Friday 12 September 2014

HISTORIA YA MADHEHEBU YA AHLU-SUNNA, MWANZO WAKE NA CHIMBUKO LAKE:

HISTORIA YA MADHEHEBU YA AHLU-SUNNA, MWANZO WAKE NA CHIMBUKO LAKE:
Maulamaa na wanazuoni wa Kisunni wametofautiana kuhusiana na chimbuko la madh-hebu hii ya Ahlu-sunna, kwamba ni lini hasa ilianza madh-hebu hii au ni nani haswa mwasisi wake?!. Zimekuwapo fikra na rai mbali mbali kwa wanazuoni hao kunako hilo.Tunazitaja kama ifuatavyo:
1- Baadhi yao wamesema kwamba: Chimbuko la Madh-habu hii lilikuwa ni katika zama za uhai wa Mtume (s.a.w.w), na kwamba Muasisi wa Madh-hebu hii ni Mtume mwenyewe (s.a.w.w). Kwa mujibu wa rai hii, ina maana madhehebu zote zilizobaki (tofauti na madh-hebu ya Ahlu-sunna) hazikuwepo zama za Mtume (s.a.w.w), hivyo zitakuwa ni Madh-hebu zilizokwenda kinyume na kupotea na hazina itibari yoyote. Kunako rai hii unaweza kurejea kitabu kiitwacho:
{Itiqadi Ahlu-sunna As-habul-Hadithi, ukurasa wa 11}.
2- Wakasema wanazuoni wengine (hao hao wa kisunni) kuwa: Fikra na Rai ya kwanza sio sahihi kuhusu chimbuko la Ahlu-sunna, bali ukweli ni kwamba: Madh-hebu hii ya Ahlu-sunna chimbuko lake ni siku ile aliyofariki Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambapo kundi kubwa la waislaam (Maswahaba) waliungana na Abubakar bin Kuhafa na kumchagua kuwa Khalifa, na kundi lingine la pili la maswahaba likaungana na Imam Ali bin Abiu Twalib (a.s) na watoto wake Imam Ali (a.s), nalo ni kundi lile ambalo halikwenda katika ukumbi wa Saqifa kuchagua nani atakuwa Khalifa baada ya Mtume (s.a.w.w) bali kundi hili lilibakia nyumbani kwa Mtume (s.a.w.w) likiwa pamoja na Imam Ali bin Abi Talib (a.s) kwa ajili ya shughuli nzima ya kuuosha mwili Mtukufu wa Mtume (s.a.w.w), kuuvalisha sanda, na maandalizi yote kwa ujumla ya kimazishi.
Hao ndio waliokataa Ukhalifa wa Abubakar na kusema hasitahiki kuwa Khalifa isipokuwa Imam Ali bin Abi talib (a.s) maana huyu ndiye aliyeteuliwa na Mtume (s.a.w.w) na wakasema Khalifa hachaguliwi na waislaam bali anachaguliwa na Mwenyeezi Mungu (s.w) kupitia kwa Mtume wake (s.a.w.w). Wakapinga uchaguzi huo wa ukhalifa kwa Abubakar na kusema si jukumu la waislaam kuchagua Khalifa maana Mtume tayari kaisha teua khalifa baada yake na huyo ndiye tunayetakiwa kumfuata na kurejea kwake baada ya Mtume (s.a.w.w).
Hivyo Masahaba wakagawanyika makundi pande mbili, wanaokubali ukhalifa wa Abubakar kuwa ndio khalifa maana watu wamemchagua, na upande mwingine wa maswahaba ukawa kwa Imam Ali (a.s) na kuthibitisha ukhalifa wake ukisema upande huu kuwa: Khalifa ni yule tu aliyechaguliwa na Mtume (s.a.w.w) katika uhai naye ni Imam Ali bin Abi Talib (a.s). Tangu hapo ndipo likachimbuka jina la Ahlusunna na Shia, kwamba:
Wale Maswahaba waliokuwa upande wa Abubakar na kumchukulia kuwa yeye ndiye Khalifa walijulikakana rasmi kama {Ahlu-sunna} na wale Masahaba waliokuwa upande wa Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) wakifuata hadithi za Mtume (s.a.w.w) za kumteua Ali kuwa wasii wake na khalifa baada yake, wakajulikana kama {Mashia au wafuasi wa Ali bin Abi Talib (a.s). Kuhusu rai hii unaweza kurejea katika kitabu kiitwacho:
(Min Hayat Al-khalifatu Abi bakari, cha Allama, Sheikh Abdul-Hasani Al-amini, ukurasa wa 30).
3- Rai ya tatu ya wanazuoni wa kisunni kunako chimbuko la Ahlu-sunna inasema:
Madh-hebu ya Ahlu-sunna chimbuko lake si katika zama za uhai wa Mtume (s.a.w.w) na wala sio siku ile aliyofariki Mtume Muhammad (s.a.w.w), bali ukweli halisi ni huu kwamba: Madh-hebu hii imeasisiwa baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w), na kwamba Mtume (s.a.w.w) hajaacha kitu kinachoitwa Ahlu-sunna wal-jamaa, bali istilahi hiyo ya Ahlusunna imezuka au imeasisiwa au imechimbuka katika zama za Ukhalifa wa Muawia bin Abi Sufiyani, yeye (yaani Muawia) ndiye mwanzilishi wa neno hili Ahlu-Sunna, na alianzisha neno hilo au istilahi hiyo pale alipofanya sulhu na Imam Hasan bin Ali bin Abi Talib (a.s) ambapo baada ya sulhu iliyojiri baina ya Imam Hasan (a.s) na Muawia, alisimama Muawia na kutangaza akisema: Hii ni Sulhu ya Ahlu-sunna Wal-jamaa, nayo ni ile Suhlu iliyofanyika baina ya Masunni hao na wafuasi wa Ahlu-bait (a.s) ambao wakati wa zama hizo za Muawia walikuwa wakimtawalisha Imam Hasan (a.s) na kuthibitisha kuwa yeye ndiye Khalifa wa Pili baada ya Imam Ali bin Abi Talib (a.s).
N/B: Rai ya hii ndio rai yenye uzito zaidi maana ndio inayothibitisha kiusahihi chimbuko au mwanzilishi wa Istilahi hii ya Ahlu-sunna. Hivyo Istilahi haikuwepo zama za uhai wa Mtume (s.a.w.w) na hata baada ya Kifo cha Mtume (s.a.w.w) haikuwepo mpaka pale Muawia alipokuwa Khalifa ndio akaja na Istilahi hii ya Ahlu-sunna wal-jamaa katika tukio hilo tulilolitaja sehemu hii (ya sulhu).
Kunako rai hii unaweza kurejea kitabu kiitwacho:
As-saqifa Ummul-Fitna, cha Jawad bin Jaafar Al-khalili, ukurasa wa 17.
4- Rai ya nne na ya mwisho inayotolewa na wanazuoni wa kisunni inasema hivi:
Madhehebu ya Ahlu-sunna imepatikana kutokana na juhudi za maulamaa wakubwa wa Ahlu-sunna (yaani: Maulamaa wakubwa wa Kisunni) kama vile: ABU HANIFA, MALIK BIN ANAS, IMAM SHAFI, HANBALI, ABU MUSA AL-ASH-ARI na wengine.

No comments:

Post a Comment