Friday 12 September 2014

UMUHIMU WA KUJIFUNZA AKIDA ZA MADHEHEBU MBALIMBALI.

Ni jambo lililo wazi na lisilopingika kuwa; dini ya Kiislamu mfano wa dini nyengine ina madhehebu tofauti, na kila dhehebu lina sifa zake katika mambo ya akida na namna ya utendaji wa amali kutokana na akida hizo wanazoziamini, lakini tofauti hizo sio kubwa kiasi ambacho pasiwe na uwezekano wa kutoshirikiana baina ya wafuasi wa dhehebu fulani na wafuasi wa dhehebu jingine, bali wafuasi hao wa madhehebu tofauti wanaweza kushirikiana na kukabiliana na fikra za watu wa kimagharibi ili kuondoa kasumba au tata zinazotolewa na watu hao kwa ajili ya kuiharifu, basi waislamu inawapasa kuihifadhi dini yao na kutowaruhusu watu hao wenye fikra hizo mbovu kufanikiwa katika malengo yao ya kuiharibu dini hiyo takatifu.
Kwa hakika kuleta mashirikiano hayo kunahitajia kutunzwa au kuadhimishwa misingi na vigezo vya kila madhehebu, na jambo la muhimu zaidi ambalo linafaa kutekelezwa ni kuwa; kila dhehebu ni lazima litambue akida ya dhehebu jingine, kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kuzuia khitilafu zilizopo baina ya dhehebu na dhehebu, na kupatikana njia zitakazoweza kuleta mashirikiano.
Njia bora inayoweza kuyafanya madhehebu kufahamiana ni kutambuana kupitia misingi ya dini yao ya Kiislamu, na kutambuana akida zao kupitia maulamaa wao maarufu waliobobea kielimu na wanaotambulika katika jamii, kwa sababu ikiwa watafahamiana akida zao kupitia wafuasi wa madhehebu yao, wafuasi ambao hawana elimu ya kutosha inayohusiana na akida zao, na wafuasi wa madhehebu tofauti wakajenga uadui na kuwekeana chuki kutokana na ikhitilafu walizonazo, hapana shaka uadui na chuki hizoz itafunga na kuzuia njia zitakazowapeleka katika mashirikiano, na mafahamiano au mashirikiano yatabadilika na kuwafanya waislamu hao watengane kutokana na tofauti zao za kiakida na kiamali.
Hivyo ni lazima tujue akida ya Historia ya kila madhehebu kupitia kwa wenye madhehebu yao badala ya kujifunza madhehebu Fulani kupitia kwa adui yao. Tukijuana tutaheshimiana na kupendana kama waislamu.

No comments:

Post a Comment