Friday, 12 September 2014

KUZALIWA KWA MUHAMMAD (S.A.W.W) NA MIAKA YA MWANZO YA UHAI WAKE

KUZALIWA KWA MUHAMMAD (S.A.W.W) NA MIAKA YA MWANZO YA UHAI WAKE
Abdullah alikuwa ndiye mtoto kipenzi cha Abdul Muttalib.
Alipokuwa na umri wa miaka kumi na saba, alimuoa Amina, bibi wa uzao bora wa Yathrib, mji ulioko Kaskazini ya Makka. Hakuwa hata hivyo, amekadiriwa kuishi muda mrefu, na akafa miezi saba tu baada ya ndoa yake.
Muhammad, Mtume wa Mungu wa wakati ujao, alikuwa bado mimbani. Sheikh Muhammad el-Khidhri Buck, profesa wa historia ya Kiislamu, chuo kikuu cha Misri, Cairo, anasema katika kitabu chake, Nur-ul-Yaqin fi-sirat Sayyid al-Murasalin (1953) hivi:
"Yeye (Muhammad Ibn Abdullah) alizaliwa katika nyumba ya ami yake, Abu Talib, katika "mtaa wa Bani Hashim" huko Makka, tarehe 12 Rabil-awal y ule Mwaka wa Tembo, tarehe ambayo inaoana na tarehe 8 Juni 570. Mkunga wake alikuwa ni mama yake Abdur Rahmani Ibn Auf. Mama yake, Amina, alituma habari za uzazi huu wa kheri kwa babu yake, Abdul Muttalib, ambaye alikuja, akamchukuwa mikononi mwake, na akampa jina hili la Muhammad."
Mgao wa Muhammad katika urithi wake ulikuwa ni mtumwa mmoja wa kike, Ummu Ayman; ngamia watano na kondoo kumi. Huu ni ushahidi kwamba Mitume wanaweza kurithi mali, na kama wanaweza kurithi mali toka kwa wazazi wao, wanaweza pia kurithisha mali kwa watoto wao wenyewe. Kuwa mitume hakuwabatilishii wao katika kupokea urithi wao wenyewe wala hakuwabatilishii watoto wao kupokea wa kwao. Kauli hii inaweza kuonekana kama isiyofuata mantiki katika muktadha huu lakini sio. Muhammad, Mtume wa Uislamu, alitoa kwa mwanae, Fatima kama zawadi, shamba la Fadak.
Lakini alipofariki; Abu Bakr, aliyekuwa Khalifa, na Umar, Mshauri wake, walilikamata shamba hilo kwa kisingizio kwamba Mitume hawarithishi mali yoyote kwa watoto wao wenyewe, na mali yeyote wanayomiliki, inahusika baada ya kifo chao, sio kwa watoto wao, bali kwa umma wao. Ni faini kali ambayo mtu anapaswa kulipa katika Uislamu kwa kuwa tu mtoto au binti wa Mtume wake. Mtu mwingine yeyote katika umma huu anayo haki ya kurithi utajiri au mali ya baba yake lakini sio binti wa Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t.)!

No comments:

Post a Comment