara hiyo ilitolewa mwaka 610 A.D. na Muhammad, mwana wa Abdillah, katika mji wa Makka, alipotangaza ujumbe wake wa Utume, na akaanzisha harakati iliyoitwa Uslamu katika kazi yake ya kuzunguka dunia.
Uislamu ulikuwa ndio neema kubwa kwa mwanadamu daima uliwaweka huru wanaume na wanawake, kupitia utu kwa Muumba wao, kutokana na utumwa katika udhahiri wowote. Muhammad, Mtume (s.a.w.) wa Allah. (s.w.t.) alikuwa ndio mkombozi mkuu wa wanadamu. Yeye alimnasua mwanadamu kutoka kwenye "Mashimo ya Maisha"
Peninsula ya Arabia ki-jiogorafia ilikuwa pembezoni na kisiasa, eneo lisilojulikana mpaka mwanzoni mwa karne ya saba A.D. Ni wakati huo ambapo Muhammad (s.a.w.) alipoiweka kwenye ramani ya kisiasa ya dunia kwa kuifanya uwanja wa matukio ya maana sana ya historia.
Kabla ya Uislamu, Waarabu walishika nafasi ya pembeni tu katika historia ya Mashariki ya kati, na wangebaki daima taifa la watu wanaodhani kila kitu kina roho, na wachunga kondoo kama Muhammad (s.a.w.) asingewapatia kiini na kichocheo kilichoyaunganisha makabila yao ya kihamajihamaji yaliyokuwa yametawanyika, kwa nguvu yenye kujiendesha, yenye lengo maalum. Alitengeneza "taifa" kutoka kwenye bonge lenye mashimoshimo lisilokuwa na umbo la msingi. Aliwapamba Waarabu na nguvu mpya, udhanifu na kipaji cha ubunifu, na walibadili mwelekeo wa historia.
Alianzisha elimu ya viumbe na mazingira ya akili na falsafa mpya kabisa, na kazi yake iliweka kipindi cha waziwazi katika historia ya ulimwengu; na ilikuwa ni mwisho wa enzi moja na mwanzo wa nyigine.
Pamoja na kazi hii kubwa aliyoifanya Mtume wetu bado kuna watu ambao leo wanachukia kusoma na kupata elimu ya kimazingira na sayansi kwa madai kuwa ni ukafiri. Mfano wa makundi yenye watu wa aina hii ni Boko Haramu ya Nigeria ambali limeua watu wengi kwa kosa tu kwenda shule kusoma. Huu ni msiba kwa ulimwengu mzima wa kiislamu na ni harakati za wanafiki kuturudisha nyumba waislamu.

No comments:

Post a Comment