Katika karne ya tano (A.D). mtu aliyeitwa Qusay, alizaliwa katika kabila la Quraish. Alipatia heshima kubwa na umaarufu kwa kabila lake kwa ajili ya hekima zake. Aliijenga upya Al-Kaaba iliyokuwa katika hali ya kukatisha tamaa, na aliwaamuru Waarabu kujenga nyumba zao kuizunguka. Alijenga pia "ukumbi wa mji" wa Makka, wa kwanza katika Arabia. Viongozi wa koo mbalimbali walikusanyika katika ukumbi huu kutafakari juu ya maswala yao ya kijamii, kibiashara, kiutamaduni na kisiasa. Qusay aliunda sheria juu ya kugawa chakula na maji kwa Mahujaji waliokuja Makka, na aliwashawishi Waarabu kulipa kodi kwa ajili ya msaada wa huduma zao.
Edward Gibbon anasema:
"Qusay, aliyezaliwa takriban A.D. 400, ni babu yake mkubwa Abdul-Muttalib, na hivyo wa tano katika kizazi cha kupanda toka Muhammad, alipata mamlaka makubwa huko Makka.
(The decline and Fall of the Roman Empire)
Qusay alifariki mwaka 480 A.D., na mwanae, Abd Manaf, alitwaa madaraka ya kazi zake. Na yeye pia alijipatia sifa kutokana na uwezo wake. Alitambulika kwa ukarimu wake na maamuzi yake mazuri. Alifuatiwa na mwanae Hashim. Ni huyu Hashim aliyeupa ukoo wake jina lake uliokuja kuwa maarufu katika historia kama Bani Hashim. Hashim alikuwa ni mtu wa namna ya pekee. Alikuwa ni yeye aliyewafanya Maquraishi kuwa wafanyabiashara na wakawa wafanyabiashara bora. Alikuwa ndiye mtu wa kwanza kuanzisha zile safari mbili za misafara ya Maquraish, ya kiangazi na kipupwe, bila yeye, Waarabu wangeweza kubakia wachunga kondoo daima.
No comments:
Post a Comment