Friday, 12 September 2014

JUHUDI ZA KUPUNGUZA MIGOGORO BAINA YA MADHEHEBU YA KIISLAMU

Katika karne hii, kiasi cha miaka thelathini hivi iliyopita, baadhi ya wanazuoni wa Kishia na wasio Shia huko Mashariki ya Kati wakaona la! Hali hii ya mizozo haifai kuachwa ikaendelea. Kwa hivyo wakakutana na kujadiliana jinsi ya kuleta mkuruba na uelewano baina ya madhehebu mbali mbali ya Kiislamu - hasa baina ya Shia na Sunni. Matokeo yake yakawa ni kuundwa chama kilichoitwa Darut Taqrib Baynal Madhahibil Islainiyya na kuweka jukwaa la pamoja la kuwawezesha wanazuoni hao wa madhehebu mbali mbali kueleza imani na misimamo ya madhehebu yao juu ya mada mbali mbali za kidini.
Hatua hii ilisaidia sana kuleta uelewano kiasi cha kwamba, Sheikh Mahmud Shaltut (aliyekuwa Mufti wa AI-Azhar wakati huo) alitoa ile fatwa yake mashuhuri ya kusema kwamba madhehebu ya Ja'fari (yaani Shia Ithnaashari) ni madhehebu ya Kiislamu yanayojuzu kufuatwa katika kufanyia ibada kama madhehebu mengineo ya Sunni. Na, kwa mara ya kwanza akaruhusu madhehebu hayo yasomeshwe katika Chuo Kikuu hicho cha AI-Azhar huko Misri.
Hata hivyo, baadhi ya masheikh wa wakati huo hawakupendezwa na hatua hiyo. Miongoni mwao ni mmoja aliyekiitwa Muhibbudin al-Khatib. Huyu aliandika kitabu kwa lugha ya Kiarabu kiitwacho al-Khututul Aridhwa kuonyesha kwamba ni muhali jaribio hilo la wanazuoni wenzake kufanikiwa - hasa inapokuja kwenye uelewano baina ya Sunni na Shia - na akatoa sababu zake. Sababu hizo ndizo wanazotumia baadhi ya watu wapenda shari kuushambulia Ushia. Katika mada zifuatazo nitaonesha udhaifu na uongo wa hoja hizo za Alkhatib.

No comments:

Post a Comment